Profesa Lipumba: Nani kashindwa kazi?


Salva Rweyemamu's picture

Na Salva Rweyemamu - Imechapwa 14 July 2009

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Profesa Ibrahim Lipumba

WIKI iliyopita, Mwenyekiti wa muda mrefu wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alikaririwa na gazeti la MwanaHALISI akisema kuwa Rais Jakaya Kikwete "ameshindwa kazi."

Kiongozi huyo pia alikaririwa akisema kuwa hata chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeshindwa kazi.

Nianze kwa kutamka kuwa kauli hiyo ya Lipumba haiaminiki kwa sababu siyo ya kweli na nina hakika na yeye anajua kuwa siyo ya kweli. Lakini zaidi ya kutoaminika, kauli hiyo ni ya kusikitisha na yenye kiwango cha juu cha kutowajibika kutoka kwa kiongozi kama Lipumba.

Kwa sababu ni ukweli usiopingika kuwa miongoni mwa viongozi wote wa vyama vya upinzani, pengine Lipumba ndiye mwenye sifa angalau zinazokaribia zile za mtu anayeweza kufikiriwa kuwa kiongozi wa kitaifa.

Isitoshe, Lipumba sasa anao uzoefu wa uongozi wa chama cha siasa. Amekuwa Mwenyekiti wa CUF kiasi cha kwamba Mtanzania mwenye umri wa miaka 15 leo na anakaribia kuwa mpigaji kura dhidi ya chama hicho, hamjui mwenyekiti mwingine yoyote wa chama hicho, isipokuwa Lipumba.

Tatizo ni kwamba Lipumba anaongoza chama kisichokubalika katika sehemu kubwa ya nchi. Anaongoza chama ambacho kwa sababu ya sera zake za udini uliokithiri, kimefanikiwa kujithibitisha kuwa chama cha kikanda – kanda ya Pemba katika Tanzania Visiwani, wala siyo chama cha Zanzibar, bali chama cha Pemba.

Ni kauli za namna hiyo za Lipumba ambazo wakati mwingine zinamfanya kiongozi huyo wa CUF kushutumiwa kwa kuwa kigeugeu. Mwanasiasa ambaye asubuhi anasema jambo la maana na busara, jioni anasema jambo la ovyo, lisilokuwa na kichwa wala miguu. Kauli hiyo ndiyo kielelezo kizuri zaidi cha tabia ya Lipumba.

Sasa kutoaminika ni jambo moja. Liko jambo la pili ambalo ni kubwa zaidi kabla ya hata kujibu moja kwa moja hoja pindifu ya Profesa Lipumba. Hili la pili liko katika mfumo wa swali. Na swali lenyewe ni je, nani hasa kashindwa kazi kati yake yeye Profesa Lipumba na Rais Kikwete?

Tulijibu swali hili kwa ufupi tu kuonyesha kushindwa kwa Lipumba katika uongozi mzima wa chama kisichochagulika. La kwanza ni lazima tukubali kuwa ni kitendo cha kushindwa kwa mtu mwenye elimu, upeo, uzoefu na ujuzi wa mambo kama alivyo Lipumba kutoka chama kama CCM na kuingia chama kama CUF, na bado akaendelea kujiaminisha kuwa anaweza kupewa ridhaa ya kuongoza nchi na Watanzania.

Inahitaji mtu ambaye hajapata kuishi Tanzania kabisa kufanya uamuzi kama aliofanya Lipumba kuingia chama kisichoaminika kwa sababu ya udini, kisichochagulika kwa sababu ya kutoaminika, na kilichoshindwa kwa zaidi ya miaka 15 sasa kusambaza mtandao wake na ufuasi nje ya eneo dogo tu la nchi hii, yaani Kisiwa cha Pemba. Hili la kwanza. Miaka yote hii, ameshindwa kufurukuta kutoka nje ya Pemba. Sasa nani hasa kashindwa kazi?

La pili katika kujibu swali la nani kashindwa kazi ni kuangalia historia ya Lipumba na Kikwete katika kusaka uongozi. Lipumba ameanza harakati za kuwania urais tokea uchaguzi wa kwanza kabisa wa vyama vingi mwaka 1995.

Aligombea mwaka 1995, akashindwa vibaya na Rais Benjamin Mkapa. Akajaribu tena mwaka 2000 akashindwa tena na Mkapa. Akajaribu tena mwaka 2005 dhidi ya Kikwete, anajua kilichompata.

Sasa nani hasa kashindwa kazi? Huyu ambaye amekuwa mgombea na mshindwa mzoefu wa urais, ama mwenzake ambaye kasi yake ya kupata alichokiwania haihitaji kuelezwa kwa yoyote?

Tatu katika kujibu swali la nani kashindwa kazi ni kuangalia mafanikio ya Lipumba katika kujenga ushawishi wa CUF kuungwa mkono na Watanzania. Tokea kuundwa kwa chama chake na tokea yeye kuongoza chama hicho, CUF imepata ufuasi wake na wabunge wake kwa asilimia 99.99 kutoka Pemba.

Katika Unguja, CUF chini ya uongozi wa Lipumba imesusua vibaya mno. Kwa sasa ina kiti kimoja tu katika Unguja kwenye Jimbo la Ngome Kongwe. Huko Bara ndiyo kabisa, ni aibu. Imeshinda viti viwili tu katika miaka yote ya uongozi wa Lipumba. Kimoja cha Kigamboni, Dar es Salaam kilipata kushikiliwa na Frank Magoba kwa kipindi kimoja tu.

Cha pili, cha Jimbo la Bukoba Mjini wakati wa Wilfred Lwakatare; sasa nacho kimeota mbawa, kama alivyoota mbawa Lwakatare mwenyewe ambaye amekwenda CHADEMA. Hivyo katika eneo zima la Tanzania Bara, CUF chini ya Lipumba haina hata kiti kimoja. Nani hasa kashindwa kuongoza? Bila shaka atakuwa ni mwenye wabunge sifuri Bara.

Nne, katika kugombea kwake urais, hali ambayo ni rekodi ya Tanzania mpaka sasa, akishindana na Katibu Mkuu wake, Seif Shariff Hamad kwa urais wa Zanzibar, hajapata kuvuka zaidi ya asilimia 10 ya kura zote za urais.

Sasa nani kashindwa kazi? Huyu anayepiga asilimia 82 katika jaribio lake la kwanza ama yule wa chini ya asilimia 10 miaka nenda, miaka rudi.

Lipumba ana nini cha mafanikio ya kuonyesha katika miaka yote hii, ukiondoa uvumilivu wa kuheshimika, kwa kweli, wa kubakia katika chama cha upinzani kisichokuwa na dira wala mwelekeo, ama matumaini ya ushindi. Uvumilivu huu, kwa hakika, ni wa kuheshimika.

Maadamu sasa tumetoa ushahidi kuthibitisha kuwa ni Profesa Lipumba aliyeshindwa kazi na wala siyo Rais Kikwete, sasa tuangalie hoja ambazo Lipumba anajengea tuhuma ya kwamba Rais Kikwete ameshindwa kazi.

Lipumba anasema kuwa Rais Kikwete ameshindwa kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar, na kwamba ameshindwa kupambana na matatizo ya sekta za elimu, afya na nishati.

Kama nilivyosema hapo juu, Lipumba anasema mambo kama vile hajapata kuishi katika nchi hii. Hivi nani asiyejua kuwa ni CUF ambayo imekwamisha kufikiwa Mwafaka wa Zanzibar kwa sababu inakataa kurejea kwenye meza ya mazungumzo ya kumaliza mpasuko huo.

Kwa hakika, CCM na CUF, zimemaliza tofauti zao kuhusu Zanzibar. Tofauti iliyopo ni jinsi ya kutekeleza yaliyofikiwa; CCM ikisema kuwa makubaliano hayo yaende kwa wananchi kwa kura ya maoni, CUF ikisisisitiza kuwa saini za Katibu Mkuu wa CCM Yusuf Makamba na mwenzake Seif Shariff Hamad wa CUF zinatosha kuhalalisha mageuzi makubwa kiasi hicho katika mstakabali mzima wa Zanzibar.

CCM inashikilia kupata ridhaa ya wananchi kwa sababu mageuzi hayo, yatabadilisha mwelekeo mzima wa siasa na Katiba ya Zanzibar kwa kuundwa kwa serikali ya Mseto, CUF inasema saini za Makamba na Hamad zinatosha. Nani asiyeoona nani anafanya usanii hapa?

Kuhusu elimu, Lipumba haihitaji kukumbushwa kuwa ni Rais Kikwete aliyeleta mageuzi makubwa katika mfumo wa elimu ya Tanzania kuliko mwingine yoyote ukiondoa mwanzilishi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere. Leo hii, hakuna mtoto wa Tanzania anayeshindwa kuingia sekondari kama ameshinda mtihani kwa sababu sasa nafasi zinatosheleza mahitaji.

Tusisahau jambo moja. Shutuma hizo za Profesa Lipumba zilitolewa wakati akizindua "Operesheni Zinduka"- yaani, kwa maelezo yake mwenyewe, dira mpya ya chama cha CUF kuelekea kwenye uchaguzi mkuu mwakani.

Ishara moja ya kushindwa kwa sera za chama chochote cha siasa ni kuanzishwa kwa shughuli zinazoitwa "operesheni." Chama kina sera inayojulikana, sasa kinahitaji operesheni ya nini? Chama chochote kinachoanzisha operesheni maalum kinakiri udhaifu wa sera zake.

Kwa hakika kinazidi kuwachanganya zaidi wananchi, na hasa wafuasi wake, kwa kuwalazimisha wachague kati ya kufuata sera za chama chenyewe, ama matakwa ya operesheni maalum inayouzwa kwa wananchi kwa ghiliba kubwa mno. Hapa linakuwa limekuwa suala la kufa ama kupona.

Chama kinachokwenda vizuri hakihitaji msukumo wa operesheni maalum ya aina yoyote. La kuvunda halina ubani. Operesheni hizo zote, iwe ni Operesheni Zinduka, Operesheni Sangara ni kiini macho, ni ishara isiyopingika ya chombo kwenda mrama.

Makala hii imeandikwa na Salva Rweyemamu katika nafsi yake binafsi, na wala siyo kwenye nafasi yake rasmi ya Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Rais (DPC). Inaelezea tu mawazo na maoni yake binafsi na wala haiashirii maoni ama mawazo ya Ikulu ama ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: