RADA imewafunua watawala, watajificha wapi?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 10 February 2010

Printer-friendly version
Tafakuri
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge

KUNA kitu kinaitwa bahati. Wapo watu waliozaliwa na bahati, mafanikio yao katika maisha hayafanani hata chembe na bidii wanayotia katika kujitafutia maisha.

Hawa ni kama wale wanaoshinda bingo; utasikia mtu kwa kununua tu tikiti ya bahati nasibu ya Sh. 1,000 anaibuka kuwa milionea, anashinda Sh. milioni 500 au hata Sh bilioni moja. Kuna watu wanashinda bahati nasibu ya nyumba ya kisasa, magari ya kisasa ya kifahari kabisa.

Kwa hali hiyo, mshindi wa bahati nasibu hana jasho lolote alilotoka kama vile mkulima anayetaabika kujipinda kwa jembe la mkono akipanda, kupalilia na kuvuna mazao yake shambani. Maisha ya hawa wawili ni sawa na mbingu na ardhi!

Tanzania nimeiweka kwenye kundi la mwenye bahati kwa sababu nyingi tu, lakini habari ya ununuzi wa rada ya bei mbaya na jinsi kampuni ya British Aerospace (BAE Systems) ilivyoamua kukubali yaishe kwa kuamua kulipa kiasi cha Pauni 30 milioni kama fidia kwa rada iliyouzia Tanzania mwaka 2002 kwa bei ya Pauni 28milioni.

Fedha hizo ni sehemu ya fidia ya Dola za Marekani 400 milioni ambayo BAE Systems wametakiwa kulipa kutokana na kujikuta katika matata ya kuuza vifaa vya kijeshi kwa nchi mbalimbali duniani, kama Tanzania na Saudi Arabia .

Kwa maneno mengine, Tanzania sasa inapata faida kutokana na rada iliyonunuliwa mwaka 2002, inalipwa fidia zaidi ya bei ya rada ambayo ililalamikiwa kuwa ni ya juu sana , lakini pia inabakia na rada hiyo. Haya yanafanyika ili kuhitimisha uchunguzi wa Ofisi ya Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza juu ya utoaji wa rushwa katika biashara. BAE Systems imekuwa ikituhumiwa kuendesha vitendo vya kifisadi katika biashara za kuuza vifaa vya kijeshi kwa nchi mbalimbali duniani.

Tanzania iliingia katika anga za kashfa hiyo wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa, ilibainika kwamba rada ya kijeshi ambayo ilinunuliwa mwaka 2002, ilikuwa ya bei ya juu sana; kwamba bei halisi ilikuwa imekuzwa mno na wapo watu waliofaidi cha juu karibia theluthi moja ya bei hiyo yaani kiasi cha Dola milioni 12, kiasi kinachodaiwa kugawa kama rushwa kulainisha tenda ya ununuzi wa rada hiyo.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba wapo watu waliotajwa katika uchunguzi wa SFO mmojawapo ni mwanasiasa Andrew Chenge. Chenge ambaye kwa sasa ni mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM) wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (1995-2005) anadaiwa kusaidia ununuzi wa rada hiyo na kwamba alinufaika katika mgawo.

Chenge aligundulika akiwa amejilimbikizia kwenye akaunti yake kisiwani Jersey kiasi cha Dola milioni moja (Sh bilioni 1.2), fedha anazodai ni mapato yake halali kutokana na kazi za kisheria na urithi wa familia.

Tangu kufumuka kwa sakata la ununuzi wa rada hiyo, mamlaka za Tanzania , hasa wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa, kwa maombi maalum kwa Serikali ya Uingereza, waliomba taarifa za uchunguzi wa rada hiyo usitolewe hadharani.

Hata hivyo, pamoja na juhudi za watawala wetu kutaka kufunika kombe ili mwanaharamu apite, mwanaharamu amegoma kupita na ameganda kwa muda mrefu ndani ya viambaza na korido za serikali na wote waliohusika katika sakata hili, matumbo yanawacheza kila uchao. Ya juzi yamewaongezea homa.

Chenge kutokana na shinikizo la uchunguzi wa SFO alijiuzulu nafasi ya Waziri wa Miundombinu Aprili 21, 2008 ili kupisha uchunguzi wa SFO kuhusiana na sakata la rada.

Katika uchunguzi wa SFO ambao nyaraka zake zimeonekana hadharani, mbali na Chenge, pia anatajwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati huo, Dk. Idris Rashidi kuhusika pia katika mtandao wa ulaji wa mgawo huo wa Sh bilioni 12 na ushei.

Wakati wote huu, Tanzania kama taifa hasa serikali haijafanya lolote kufanikisha Chenge na Dk. Rashidi kukiri au walau kuwawajibisha kwa njia yoyote juu ya tuhuma hizi.

Kikubwa sana kilichotokea ni kujiuzulu nafasi ya uwaziri kwa Chenge na wala si kutimuliwa na Rais. Dk. Rashidi ambaye utumishi wake BoT ulifika kikomo wakati wa kipindi cha ya pili cha utawala wa Mkapa, amezidi kuonekana kipusa, baada ya kupewa nyadhifa nzito nzito huko na huko kwenye sekta binafsi, serikali iliishia kumpa majukumu ya Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco.

Chenge angali mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, tena ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya CCM, ameteuliwa huko na huko na CCM kusaidia katika kutoa ushauri wa kisheria kwenye miradi ya CCM, kama vile mradi wa ujenzi wa majengo ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) barabara ya Morogoro jijini Dar es Salaam.

Wakati serikali imejikalia kama haina taarifa zozote kuhusu Chenge na Dk. Rashidi, na wakati ukweli ukikataa kufunikwa kombe, mwishoni mwa wiki bahati ya mtende imeangukia taifa hili, kwamba sasa italipwa Pauni milioni 30,000 (Sh. bilioni 60) na BAE Systems kwa udanganyifu tuliofanyiwa, lakini kwa aibu ya kiwango cha juu kabisa watawala wetu wakautetea.

Sote tunamkumbuka yule Waziri wa Uingereza wa Misaada ya Maendeleo, Claire Short, maarufu kama mama wa rada, aliyekataa kusadikishwa kwamba mchakato mzima wa ununuzi wa rada ya Tanzania ulikuwa wa halali, alipokuja nchini alikaa na Rais Mkapa, lakini mwisho wa siku alituacha na majonzi kama wananchi kwa kuwa hakupasua jipu lake kama alivyotaka.

Alituacha, lakini hata hivyo alirejea kwao akashikilia msimamo kwamba kuna ‘mchezo’ mchafu katika ununuzi wa rada hiyo ingawa hakuwa na ushahidi madhubuti.

Mama wa rada hapana shaka alikuwa anatumia kile kinachoitwa kwa kimombo gut- feeling. Hisia zake zilikataa kukubalia kwamba inawezekana kwa nchi masikini kama Tanzania bila kupepesa macho ifikie umauzi wa kununua rada kwa bei mbaya kiasi hicho, bila kuwepo kwa kishawishi chochote kwa pande zote, yaani muuzaji na mnunuzi!

Leo mwaka 2010, lile kombe alililotaka Mkapa kufunika mwaka 2003, na zile juhudi za watawala wa sasa kumwona Chenge na Dk. Rashidi kama watu safi , vyote vimekataa kufanya kazi.

Kudra zimefanya kazi, taifa linarejeshewa kile lilichoporwa. Kweli tuna bahati, tunanufaika na fedha hizi hata kama Takukuru au polisi wetu au hata usalama wa taifa hawakufanya lolote la maana kusaka ukweli kuhusu unyang’anyi huu tuliofanyiwa na watu wetu wenyewe tena tuliowapa madaraka na kukalia ofisi za umma.

Baada ya habati hii ya mtende, sasa tunazidi kujiuliza, bado watawala wetu wanakosa soni; nyuso zao hazina hata haya, kiasi kwamba tunasonga mbele na Chenge wetu pamoja na kina Dk. Rashidi?

Hivi katika hali kama hii Takukuru watatuambia nini, kwa kuwa SFO wamesema sasa kazi iko mikononi mwa serikali ya Tanzania .

Tunathubutu kufanya lolote, au hii na Kagoda ni baba na mwana, hakuna kudhuriana. Jamani watawala wetu waliumbwa na nini? Nyama na mifupa kama watu wengine au wao wana miili ya chuma na zege kiasi kwamba hawana hisia wala chembe ya soni?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: