Rada kumuumbua Mkapa


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 10 February 2010

Printer-friendly version
Lipumba ataka Bunge lichunguze
Hata dili za helikopta na ndege ya rais
Rais  mstaafu, Benjamin Mkapa

BAADA ya kampuni iliyouza rada kwa serikali kukiri kutumia rushwa, Bunge limeombwa kuchunguza mikataba yote mikubwa inayomuhusisha mfanyabiashara Sailesh Vithlan.

Vithlan ndiye wakala mkuu katika ununuzi wa ndege ya rais, helikopta na vifaru vya jeshi na rada ambayo uchunguzi wa kashfa yake umekamilika.

Akiongea na MwanaHALISI jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kwa vile rushwa imeonekana kwenye suala la rada, lililosimamiwa na Vithlani, basi kuna uwezekano wa kuwepo ufisadi katika manunuzi mengine yaliyowezeshwa na mfanyabiashara huyo.

Katika mahojiano maalum juzi Jumatatu, Profesa Lipumba amependekeza kuwa Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza mikataba yote ya manunuzi ambako serikali ya Banjamin Mkapa ilimtumia Vithlan.

“Ombi langu kwa Bunge ni kwamba liunde Kamati Teule, kama ilivyokuwa kwa Richmond ili kuchunguza makubaliano yote ya mununuzi ya vitu hivi ambapo serikali ilimtumia Sailesh Vithlani,” alisema Prof. Lipumba.

Wakati wa utawala wa Rais Mkapa, Tanzania ilinunua rada kutoka kampuni ya Uingereza ya British Aerospace Systems (BAE Systems) kwa pauni milioni 28 (zaidi ya Sh. 40 bilioni).

Taarifa za uchunguzi zilizopatikana baada ya ununuzi zilieleza kuwa bei ambayo Tanzania ilinunulia rada ilikuwa mara tatu zaidi ya bei halisi.

Uchunguzi wa shirika la kikachero la makosa makubwa ya jinai la Uingereza (SFO) uligundua kuwa Vithlan pamoja na washirika wake ndani na nje ya nchi, walilipwa zaidi ya Sh.12 bilioni za kulainisha maofisa wa serikali ili rada inunuliwe kwa bei waliyotaka.

Wiki iliyopita, BAE walikiri kutumia rushwa kulainisha watendaji katika serikali ya Tanzania na kwamba wanajutia adhabu waliyopewa ambayo wameita kubwa kuliko zote zilizowahi kutolewa nchini Uingereza.

BAE wametozwa faini ya Sh. 500 bilioni kwa ufisadi huo katika nchi mbalimbali kupitia uuzaji vifaa vya kijeshi.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa BAE, Dicky Oliver, katika taarifa yake kupitia tovuti ya kampuni yao, alisema hawatachukua hatua yoyote kwa maofisa wa Tanzania waliochukua mlungula. Alisema hao watashughulikiwa na serikali yao.

Prof. Lipumba amesema kwa kuwa serikali ya Uingereza imethibitisha kwamba ununuzi wa rada uliofanywa na serikali ya Tanzania ulighubikwa na rushwa, inawezekana kabisa kuwa kila ununuzi uliofanywa kwa kuhusisha Vithlani, ulifanywa kwa misingi ya rushwa.

“Huyu alihusika kwenye ununuzi wa ndege ya rais, magari ya jeshi pamoja na zile helikopta. Sasa kwa kuwa tumethibitishiwa kuwa rushwa ilitumika, ni muhimu tukachunguza dili zote hizo,” alisema.

Prof. Lipumba alisema amesikitishwa mno na namna serikali ya Rais Jakaya Kikwete inavyolishughulikia suala zima la ununuzi wa rada.

Alisema SFO waliishataja maofisa wa ngazi ya juu serikalini akiwemo Andrew Chenge ambaye anahifadhi fedha katika akaunti yake kwenye benki iliyoko kisiwa cha Jersey, nchini Uingereza.

Prof. Lipumba alisema inashangaza kuona serikali ya Tanzania siyo tu imeshindwa kuchangamkia kufuatilia kashfa hiyo bali viongozi wake kadhaa wa ngazi ya juu wamethubutu kutetea kwamba hakuna uovu wowote.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka mjini London, kampuni hiyo pia imeagizwa kuwasilisha pauni 30 milioni (kiasi cha Sh. 30 bilioni) kwa serikali ya Tanzania kama fidia kutokana na hujuma iliyoifanyia.

Mfanyabiashara Vithlani ambaye amefunguliwa mashitaka akiwa hayupo nchini, baada ya kudaiwa kutoroka, anadaiwa kutafutwa na vyombo vya dola vya Tanzania na kwamba tayari taarifa zake zimefikishwa Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol).

Iwapo suala hilo litachunguzwa na bunge, na hasa baada ya SFO kukamilisha uchunguzi na BAE kukiri matumizi ya rushwa, ni wazi rais mstaafu Mkapa, atakutwa na tuhuma, ama za kushiriki au kunyamazia rushwa katika ununuzi huo.

Andrew Chenge, aliyekuwa mwanasheria mkuu, amekuwa akibeza tuhuma kwa madai kuwa uamuzi wa kununua rada ulipitishwa na Baraza la Mawaziri na siyo yeye binafsi.

Rais ndiye anayeongoza vikao vya baraza la mawaziri wakati mwanasheria mkuu wa serikali ndiye mshauri mkuu wa serikali kuhusu masuala ya sheria.

Prof. Lipumba amesema, “Hata hicho kiasi cha fedha ambacho Uingereza imeamuru kirejeshwe nchini, hakikuwa kimeombwa rasmi na serikali yetu. Inakera kwamba serikali haikuchangamka kabisa katika hili.”

Akizungumza na MwanaHALISI juzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, alisema suala hilo liko mikononi mwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

“Naomba maswali yako kuhusu hayo mambo ya rada uyapeleke kwa Hoseah (Edward, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU).

“Wao ndio waliokuwa wakichunguza hilo suala la rada na hawajatuletea ripoti yao ya uchunguzi kwa ajili ya prosecution (mashitaka). Wao ndio wanaojua kila kitu kwa sasa,” alisema Werema.

Dk. Hoseah alipozungumza na gazeti hili alisema hana cha kuzungumza kuhusu ripoti ya SFO.

Alipong’ang’anizwa kutoa kauli kwa kuwa ofisi yake ilitoa ushirikiano wakati makachero wa SFO wanachunguza kashfa hiyo, Hoseah alisema, “Andikeni mnavyotaka.”

MwanaHALISI haikufanikiwa kumpata Chenge ambaye anahudhuria mkutano wa bunge mjini Dodoma, ili atoe msimamo wake baada ya taarifa za kuthibitishwa kwa rushwa katika ununuzi wa rada.

Hata hivyo, Chenge alinukuliwa hivi karibuni na vyombo vya habari nchini akisema wanaostahili kuulizwa kuhusu suala hilo ni TAKUKURU kwani ndio wanaolishughulikia.

Akizungumzia sakata hilo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Ubalozi wa Uingereza nchini, John Bradshaw, alisema kwa sasa serikali yake haina cha kusema.

“Hatuna lolote la kuongeza kuhusu suala la rada. Ningeshauri ufuatilie taarifa kutoka tovuti ya SFO, lakini sisi kama serikali hatuna cha kuongeza,” alisema.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: