Raha ya tajiri na suluba za masikini Bulyanhulu


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 30 March 2011

Printer-friendly version

UKITAKA kujua matajiri wanavyopata raha maishani, tazama jinsi maskini wanavyohangaika kupata mkate wao wa kutwa.

Angalia masikini wanavyomega ardhi kwa kutumia nyenzo duni hadi wanapata vipande vidogo sana vya dhahabu.

Kazi ya kuchimba, kuchakata hadi inapatikana dhahabu, ina mlolongo mrefu, na wakati mwingine kipato huwa kidogo.

Kampuni kubwa kama ya African Barrick Gold inaweza kupima eneo na kujua kiasi itakachopata, tena kwa siku moja baada ya kupasua miamba, kusaga na kusafisha.

Wachimbaji wadogo huweza kuhangaika wiki nzima na wasipate kitu cha maana au wakati mwingine wasipate chochote. Wanakwenda kwa mtindo wa kubahatisha.

Mathalani, kwa miezi mitatu sasa, wachimbaji wadogo wanaguguna ardhi katika eneo la Nyakagwe wilayani Geita (kilometa tano hivi hadi Bulyanhulu). Wanatarajia kufikia mwamba wenye dhahabu mwishoni mwa Aprili.

Nyanda Emmanuel (24) anasema kazi ya kuchimba dhahabu ni ngumu na hushirikisha kikundi cha vijana kati ya wawili hadi watatu.

Uchimbaji huhusisha kubeba udongo kupeleka kwenye krasha (mashine ya kusaga mawe), kuosha kwenye mwalo na kunasa kwa zebaki kisha kuchoma ili kupata kitu kamili.

“Ni kazi ngumu, lakini heri hii kuliko wizi. Sisi tukihangaika tukafanikiwa kupata dhahabu ya uzito tola moja ya rangi ya kaki, tunauza kwa Sh. 650,000; ile ya rangi nyekundu tunauza kwa Sh.750,000,” anasema Emmanuel.

“Hii ni bei ya hapa. Barrick wanaochimba kwa wingi na kuuza nje, tunaambiwa wanauza kwa zaidi ya Sh. 1.6m kwa tola moja,” anasema.

“Katika kikundi chetu kila mtu hupata si chini ya Sh. 30,000 tukiondoa gharama zote.”

Gharama zinazoondolewa ni malipo kwa wanaonasa dhahabu kwa zebaki na mashine ya kusaga mawe yanayosadikiwa kuwa na dhahabu hadi unakuwa unga.

Ramadhani Embasi (27) ambaye amekuwa akifanya kazi ya kuendesha krasha tangu mwaka 2002, anatoza Sh. 5,000 kwa mzunguko mmoja wa dakika 40.

Katika mzunguko huo, mashine huponda hadi linabaki vumbi ambalo mmiliki hupeleka kulowanisha kwenye mwalo ili kunasa vipande vidogo vya dhahabu.

“Nikinunua lita tano za dizeli natumia kwa mizunguko sita. Faida ipo lakini anayefaidika ni mmiliki wa krasha na katika mazingira mazuri wachimbaji huvuna sana,” anasema Embasi.

Tofauti na kipato cha wachimbaji wadogo, ofisa mmoja wa ngazi ya juu wa Barrick amesema kila mgodi wao unazalisha vitofali vitano vya dhahabu kwa wiki. Kila kitofali kina uzani wa kilo 25 na kila kilo moja ina uzani wa tola 83.

Ofisa wa kigeni kwenye mgodi wa Bulyanhulu amesema, “Haya ni mapato yanayotangazwa serikalini na serikali yenyewe haina takwimu juu ya kinachoendelea. Ni wazi mmewaachia mno.”

Mfanyakazi ndani ya mgodi anasema taarifa walizonazo ni kwamba mgodi unaendeshwa kwa gharama zinazotokana na mchanga tu unaodaiwa kusafirishwa usiku kwenda nje ya nchi.

“Bulyanhulu ni mgodi mama; ndio uliozaa Tulawaka (Biharamulo) na Buzwagi. Mchanga peke yake ndio unalipa mishahara ya wafanyakazi hapa,” anasema mfanyakazi huyo.

Wafanyakazi na wananchi wanalalamikia uamuzi uliofanywa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuwapokonya eneo walilokuwa wanalima na kuchimba dhahabu mwaka 1996 ambalo ndilo walipewa KMCL.

“Maeneo ambayo tulikuwa tunalima yalichukuliwa na mgodi na ndiko wanalima mibono. Hatuna mashamba wala eneo la kuchimba dhahabu. Hapa tunaishi kwa kuosha marudio ya mchanga ili kupata dhahabu na baadhi wanachimba kule Nyangalata na Nyamalata,” anasema mwenyekiti wa kijiji cha Kakola, Emmanuel Bombeda.

“KMCL (sasa African Barrick Gold) walimilikishwa eneo lote la kijiji cha Kakola. Hata ulikofika kule Nyangalata na Nyamalata, ambako vijana wanachimba dhahabu, ni ‘sehemu’ ya mgodi,” anasema.

“Mwekezaji aliamua kung’oa alama zote za mipaka zilizokuwa zinatenganisha kijiji na mgodi; akaweka zake kibabe kuonyesha Kakola yote ni yake na wananchi wahame. Tulikataa na mgogoro ulimalizika mwaka jana mipaka ilipowekwa upya,” anaeleza Bombeda.

Vipimo vya mipaka vinaonyesha kampuni ya Barrick iliyorithi mgodi wa Bulyanhulu imebakiwa na eneo lenye ukubwa wa ekari 27 wakati kijiji kina eneo la ekari 17 tu.

0
No votes yet