"Acha Tarime wachague mbunge wao"


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 07 October 2008

Printer-friendly version
Ana kwa Ana
Kada CCM aonya wenzake
Mpiga kura Tarime akionyeshwa jinsi ya kupiga kura

“SIKU zote nasimamia kile ninachokiamini. Mbunge atakayekuja hatakuwa wa watu walioletwa kutoka Dar es Salaam, bali atakuwa wa wananchi wa Tarime. Hivyo basi, ni vema wananchi wasiingiliwe katika maamuzi ya kuchagua mbunge wao.”

Ni kauli nzito ya Mwita Mwikabe Waitara. Haina utata. Inalenga kujenga hoja isiyopingika, kwamba kila mbunge anachaguliwa na wale wanaomhitaji kwa kazi maalum ya uwakilishi wao. Basi!

Mwita Mwikabe Waitara ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alifanya mahojiano na MwanaHALISI wiki hii kueleza, pamoja na mambo mengine, vuguvugu la uchaguzi Tarime na hali ya kisiasa nchini kwa ujumla.

“Hawa (wananchi wa Tarime) ni watu wenye msimamo. Wameumbwa hivyo. Wengine wamezaliwa wakiwa tayari ni wanajeshi; hawana haja ya kujisajili jeshini. Ni vema matakwa yao yakaheshimiwa. Vinginevyo hapa hapatakalika,” anasema Waitara.

Kiongozi huyu wa Umoja wa Vijana (UV-CCM) aliyekuwa Katibu wa mkoa Tanga, anasema hatishii mtu. Halalamiki. Hana ugomvi na yeyote, bali anaeleza hali halisi na misingi ya mwakilishi na watu wake.

Ni Waitara ambaye Jumatano iliyopita alidondosha nyundo kichwani mwa CCM na viongozi wake waliotoka nchi nzima kwa madai ya kutafuta mbunge wa Tarime.

Alisema hatimaye mbunge atakuwa mbunge wa Tarime; hivyo wananchi wa Tarime ndio wanajua nani, miongoni mwao anafaa kuwa mwakilishi wao na siyo kwa utashi wala kauli za watu kutoka mbali.

Kutokana na kauli ya Waitara, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba amemwondoa kwenye timu ya kampeni, kumkatia tiketi ya ndege na kumwamuru kwenda Dar es Salam. Hivi sasa yuko jijini.

Katika kinyang’anyiro cha ubunge jimboni Tarime, kuziba pengo la Chacha Wangwe aliyefariki kwa ajali ya gari, CCM imeita viongozi na wasemaji kutoka nchi nzima kwa nia ya kupiga kampeni kwa mgombea wake.

Aidha, CCM imepata msaada, ama kwa kupanga au bila kutarajia wa baadhi ya vyama vya upinzani ambavyo vimeacha kupambana na chama hicho tawala na kuanza ugomvi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Alipoulizwa juu ya kauli yake aliyoitoa katikati ya uchaguzi Tarime, Waitara hakumung’unya maneno.

Alisema, “Chama tunakipenda, lakini mahali penye ukweli lazima tuuseme.”

Kuhusu kama haogopi kuchukuliwa hatua, kama ya kufukuzwa uanachama kwa kuonekana amekigeuka chama chake, Waitara alisema:

“Sina nidhamu ya woga. Mimi sijaumbwa hivyo. Ni lazima matokeo yamtamgaze mshindi halisi wa uchaguzi, vinginevyo tutaingia katika machafuko.”

Kabla ya uchaguzi unaoendelea Tarime,  Waitara alikuwa Katibu wa Umoja wa Vijana (UV-CCM) mkoa wa Tanga. Alishiriki katika kinyang’nyiro cha kura za maoni ndani ya chama chake kutafuta mgombe Tarime lakini aliambulia nafasi ya tatu.  

Baada ya zoezi la kura za maoni, Waitara aliteuliwa kuwa mmoja wa wapigadebe wa mgombea wa CCM, Cristopher Kangoye. Lakini sasa anasema waziwazi kuwa wananchi wamchague mgombea yeyote wanayeona anafaa.

“Kama watu wanataka kumchagua Kangoye, acha wamchague; kama wanamtaka Charles Mwera wa Chadema, waachwe huru kumchagua kwani hayo ndiyo maamuzi yao,” Anasema Waitara.

Anasema watu wanaotumia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Chacha Zakayo Wangwe “kutafuta ushindi, wamefilisika kisiasa.”

“Hapa hakuna uwezekano wa kutumia kifo cha Wangwe kushinda; huo ni uhalifu wa kisiasa. Wananchi wa hapa wanataka kujua hatua gani mbunge wao atazichukua kukabiliana na vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na wamiliki wa mgodi wa dhahabu wa Nyamongo,” anasema.

Kuna taarifa kwamba katika uchaguzi uliopita, Kangoye alipandikizwa kumg’oa Kisyeri Chambiri aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka15.

Kisyeri ni ndugu wa tumbo moja na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Enock Chambiri. Kangoye alishindwa kumg’oa Chambiri na hivyo wakaungana kumpigia kampeni Wangwe.

Waitara anakemea kuwepo kwa askari wengi katika wilaya ya Tarime hivi sasa. Anasema, “Kuna mauaji ya raia huko Bhumera na  nyumba zinachomwa moto katika vita vya koo. Lakini askari wamejichimbia hapa kusaidia kupora haki za wananchi. Hili ni jambo ambalo haliwezi kunyamaziwa,” anasema.

Waitara anasema CCM inakabiliwa na changamoto kubwa ya kujibu tuhuma za ufisadi zinazoandama chama na viongozi wake waandamizi.

Anasema kinyume na madai ya baadhi ya watu kwamba “ameamua kukiasi” chama chake kutokana na kushindwa uchaguzi, yeye bado mwanachama mwaminifu wa CCM.

Anasema, “Hapana. Ninachofanya mimi ni kusema ili kukisaidia chama hiki. CCM kinaelekea kubaya. Kimehama kutoka chama cha wakulima na wafanyakazi na sasa kinakumbatia watu wenye fedha tu.

“Kama huna fedha na huna watu wenye fedha kukutetea, huna chako ndani ya chama hiki. CCM imeshindwa kupambana na ufisadi, badala yake inakumbatia watuhumiwa wa ufisadi,” anasema.

Anatoa mfano wa alipokuwa Katibu wa  UV-CCM Tanga uongozi ulitoa tamko kutaka waliohusika na ufisadi wajiuzulu nafasi zao katika chama ili kutenganisha chama na ufisadi.

Lakini anasema Emmanuel Nchimbi, mwenyekiti wa UV-CCM taifa, alimwita Dar es Salaam na kumtaka kuomba radhi watuhumiwa hao, husasan aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Hata Makamba hakuwa nyuma. Alimtaka kufanya hivyo. “Sikukubali kwa sababu niliamini tamko lile lilipitishwa na vikao halali,” anasema.

Anasema badala ya CCM kushughulikia mafisadi, wanahangaika na wanaopinga ufisadi. Anatoa mfano wa mradi wa kitega uchumi cha UV-CCM, kwamba haukupitishwa na vikao vya jumuiya.

“Lakini Nape (Nape Moses Nnauye) alipozungumza akaishia kufukuzwa uwanachama. Hata mimi nimehukumiwa kutokana na msimamo wangu wa kumuunga mkono Nape,” anafafanua.

Waitara amehamishwa kutoka Tanga na kupelekwa makao makuu ya UV-CCM mkoani Dar es Salaam ambako amefanywa kuwa katibu msaidizi wa Nchimbi.

Je, amekubali uteuzi huo? Waitara anajibu kwa sauti ya juu, “Nani? Mimi? Siwezi! Mimi siwezi kuwa karani wa Nchimbi.  Mimi na usomi wangu wote na heshima yangu, nifanye kazi ya kumfungulia mlango Nchimbi akifika ofisini; kumwandalia chai na kupeleka maji kwenye vikao? Siwezi kujidhalililisha na kudhalilisha elimu yangu. Hilo haliwezekani,” anasema.

Aidha, Waitara anadokeza kuwa wakati wa kuandaa mkataba wa kinyonyaji wa UV-CCM na mwekezaji, Beno Malisa (Kaimu Naibu Katibu Mkuu) alikuwa mwanasheria wa umoja huo. “Huyu ndiye aliyeshiriki kwa asilimia 100 kupitisha mkataba,” anasema.

Baada ya kufanikisha kazi hiyo anayoita haramu, Malisa alipewa zawadi ya kuwa Naibu Katibu Mkuu. “Na sasa wanataka kumpa uenyekiti wa jumuiya ili alinde mradi wao,” anaeleza.

Anamtaja pia Isaack Francis aliyekuwa Katibu wa Fedha, Uchumi na Mipango katika umoja huo, kwamba alikuwa mmoja wa washirika wakubwa wa mkataba huo wa kinyonyaji.

Anasema, “Huyu (Francis) ameshiriki kwa asilimia 100 kupitisha mradi. Baada ya kumaliza kazi yao wamempa wadhifa wa Kaimu Katibu Mkuu ili baada ya uchaguzi Malisa amthibitishe kuwa Katibu mkuu.”

Kinachomtia masikitiko zaidi Waitara, ni kile alichoita hatua ya mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani Kikwete, kujiingiza katika “kutetea mafisadi.”

“Ridhiwani anapita kila mkoa kumnadi Beno Malisa ili baadaye naye ampitishe Issack. Tayari amefanya mikutano Singida, Shinyanga na Mwanza. Lakini hakuna mtu anayemuuliza,” anasema kwa masikitiko.

Anasema, Ridhiwani “Hana mamlaka ya kutuchagulia viongozi. Yeye si rais, ni mtoto wa rais. Hata rais hana uwezo huo. Aache kutumia kivuli cha baba yake kutupandikizia viongozi.”

Waitara alizaliwa katika kijiji cha Ingwe, kata ya Nyamungu, wilayani Tarime akiwa mtoto wa saba kati ya kumi wa Mwikabo Waitara. Hana undugu na aliyekuwa mkuu wa majeshi Jenerali George Waitara.

Alijiunga na UV-CCM mara baada ya kuhitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alifanywa kuwa Katibu wilaya, Kinondoni.

Waitara amekuwa kiranja mkuu shule ya msingi; waziri wa elimu shule ya sekondari Azania na rais wa serikali ya wanafunzi (DARUSO).

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: