Profesa Lipumba: 'Rais' bora anayekosa kura za kutosha


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 10 November 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

SIKU moja niliota ndoto kwamba mimi ni mpiga kura wa mwisho katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania. Kabla ya kwenda kupiga kura yangu tayari niliambiwa kwamba wagombea urais wamefungana kwa kura.

Wagombea hao ni waliowania urais katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu. Kwenye ndoto, nikafahamishwa kwamba yeyote nitakayempigia, ndiye hatimaye atakuwa rais wa nchi hii.

Televisheni na redio zote zikaelekeza macho kwangu. Taifa zima likasimama kwa dakika moja. Nikachukua karatasi ya kupiga kura. Na nikajua mapema kwamba kuna mgombea mmoja tu ambaye angepata kura yangu siku hiyo.

Kura yangu nikampa mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba. Na niseme wazi, hata nje ya ndoto hiyo, nisingefanya kitu tofauti na hicho.

Kura yangu kwa Prof Lipumba haimaanishi kwamba mimi ni mwana CUF. Kwa bahati mbaya au nzuri, hili linategemea na maoni binafsi ya mtu—sijawahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.

Nimebahatika kumfahamu Profesa Lipumba kwa karibu. Ninaweza kukiri hapa kwamba pengine ni mgombea urais ninayemfahamu zaidi kuliko wagombea wengine wote wa urais waliowania nafasi hiyo katika uchaguzi huu uliopita ambao Jakaya Kikwete aliibuka mshindi.

Ninashukuru kwamba kwa kazi yangu ya uandishi wa habari, nimeweza pia kufahamiana na aliyekuwa mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.

Kwa kiasi nimemfahamu mgombea wa CCM, Rais Kikwete. Kwa kuwafahamu wote hao, kwa sifa zao zote, kila mara nimekuwa na maoni kwamba Lipumba angeweza kuwa rais mzuri kuliko wawili hao. Hayo ni maoni.

Kuegemea kwangu kwa Prof. Lipumba kunatokana na sera zake za kiuchumi. Kati ya wagombea wote wa urais, hakuna anayeweza kueleza ni kwa vipi Tanzania inaweza kuendelea kiuchumi kwa miaka michache kuliko yeye.

Prof. Lipumba ni mchumi wa kiwango cha juu. Katika mazungumzo yangu naye, mara nyingi nimekuwa nikishangazwa na aina ya wachumi wanaoheshimika duniani ambao amewahi kufanya nao kazi kama mchumi.

Prof. Lipumba ama amewahi kusoma nao, kufanya nao kazi au kufundisha katika chuo kimoja na magwiji wa uchumi wa kizazi cha sasa duniani.

Anamfahamu vizuri Profesa Joseph Stiglitz, aliyekuwa mshauri wa uchumi wa Rais Bill Clinton na baadaye Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia (WB), ambaye ni miongoni mwa wachumi wakuu zaidi duniani.

Prof. Lipumba amefanya kazi pia na Prof. Hernando de Soto, yule raia wa Peru na mchumi maarufu ambaye rais mstaafu, Benjamin Mkapa, aliwahi kumwita nchini kuwafundisha Watanzania kuhusu kile ambacho sasa kinafahamika kama Mkakati wa Kurasmisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA).

Yule mchumi maarufu kuliko wote duniani, Jeffrey Sacchs, aliwahi ama kusoma au kufanya kazi pamoja na Prof. Lipumba katika Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani.

Achilia mbali kazi mbalimbali ambazo Prof. Lipumba amewahi kufanya na mashirika mbalimbali ya kimataifa ya nchi wafadhili na Umoja wa Mataifa kama mshauri mwelekezi.

Kwa hiyo, kwa mimi ambaye ninafikiria zaidi kuhusu maendeleo ya uchumi kuliko kitu kingine chochote, Prof. Lipumba ndiye ninayemwona kama mtu anayejua namna ya kuikwamua Tanzania kiuchumi kutoka ilipo sasa.

Kaa naye, zungumza naye, utafurahi atakapokueleza kuhusu kitu kinachoitwa Multiplier Effect kwenye uchumi. Kwamba, kwa mfano, serikali itafaidika vipi na kuanzisha kiwanda cha kusindika matunda pale Lushoto, mkoani Tanga.

Prof. Lipumba atakueleza kwamba ukiwa na kiwanda cha watu 400 cha kusindika matunda, kutakuwa na faida zaidi ya moja kwa wakulima, serikali na wananchi wa Lushoto kwa ujumla.

Kwanza, atakwambia Lupumba ni ajira 400. Pili soko la matunda kwa wakulima na tatu kodi kwa serikali. Lakini utafurahi zaidi wakati atakapokuambia faida nyingine ambayo jicho la kawaida haliwezi kuona.

Kwamba wale waajiriwa 400, kwa ajira zao watamudu kununua sukari kwa ajili ya chai au uji. Kwa hiyo viwanda vya sukari nchini vitaongeza wateja.

Pili, waajiriwa hao wataweza kununua au kushona suruali na nguo nyingine. Hapo maana yake ni kwamba mafundi cherehani wa Lushoto watapata wateja.

Waajiriwa hao 400, watakuwa na uwezo wa kununua mikate, vitumbua na maandazi kwa ajili ya vifungua kinywa. Maana yake ni kwamba akina mama wauza vitafunwa na wenye maduka nao watafaidika.

Faida hiyo itakwenda kwa mafundi ujenzi watakaoanza kupata tenda za kufyatua matofali kwa vile waajiriwa hao watataka kujenga nyumba za kuishi.

Kwa mtaji huo, kwa sababu ya hiyo Multiplier Effect ya kuanzisha kiwanda Lushoto, eneo hilo lenye kiwanda litabadilika kiuchumi katika muda wa miaka mitano tu. Hayo ni maneno ya Prof. Lipumba.

Hata katika maisha yake ya kawaida, Lipumba si mtu anayependa ufahari. Binafsi nimewahi kula naye chakula katika maeneo ambayo mtu wa hadhi yake asingeweza kula.

Katika kampeni, nimewahi kushuhudia akilala katika nyumba za kulala wageni ambazo thamani yake haifiki Sh 10,000. Havai kifahari na wala si mtu mshaufu wa kupenda kujisifu.

Nimefika mpaka kijijini kwake, Ilolangulu, Tabora ambako nilizungumza hadi na mama yake mzazi. Prof. Lipumba anatoka katika familia ya kawaida kabisa na siku zote ni mtu anayekumbuka asili yake hii.

Katika nchi maskini kama Tanzania na ambayo imejaaliwa wingi wa rasilimali, ni muhimu kwa mtu anayekabidhiwa madaraka ya uongozi kuwa mwenye sifa hizi za Lipumba.

Siku moja, mwaka 2006 au 2007, wakati kashfa kuhusu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zilipoanza kuvuja, ni Prof. Lipumba aliyedokeza kuhusu mtu anayeitwa Prof. Benno Ndullu.

Wakati huo, aliamini kwamba Ndullu ndiye anayestahili kuwa gavana wa BoT. Wakati huo, gavana huyo wa sasa wa BoT, alikuwa akifanya kazi na WB nchini Marekani na kweli ndiye aliitwa kuwa mrithi wa nafasi hiyo iliyoachwa na Daudi Balali.

Baada ya mafanikio ya BoT, hasa katika kipindi cha mtikisiko wa kiuchumi duniani mwaka 2008, huku Prof. Ndullu akitangazwa na magavana Afrika kuwa ndiye bora miongoni mwao, nilimpa Prof Lipumba sifa kwamba anajua kufanya uteuzi wa watu makini.

Tatizo kubwa la Tanzania liko katika uteuzi wa watu kushika nyadhifa mbalimbali. Utakuta daktari wa binadamu akipewa wizara ya ujenzi, mtaalamu wa bima anapewa kuendesha shirika la ndege la umma huku kada wa chama asiye na elimu yoyote, akipewa wizara ya kilimo.

Hata hivyo, pamoja na sifa zote hizo za Prof. Lipumba, amewania urais wa Tanzania mara nne lakini ameshindwa kupata kura za kutosha ukiwemo uchaguzi uliomalizika wiki mbili zilizopita. Tatizo ni nini?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: