Rais abebeshwa zigo la umeme


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

MVUTANO wa kisheria kati ya serikali na mabenki umezidi kuchelewesha mkopo wa Sh. 408 bilioni ulioombwa na Shirika la Umeme (Tanesco) na sasa umetua mezani kwa Rais Jakaya Kikwete.

Tangu Agosti mwaka jana kumekuwa na mchakato wa kupata mkopo kutoka mabenki kwa udhamini wa serikali lakini bila mafanikio.

Hii imetokana na kutokuelewana kati ya wizara mbili za serikali kwa upande mmoja; na serikali na mkopeshaji kwa upande mwingine.

Kutokana na mvutano huo, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo amemwandikia Rais Kikwete kumweleza kuwa bado kuna masuala ambayo yanahitaji “msimamo mbadala wa serikali kutoka ngazi za juu.”

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Meja Jenerali Robert Mboma “alimlima” barua Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja akimweleza kuwa kuchelewesha mkopo huo ni kumdharau Rais Kikwete ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Jenerali Mboma alipendekeza vifanyike vikao mbalimbali kati ya Tanesco na wizara hiyo, na hatimaye waonane na Rais Kikwete.

Kabla ya hatua ya Mboma kufikiwa, Mkulo amemwandikia Rais Kikwete akieleza sababu za kukwamishwa mkopo huo.

Masharti ya awali ya mkopo yalifikiwa baina ya Tanesco, benki ya NMB na NBC, ambazo katika majadiliano hayo zinaongozwa na Citybank Tanzania Limited.

Suala ambalo limeshindikana hadi sasa, ni matakwa ya mabenki, kuwa serikali idhamini mkopo huo kwa asilimia 100, wakati Sheria ya  Mkopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 inamtaka Waziri wa Fedha kutoa dhamana ya asilimia 85 tu.

“Iwapo serikali itaridhia vipengele kama hivyo kwenye mkataba itakuwa inakiuka sheria ya Mkopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 (kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2003) ambayo imemnyima waziri wa fedha kutoa fidia ya gharama au hasara kwa wakopeshaji na wakopaji,” amesema Mkulo katika waraka huo.

Hatua hiyo ya Mkulo inalenga kutoa maelezo kwa Rais Kikwete ambaye aliagiza, tangu Januari mwaka huu, kwamba mkopo huo upatikane haraka ili kuiwezesha Tanesco kupata umeme wa dharura.

Kabla ya kufikia hatua hiyo, mvutano ulikuwa kwenye ajenda ya jinsi ya kulipa mkopo huo na sheria gani zitumike. Wahusika wa pande mbili waliafikiana zitumike sheria za Tanzania na Uingereza kwa kutegemea nani anatoa fedha hizo.

Sheria ya Tanzania itatumika kwa dola za Marekani 115. 5 milioni (Sh. 188.1 bilioni) zitakazokopwa kutoka ndani ya nchi na sheria ya Uingereza itatumika kwa dola za Marekani 135 milioni (Sh. 219.9 bilioni) zitakazokopwa nje ya nchi.

Baada ya maafikiano ya awali, Citibank kwa niaba ya NMB na NBC, iliandaa rasimu ya mkataba wa dhamana inayozingatia masharti ya benki hizo, ambayo baadaye Tanesco, kupitia Wizara ya Nishati na Madini, iliiwasilisha kwa Wizara ya Fedha ili kupata dhamana ya mkopo husika.

Katika maafikiano hayo ya Februari mwaka huu, lilikuwamo pia suala la “mkataba mdogo wa mkopo wa dola za Marekani 65 milioni ambao ungewezesha Tanesco kupata fedha haraka.

Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Deni la Taifa (NDMC), ilikutana tarehe 20 Februari mwaka huu kujadili maombi ya Tanesco kupewa dhamana ya serikali.

Kamati ilibaini kasoro katika mchakato wa maombi hayo na ilikosa uhakika wa uwezo wa Tanesco kulipa mkopo huo.

“Kamati ilielekeza Tanesco wathibitishe uwezo wa kulipa mkopo huo na kumwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa ushauri wa kisheria kabla waziri wa fedha hajashauriwa kusaini dhamana hiyo,” amesema Mkulo katika waraka kwa rais.

Pamoja na kupata uthibitisho wa Tanesco na ushauri wa mwanasheria mkuu wa serikali kuwa Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 ifuatwe, NDMC iliunda kamati ya watalaam kupitia mikataba husika ili kujiridhisha kabla ya kumruhusu Waziri Mkulo kutoa dhamana.

Mikataba iliyopitiwa na hatimaye kusababisha Mkulo asitoe dhamana ya mkopo huo ni miwili:  Kati ya Tanesco na mabenki – ambao ulikuwa haujaidhinishwa na mwanasheria mkuu wa serikiali; na ule wa dhamana kati ya mabenki na serikali – ambao unasubiri uamuzi wa rais.

Hata hivyo, katika kikao cha kamati ya wataalam na mwakilishi wa mabenki, 22 na 23 Machi mwaka huu, walikubaliana serikali na mabenki yasaini mkataba mdogo wa mkopo wa dharura wa dola 65 milioni na mikataba mingine ishughulikiwe baada ya “fedha za haraka” kupatikana.

Haikuweza kufahamika iwapo fedha hizo za haraka zimepatikana.

Wataalam wameafikiana juu ya taratibu na sheria zipi zitumike kupata mkopo huo, lakini wameshindwa kuafikiana juu ya kiwango cha dhamana, suala ambalo Mkulo anaomba msaada wa ufumbuzi kutoka kwa Rais Kikwete.

Iwapo Citibank itaendelea kushikilia msimamo wake, rais atakuwa amebakia na njia mbili chungu: Ama avunje sheria ya nchi yake ya mikopo na dhamana ili Tanesco ipate mkopo; au agangamale na aukose mkopo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: