Profesa Shivji amemaliza kila kitu


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir
Maridhiano Zanzibar
Profesa Shivji

KATIKA ujumbe mahsusi aliowatumia Rais Amani Abeid Karume na Maalim Seif Shariff Hamad, Profesa Issa Shivji, anauliza: Uchaguzi mwaka huu, bila ya kutanguliwa na mabadiliko katika hali ya kisiasa Zanzibar, utakuwa wa amani, haki na huru?

Ukweli haiwezekani. Kwa mazingira yaliopo sasa, ni ndoto hilo kutokea. Kama ambavyo ilishindikana katika uchaguzi uliotangulia tangu mwaka 1995, hakuna matumaini ya uchaguzi huru na wa haki.

Kwanza, mfumo wa kuratibu na kusimamia uchaguzi uliokuwepo mwaka 1995 na ambao uliendelezwa mwaka 2000 na 2005 haujabadilika.

Sekretarieti ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) haijabadilika kimtazamo na kiutendaji. Ingawa tume imepata mkurugenzi mpya wa uchaguzi, Salum Kassim Ali – mtaalamu wa teknolojia ya kompyuta aliyekulia ndani ya ZEC – watendaji wengine ni walewale.

Mfumo ungali ni uleule usiotoa fursa ya kuwepo kwa ushindani wa haki baina ya vyama shiriki. Ni mfumo unaokipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kinaendelea kunufaika na utaratibu wa asili wa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na vyombo vya habari vya umma, katika kushiriki kwake uchaguzi.

Huku akisema wazi kwamba mtindo wa wanasiasa kujali maslahi binafsi zaidi kuliko yale ya nchi ndiko kunakoendeleza matatizo ya Zanzibar, Profesa Shivji anasema maridhiano yaliyofikiwa na wakuu wa CCM na CUF upande wa Zanzibar yaimarishwe haraka kwa manufaa ya nchi.

Sasa Profesa Shivji, mtaalamu mahiri wa masuala ya katiba, anahimiza kwamba ni viongozi haohao wenye dhamana ya kuyafikisha maridhiano hayo panapotakiwa.

Kwa hivyo basi, analaumu na kuita ni jitihada za kupotosha mwelekeo mzuri wa kujenga Zanzibar kauli za watu wanaobeza hatua zinazofanywa.

Kauli kama Katiba isichezewe kwa kubadilishwabadilishwa; rais Karume asiongezewe muda wala kipindi kingine cha urais; hiyo ni kinyume na katiba na sera ya CCM; yaliyoanzishwa na Karume yanaweza kuendelezwa na mrithi wake anasema ni za upotoshaji.

Kwa muda sasa, tume ya uchaguzi inaendelea na uandikishaji watu wa kujumuishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar. Hata hivyo, kasi ya uandikishaji ni ndogo kutokana na idadi kubwa ya watu kukosa kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi ambacho ni shuruti kwa mtu kuandikishwa.

Kuna tuhuma nyingi za udanganyifu usiopatiwa majibu na Tume. Lakini hata wenyewe wamesema kuna watoto wanapelekwa kuandikishwa na baadhi ya watu wameshaandikisha zaidi ya mara moja.

Matatizo haya yanahitaji uhakiki. Kazi ya kuhakiki majina ilifanywa kwa chusha mwaka 2005 na hatimaye tume ikatangaza katika ripoti yake baada ya uchaguzi kuwa zaidi ya watu 3,000 waliandikishwa zaidi ya mara moja.

Hadi leo Tume imeshindwa kuwataja na kutoa taarifa zao ili vyombo vinavyohusika viwachukulie hatua kwa kuwashitaki mahakamani. Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Othman Masoud Othman amewahi kusema wamepewa orodha lakini taarifa zake hazitoshi kufanya uchunguzi na hivyo ni vigumu kuwapeleka mahakamani.

Pale baadhi ya wenye haki wanaponyimwa kushiriki na wasiosifa wakashiriki, basi uchaguzi wa haki umefutika. Kunapokuwa na vitisho katika hatua mbalimbali za uchaguzi, hapo uhuru umefutika. Na Tume inapoficha taarifa kuhusu mwenendo wa uchaguzi tayari uwazi umekosekana.

Sasa kwa kuwa hakuna mazingira ya kufanyika uchaguzi huru, wa haki na amani, panahitajika muda wa kujenga mazingira hayo. Ndipo profesa anapounga mkono uchaguzi uahirishwe.

Anashauri serikali ya mpito ambayo kwa utaratibu wa kisheria itapewa dhamana hiyo. Katika kipindi hicho cha kuondokana na mazingira ya kisiasa ya uhasama na kujenga mazingira ya ushindani wa kweli, mambo ya kutekelezwa itakuwa yanayozingatia makubaliano.

Utaratibu wa kisheria utaidhinishwa na wananchi kupitia Baraza la Wawakilishi. Hili litakiwe kuruhusu kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitafa – anasisitiza siyo serikali ya mseto (maana ni vitu viwili tofauti) – itakayotokana na viongozi kutoka CCM na CUF na kuiwekea msingi wa kuyatekeleza.

Serikali hiyo, profesa anasema, itaanzisha majadiliano ya kurekebisha katiba na sheria mbalimbali zikiwemo zinazogusa maslahi ya muungano na ambazo zitachochea maendeleo Zanzibar.

Katika njia tatu alizopendekeza kuweza kutumika, Profesa Shivji anaafiki moja inayoelekeza mpango wa kuongezewa muda rais aliyepo madarakani – anasisitiza siyo kuongeza kipindi cha urais – ili aongoze serikali ya mpito.

Anavyoona rais aliyepo anafaa. Kwanza, anasema, alichaguliwa, chama atokacho kina wawakilishi katika Baraza la Wawakilishi, anakubalika na chama cha upinzani chenye wawakilishi, wananchi inaonyesha wanamkubali katika hatua hii mpya.

Lakini profesa anaweka wazi kwamba mpango huo kamwe hauwezi kuwafurahisha wanasiasa waliotia nia ya kutafuta urais Oktoba. Hawa anasema wana haraka ya kushika Ikulu.

Hatua inayofuata itakuwa ni kuandaa muswada wa sheria itakayotaja hatua zote muhimu za kutekelezwa kikiwemo kifungu kinachoelekeza kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Sheria hiyo pia itatamka kuviweka kando vifungu vinavyohusika na masuala ya uchaguzi na kipindi cha urais kwa muda wa mpito. Sheria itapaswa kutamka ukomo wake wa kutumika ni muda gani jambo litakalotegemea vyama vimekubaliana muda gani serikali ya mpito iwepo.

Hatua iliyochukuliwa na CUF ya kumkubalia mjumbe wake katika Baraza la Wawakilishi, Abubakar Khamis Bakary (Mgogoni), ambaye pia ni kiongozi wa upinzani barazani, awasilishe hoja binafsi ya kuendeleza mwelekeo huo, inastahili kuungwa mkono.

Profesa Shivji anatoa funzo muhimu kwa Watanzania kwamba penye maridhiano hakuna tatizo lolote katiba ya nchi kubadilishwa. Muhimu ni kukubaliana eneo gani na kwa manufaa gani. Katiba inabadilishwa iwapo wananchi wamekubaliana kufanya hivyo ili kuleta manufaa kwao badala ya mabadiliko ya kunufaisha watu wachache.

Hapa hakuna jipya. Serikali ya CCM imebadilisha katiba mara ngapi tangu uhuru? Imekuwa ikibadilisha katiba kila inapotaka. Lakini haijaridhia hata mara moja mabadiliko ya maana yanayopigiwa kelele na Watanzania kupitia wataalamu.

Serikali imekuwa ikipuuza hata ushauri wa kitaalamu wa kutakiwa ifute sheria kadhaa kandamizi – kama ilivyoelekeza Tume ya Nyalali 1992 – badala yake kila wanapojisikia huongeza kutunga sheria mbaya.

Hivi sasa imo mbioni kupeleka bungeni marekebisho ya sheria mbili zinazohusu uchaguzi. Wadau – vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia – wameshakataa mapendekezo hayo kwa kuwa yanalenga kuviza demokrasia.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hadi leo haijapeleka muswada wa sheria ya kuanzisha Tume ya Kudhibiti Rushwa Zanzibar. Kwa miaka yote sheria hiyo imekuwa ikitajwatajwa lakini viongozi wa CCM wanaipinga.

Baada ya ofisi ya Spika wa Baraza la Wawakilishi kuthibitisha kupokea hoja binafsi ya Abubakar, wengi wamejenga imani kuwa Spika Pandu Ameir Kificho atairuhusu iwasilishwe na kujadiliwa.

Nataka kuamini kwamba kwa kuwa rais Karume ni zao la CCM, na sasa anatiiwa na CUF, wajumbe wataikubali hoja. Hiyo itakuwa hatua muhimu ya vyama hivi kuendeleza maridhiano na mambo mengine yatafuata.

0
No votes yet