"Msemaji" wa Ikulu si taswira halisi ya msimamo wa Rais


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 29 April 2008

Printer-friendly version

MANENO matupu ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu ufisadi yanachosha. Nina imani wananchi wanaamini hivi kwa sasa baada ya kuona maendeleo madogo ya juhudi za kuwaondoa katika umasikini.

Tabia ya viongozi wakisema "uchunguzi bado unaendelea" na "wananchi vuteni subira" ikiendelea, ni dhahiri matarajio yao ya kupata maisha bora yatazidi kufifia.

Tukiacha lugha hii ya kukatisha tamaa, kuna nyingine inayosumbua pia kuisikia. Mwishoni mwa wiki, Rais, kupitia Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, aliasa wafanyakazi nchini kukataa kutumiwa katika miradi ya mafisadi na vigogo wa rushwa ili washindwe kutimiza malengo yao.

Rais ametaka wafanyakazi wawe mstari wa mbele kufichua vigogo wala rushwa, tena bila ya woga.

Kauli zote mbili zinaonyesha namna serikali inavyolega katika vita dhidi ya ufisadi na mtu anaweza kusema kuna usanii mwingi.

Tutakwenda pamoja na kuweka maswali muhimu: Jee wafanyakazi wanafahamu vigogo mafisadi na miradi yao? Tuseme wanawafahamu, hivi kweli kuwataja ndiyo njia sahihi?

Vyombo vya usalama na sheria viko wapi? Na kwa nini utaratibu huu uwe kwa vigogo tu, ambao wengi wao ni wakubwa serikalini au wafanyabiashara wanaokifadhili chama tawala?

Hali inaonyesha bila ya kuwa na sifa hizi, ni vigumu mtu kufisidi nchi; ule ufisadi tunaouzungumza, na siyo huu wa manesi hospitalini, makarani mahakamani na matrafiki barabarani wanaosumbuliwa na njaa ya kutwa moja.

Tuendelee pamoja: Kauli ya pili ya kuasa wafanyakazi kutoogopa kufichua vigogo waovu, inashangaza nayo na naiona ni ya kinafikinafiki hivi. Ni dhahiri, kwao wafanyakazi, wametoa mchango mkubwa kufichua baadhi ya vigogo. Ni wao walioiba na kunyofoa nyaraka muhimu za serikali zilizobaini na hatimaye kuibua vitendo vya ufisadi.

Lakini wanafanyakazi hii hatari bila ya kinga yoyote. Hadi sasa serikali haijapitisha muswada wa sheria ya kulinda watu wa aina hii, sheria ya kuhami wafuchua maovu (Protection of Whistleblowers Act).

Sheria hii ilikuwa ipitishwe pamoja na iliyoisuka upya TAKUKURU (ambayo ilipitishwa 2007) ili ziende sambamba. Kutoipitisha hii ya kukinga wafichua uovu kwa kutoa nyaraka za serikali, kunamaanisha serikali ina haki ya kushitaki wafanyakazi hawa chini ya Sheria ya kulinda Siri za Serikali; Official Secrecy Act.

Lakini kikubwa zaidi, wito wa Rais wa kutaka wafanyakazi wasihofu kufichua mafisadi, ni kichekesho iwapo sheria zilizopo zinakataza kufichua vigogo wa serikali wanaoshukiwa kwa ufisadi: Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma (Public Leadership Ethics Act) na kanuni zake.

Sheria hii sasa iko majaribuni baada ya taasisi za wanaharakati wa haki za binadamu, kufungua kesi Mahakama Kuu kutaka kuondolewa kwa vipengele vinavyokataza uchapishaji wa taarifa zinazohusu mali za viongozi wa umma walizoziandikisha.

Kama serikali ingekuwa thabiti, ingekwishaona sheria hiyo haifai na ikarekebishwa. Rais anahimiza harakati za kukomesha ufisadi lakini serikali anayoongoza inalinda sheria zinazokwaza harakati; ajabu kubwa.

Kauli nyingine aliyoitoa Rais kupitia msemaji wake, inagusia kwamba si kazi ya Rais kufikisha mahakamani waziri anayejiuzulu, maana kuna vyombo vinavyohusika na hatua hiyo.

Inamaanishwa TAKUKURU, taasisi iliyo chini ya Ofisi ya Rais. Ni taasisi isiyothubutu kujitambulisha kama chombo huru kimajukumu. Kwa asili yake, taasisi hii inafanyakazi kwa maelekezo.

Pili hali hii inapingana na kanuni moja kuu ya usimamiaji na utoaji haki inayosema "Haki si tu itendeke, bali pia ionekane inatendeka."

Ile tu TAKUKURU kuwa chini ya Utawala (moja ya mihimili muhimu ya Dola), inatosha kuonesha kuwa inakabiliwa na ugumu katika kutekeleza majukumu yake kwa uhuru. Tumeona namna watuhumiwa wengi wa ufisadi wanavyolelewa badala ya kushughulikiwa ipasavyo.

Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU ni Dk. Edward Hoseah, ambaye anatuhumiwa kuhusika na ufisadi katika sakata la Richmond kama ilivyobainishwa na Bunge (mhimili mwingine). Baada ya kujadili ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza utata wa mkataba wa Richmond, lilipendekeza Hoseah achukuliwa hatua.

Bado hatua hizo hazijaonekana (maana angalau serikali ingesema Hoseah anachunguzwa) ikiwa na maana ya mhimili mmoja (Utawala) kubeza uamuzi wa mhimili mwingine (Bunge).

Ni Hoseah huyu amejumuishwa katika uchunguzi wa wahusika wa ufisadi wa Sh. 133 bilioni zilizoibwa katika akaunti ya madeni ya nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Umma unaambiwa kwamba Rais hahusiki tena kwa yale yanayofuata baada ya kuwa amemfukuza Gavana wa BoT, Daudi Ballali na kwa sababu hiyo, hata baada ya Andrew Chenge kujiuzulu kwa tuhuma za kula mlungula kutokana na mpango wa ununuzi wa rada.

Ingeonekana kuna umakini iwapo Rais angeongoza kweli vita dhidi ya ufisadi kwa kuonyesha kwa vitendo hatua anazochukuwa pale mteule wake anapoguswa. Basi hata kumsimamisha kazi mtendaji anayetuhumiwa?

Lazima nishauri kwamba mtindo unaoanza tena wa Rais kuwasiliana na wananchi kupitia msemaji wake, hautaleta manufaa yanayotarajiwa.

Naona si utaratibu mzuri, kwani utategemea sana na hulka ya msemaji mwenyewe. Juzi nimesoma makala moja ikitahadharisha kuzuka kwa "Alfred Mutua"? wa Tanzania. Kuna hatari kuwa kile anachodhamiria kukisema Rais hakitakuwa kile kinachoweza kusemwa na msemaji wake.

Alfred Mutua ni msemaji wa Rais Mwai Kibaki wa Kenya.

Ipo hatari ya akina "Mutua" kupotosha mambo, kwa kumwambia yale ya kumpendezesha tu, badala ya hali halisi inayojionesha. Hii ni hatari kwani kiongozi wa nchi anaweza kujikuta mbali mno na wananchi.

Lakini hata hivyo inavyoonyesha yeye mwenyewe Kikwete anapendelea hivyo. Chukulia kwa mfano suala la wadhifa wake wa sasa kama Mwenyekiti wa AU. Jee mtu hawezi akasema kuwa "pumu imepata mkohozi."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: