Rai wametuvunjia heshima


editor's picture

Na editor - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

GAZETI la Rai, linalomilikiwa na mtuhumiwa mkuu wa ufisadi nchini, Rostam Aziz limeshusha tuhuma nzito dhidi ya MwanaHALISI kwamba lina mkakati wa kufanya uhaini.

Katika toleo lake Na. 907 la Alhamisi iliyopita, gazeti hilo lilituhumu MwanaHALISI katika habari iliyokuwa na kichwa; ‘Mkakati mzito wa kuiangusha Serikali ya Kikwete wapangwa’.

Rai lilisema mkakati huo unatekelezwa kwa ushirikiano na mfanyabiashara na vigogo wa CCM. Hawakutajwa majina.

Habari hiyo kubwa ambayo ilishindiliwa kwa maoni ya mhariri, Rai lililoanzisha utamaduni wa kushambulia magazeti mengine bila ushahidi, limedai MwanaHALISI linapandikiza chuki dhidi ya serikali ili wananchi wamchukie rais na serikali yake.

Aidha, likafanya kazi nzito ya kuwasafisha Rostam Azizi na Edward Lowassa kutokana na kuhusika kwao katika kashfa ya kuingiza kampuni feki ya kufua umeme ya Richmond pamoja na kampuni ya Kagoda ambayo inatuhumiwa kuchota fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA). Halafu limevitaka vyombo vya dola, Wizara ya Habari kuchukua hatua MwanaHALISI.

Hatupingani na juhudi za Rai kuwasafisha watu ambao kwa taarifa walizonazo wanaona kuwa wasafi. Lakini tunawashangaa kuandika habari zenye tuhuma nzito za uhaini bila kupata maoni ya watuhumiwa; vigogo wa CCM, mfanyabiashara na MwanaHALISI.

Taaluma inatuka kwamba tunapoandika habari yoyote lazima iwe na uthibitisho wa nyaraka au vielelezo au watu waliohojiwa katika uchunguzi. MwanaHALISI huzingatia hayo wakati wote.

Hata tukipopata uvumi kuhusu tuhuma fulani, tunafanyia kazi; tunahoji vyanzo mbalimbali, tunatafuta nyaraka na kuzikagua kikamilifu kabla ya kuchapisha. Hii ndiyo siri ya kuaminika hata ndani ya serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama.

Ni kwa msingi huo, Wizara ya Habari hawaoni tishio lolote katika habari zilizofuata misingi ya uandishi wa habari.

MwanaHALISI halijawahi na halitathubutu kuhusika katika njama za kuiangusha serikali si ya Rais Kikwete bali hata nyingine zijazo.

Tunawataka Rai watuombe radhi kwa kutuzushia na kutuchafua au waweke bayana uhusika wetu; wamtaje mfanyabiashara na wana CCM ‘wahaini’ na waeleze njama hizi zinafanyika wapi.

Mwisho tunawasihi wasomaji wapuuze uzushi wa Rai waendelee kusoma gazeti lao pendwa MwanaHALISI.

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: