Rais ajutie mauaji


editor's picture

Na editor - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

INASIKITISHA kwamba mwenye madaraka hataki kuyaachia hata kwa sheria za mazonge zilizopo. Anatumia nguvu kuyahifadhi. Hiyo inaashiria kuchoka kufikiri.

Tanzania tumefika hapo. Viongozi waliopo madarakani – na hapa tuseme wazi ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) – wamechoka kufikiri.

Utamu wa madaraka umewalevya. Tena umewalevya kisawasawa. Hawaoni wala hawasikii. Wanataka kuhakikisha madaraka wanayotamba nayo usiku na mchana, kuwa wamepewa kwa ridhaa ya wananchi yanabaki kwao; iwe iwavyo.

Kama walivyo wenzao kwingineko Afrika, nao wanatumia misuli kuyahifadhi. Wanalinda “utamu.” Mazoea yana taabu, kuyakosa ni adhabu.

Tatizo ni kwamba tayari nao wameanza kupenda damu. Hawajali damu inamwagika mradi wahifadhi madaraka. Hawajui kupenda damu ni ushetani. Labda wanajua bali hawajali.

Waliua kule Zanzibar, mwaka 2001. Wakati ule, Benjamin Mkapa akiwa rais na amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama. Akapokea damu mikononi. Angalau aliunda tume ikathibitisha kweli dola imeua raia wema.

Kule tu kutoshughulikiwa kama walivyofanyiwa kina Slobodan Milosevic wa Kosovo, Albert Fujimori wa Peru na sasa Charles Tailor wa Liberia hakukuwapa fundisho lolote.

Mkapa na wenzake katika CCM hawakuona ubaya wowote kwa kumwaga damu ya wananchi wadai haki. Si ilikuwa damu ya mafukara wakubwa! Wajali nini?

Kweli hawakujali. Miaka tisa haijatimia vizuri, wameruhusu damu imwagike tena. Safari hii mkoani Arusha. Wamemwaga damu mchana kweupe.

Ona wanavyoadhirika. Wanasema tukio lile lilikuwa la “bahati mbaya.” Jaji humhukumu kifo muuaji aliyemthibitisha kubeba panga, akaondoka alipo, akamfuata mtu masafa, alipomkuta, akamtwanga pwaa. Mtu yule kakata roho. Basi muuaji alikusudia kuua.

Polisi wa Arusha na washirika wao walitoka kituoni na silaha. Walipewa na risasi. Ni za moto. Wakaondoka kwa amri ya wakubwa wao kwenda walikoambiwa.

Walikuta waandamanaji. wakawaelekezea bunduki. Wakaweka risasi chemba. Wakadofyoa vidole zitoke. Zikatoka.

Wametekeleza amri ya “piga, piga, piga.” Wakapiga risasi za moto. Hapo wananchi wanaambiwa, “Mauaji yale ni tukio la bahati mbaya.” Haikubaliki.

Bahati mbaya ni kauli ya Rais Jakaya Kikwete. Bali kwa vyovyote, mauaji hayakubaliki. Yanapotekelezwa ovyo, ni dhambi kubwa isiyosameheka. Si rais wala kiongozi yeyote mwingine awezaye kuumba. Hawapaswi kuua. Marufuku.

Tunataka uchunguzi wa kina. Kama kweli rais alitoa amri, atoke tena hadharani. Atoe kauli mpya. Ajute dola kuua raia. Aseme hasa, “Ndugu wananchi, nimekoma sitaruhusu mauaji rahisi hivi.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: