Rai ni wazushi, wachonganishi


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version
Gazeti la Rai

MCHAPISHAJI wa gazeti la MwanaHALISI, Saed Kubenea, amekana tuhuma kwamba gazeti lake linashiriki “njama za kupindua serikali ya Rais Jakaya Kikwete.”

Tuhuma hizo nzito zilitungwa na kuibuliwa kupitia gazeti la Rai linalomilikiwa na mmoja wa watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini, Rostam Aziz.

Katika toleo Na. 907 la Februari 10 – 16, 2011, Rai liliandika kuwa MwanaHALISI linapanga mkakati wa kuangusha serikali ya Kikwete.

Chini ya kichwa cha habari, “Mkakati mzito wa kuiangusha Serikali ya Kikwete wapangwa,” Rai lilidai MwanaHALISI linapandikiza chuki dhidi ya serikali ili wananchi wamchukie rais na serikali yake.

Kana kwamba haitoshi, gazeti lilishindilia madai yake kupitia safu ya maoni ya mhariri.

“Huu ni upuuzi mtupu. Kwanza siamini kuwa waandishi wenye akili wanaweza kuandika upuuzi wa aina hii. Yawezekana wanatumiwa kuficha kile ambacho mafisadi wanaandaa dhidi ya serikali ya Kikwete,” ameeleza Kubenea.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, Kubenea amesema tuhuma zilizoibuliwa na Rai ni chafu na nzito kiasi kwamba haziwezi kutoka kwa mwandishi wa habari dhidi ya mwandishi mwenzake.

“Hapa kuna watu wanaochukia jinsi gazeti letu linavyosakama ufisadi. Wamekaa chini, wakatunga tuhuma, wakaandika na kuwapa wahariri wanyonge wa Rai ili wawafanyie chapuo,” amebeza Kubenea.

Katika hali inayoonyesha kuweweseka na kutaka MwanaHALISI lifungiwe au lifutwe, gazeti la Rai limekwenda mbali hadi kulaumu wizara ya habari na usalama wa taifa kwa kutochukua hatua dhidi ya waliowaita wala njama za “kupindua serikali.”

Rai lilisema MwanaHALISI, kwa ushirikiano na vigogo maarufu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM); na mfanyabiashara mmoja anayedaiwa kuwa nusu ni mwana-CCM na nusu mpinzani, linashiriki mkakati wa kuangusha serikali ya Rais Kikwete.

Gazeti halikutaja majina ya “vigogo” wa CCM; jina la mfanyabiashara mwenye imani “nusu-nusu” wenye mkakati wa kupindua serikali; wala maelezo ya kina juu ya njama zenyewe.

Hadi gazeti hili linapelekwa mtamboni, si ikulu, usalama wa taifa au wizara ya habari, utamaduni na michezo iliyokuwa imetoa taarifa juu ya tuhuma hizo.

Kabla ya kununuliwa na Rostam Aziz, gazeti la Rai lilikuwa likimilikiwa na wanahabari sita nchini akiwemo Salva Rweyemamu, swahiba wa Rostam ambaye hivi sasa ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya rais.

“Ninawaomba wasomaji wa MwanaHALISI wapuuze uzushi wa Rai; waendelee kusoma gazeti letu lenye kutoa taarifa za kweli, sahihi na zenye ushahidi usiopingika,” amesema Kubenea.

Tuhuma za Rai – gazeti la Rostam – dhidi ya gazeti hili, zimetolewa katika wiki ambayo MwanaHALISI lilifumua habari za uchunguzi kuhusu makampuni yanayotuhumiwa kwa ufisadi.

Katika toleo Na. 228 (Februari 9-15, 2011), MwanaHALISI lilikuwa na habari kuu yenye kichwa kisemacho “Wizi wa Kagoda.”

Wakati serikali imekuwa ikidai kuwa haijui mmiliki wa Kagoda, gazeti liliweka wazi taarifa na nyaraka za Yusufu Manji, baba yake na kampuni yao, wakikopa kutoka Kagoda zaidi ya Sh. 30 bilioni.

Aidha, lilionyesha mahusiano ya serikali na wanaodai kukopa kutoka Kagoda Agriculture Limited, jambo ambalo lilifanya wengi wajiulize kwa nini serikali imekuwa na “ndimi mbili” – ikidai haijui Kagoda.

Katika toleo Na. 227 (Februari 2-8, 2011), MwanaHALISI liliandika katika habari kuu,  “Anayedai mabilioni ya Dowans ni Rostam Aziz.”

Taarifa ilionyesha kuwa Rostam ndiye anadai kupewa nguvu za kisheria (Power of Attorney) za kuwakilisha kampuni ya Dowans Holding SA ya Costa Rica katika kudai, kushitaki, kutetea, kufungua akaunti, kupokea na kuhamisha fedha za kampuni.

Habari zaidi kuhusu Rostam zilitokana na yaliyojiri katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara (ICC) katika shauri la Dowans na TANESCO.

Rostam, ambaye amekuwa akikana kuifahamu Richmond pamoja na Dowans, ameanikwa kuwa mwandani wa Dowans na aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika kuhamisha mkataba wa kampuni feki ya kufua umeme ya Richmond kwenda Dowans “kwa manufaa binafsi.”

Kuhusu Kagoda, nyaraka zinaonyesha wakili Bhyidinka Sanze wa kampuni ya mawakili ya Malegesi – Malegesi Law Chambers ya Dar es Salaam, akihusisha kampuni hiyo na Rostam.

Katika taarifa iliyotolewa chini ya kiapo kwa Kamati Maalum ya Rais ya kushughulikia wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT), Sanze anakiri kushuhudia ‘…mikataba ya Kagoda na makampuni mengine ya nje,’ ndani ya ofisi za kampuni ya Caspian Construction Limited inayomilikiwa na Rostam.

“Niliitwa na Malegesi ofisini kwa Rostam Aziz, 50 Milambo, Ofisi za Caspian Construction Limited. Nilipofika… niliwakuta Rostam Aziz, Peter Noni na Malegesi, wakaniambia fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya kugharamia uchaguzi wa CCM na rais wake,” alieleza Sanze.

Pembeni mwa habari ambayo MwanaHALISI limechapisha au ndani, kumekuwa kukichapishwa vivuli vya nyaraka kuthibitisha uhalisi wa uchunguzi.

Hatua ya Rai ya kujaribu kuwakokota wasomaji kutoka kwenye ukweli wa taarifa, nyaraka na tarakimu na kuwapeleka kwenye madai matupu, umeelezwa na mwandishi wa habari mahiri Joster Mwamgulumbi kuwa ni “kujidhalilisha kitaaluma.”

“Ni uandishi wa kina wa MwanaHALISI, unaokidhi viwango kitaaluma, ambao umewaudhi wamiliki wa Rai na wabia wao hadi kufikia kukimbilia kwenye gazeti lao kuporomosha tuhuma ambazo hata mjinga hawezi kuamini,” ameeleza Mwangulumbi ambaye ni kaimu mhariri wa gazeti hili.

Katika umri wake wa miaka mitano, MwanaHALISI limekuwa likifanya uandishi wa uchunguzi ambao umesukuma wengi kujirudi na hata serikali na baadhi ya watendaji wake kufurahia uibuaji wa taarifa zilizozuia wizi na ufisadi au kuvianika ili wahusika waweze kuchukua hatua.

Hii ni mara ya kwanza nchini kwa gazeti moja kutumiwa kutuhumu jingine kuwa linataka kupindua serikali.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili, tuhuma dhidi ya MwanaHALISI ziliandaliwa katika kikao nyumbani kwa Rostam Aziz, Mtaa wa Laibon, Kinondoni, jijini Dar es Salaam kwa lengo la “kumsafisha.”

Waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Salva Rweyemamu, anayekiri katika mahojiano yake na Kamati Teule ya Bunge kuwa alikuwa ofisa uhusiano wa Richmond iliyorithisha mkataba wake kwa Dowans isivyo halali.

Alikiri pia kuwa aliyemtabulisha kwa wanaojiita wamiliki wa Richmond nchini, ni Rostam Aziz. Uhusiano wao ungalipo kwa kiwango kikubwa.

Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Kennedy Fungamtama, wakili wa Rostam na Dowans ambaye amekuwa wakili wa Rostam katika kesi zake mbili dhidi ya MwanaHALISI.

Wajumbe wengine wawili wa kikao hicho walikuwa Dany Mwakitelekeko, naibu mhariri mtendaji wa magazeti hayo na Hussein Bashe, mtendaji mkuu wa kampuni ya New Habari Corporation Limited inayochapisha Rai.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, kikao nyumbani kwa Rostam kilianza saa 1:30 asubuhi, Jumatano 9 Februari 2011.

0
Your rating: None Average: 4.3 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: