Rais akwepa kuwaudhi mafisadi


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 20 October 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

NIMEPATA kigugumizi kuhusu mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete.

Upande mmoja nampenda Kikwete kwani kuna mambo mengi mazuri yametokea chini yake, ambayo ninaamini yasingeweza kutokea chini ya rais mwingine.

Hata hivyo, baadhi ya mambo hayo hayo mazuri yananifanya upande mwingine nisiwe na hamu ya kumwona anatawala tena kwa miaka mingine mitano.

Kuna vitu ambavyo Kikwete amefanya (au hakufanya) ambavyo vinanifanya nione kuwa ilikuwa vyema kabisa kwa yeye kuwa rais miaka mitano iliyopita, lakini nikiviangalia vitu hivyo hivyo tena, na kujaribu kuviona vinatokea miaka mitano ijayo, najikuta sina hamu. Lakini bado ninampenda Kikwete.

Kwanza ni kwa sababu ya uvumilivu wa hali ya juu aliouonesha katika utawala wake. Watu wengi bila ya shaka hawakumbuki mwanzoni alipoingia madarakani ilikuwaje.

Baada ya gazeti moja la Kenya kuchapisha katuni iliyomwonesha Kikwete akiwa amekaa kwenye kiti huku waandishi wakiwa wanamlamba miguu (viatu), baadhi ya magazeti yakabadilika na kuanza kumkosoa.

Serikali nayo ikaja juu ikatisha wananchi waache kumwandika vibaya Kikwete.

Katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba alijitosa kwa kupiga mkwara waandishi ili wasimwandike vibaya rais eti kwa vile yeye ni “Amiri Jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama” hivyo kwa uandishi wa kumchokoza kunaweza kumfanya Rais atumie hulka yake ya kijeshi.

Alikumbusha kuwa Kikwete aliwahi kupitia jeshini hivyo, mtu aliyepitia jeshini hulka hiyo haimtoki. Lakini lilipokuja suala la mapanki waandishi na wachambuzi wakaanza kuchambua kauli za Rais Kikwete na kuzihoji.

Aidha, waandishi wa habari walichambua kwa kina matukio ya utiani saini nje ya nchi mkataba wa mgodi wa Buzwagi, uchotaji wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT), mkataba wa uidhinishaji kampuni ya Richmond. Uchambuzi mwingine ulifikia hatua ya kumvunjia heshima Rais Kikwete.

Hapo likatokea kundi la watu walioshinikiza serikali ishughulikie vyombo vya habari au waandishi wa habari walioonekana kuandika habari zilizodaiwa za “kumdhalilisha” Rais.

Mambo ambayo yamesemwa, kuandikwa, kujadiliwa, kuchorwa na hata kusimuliwa kuhusu Rais Kikwete kama yangefanyika kwa mtu mwingine huenda magazeti kadhaa yamefungwa, waandishi wangetiwa pingu na “wanaharakati” kusimamishwa kizimbani kwa madai ya uchochezi.

Hata baadhi ya watu wamekuwa wakiyachukulia maandishi yangu kuwa ni ya “kichochezi”. Hawa wangepata nafasi kwa kweli wangenishughulikia mapema tu.

Kwa hiyo kama ni suala la uvumilivu wa kisiasa binafsi nampa Rais Kikwete alama 100. Sijui kama Dk. Willibrod Slaa akishinda na akaingia ikulu ataweza kuvumilia kuandikwa, kukosolewa na kuchambuliwa?

Jambo la pili ni kuwa Rais Kikwete hapendi kuonekana kuwa ni adui wa mtu yeyote; anataka aonekane anapendwa. Wanasiasa karibu wote duniani wanapenda kupendwa na ni vigumu sana kumpata mwanasiasa asiyefurahia kupendwa, na kwa namna fulani, hakuna mwanadamu asiyependa kupendwa.

Lakini wapo baadhi ya watu ambao kupendwa linakuwa takwa la aina fulani. Hawa wanajikuta wanalazimisha kupendwa ama kwa kufanya mambo fulani au kutofanya mambo fulani.

Kikwete ili apendwe zaidi hataki kuwa na uadui wa wazi na mtu yeyote. Mwanzoni, watu walikuwa wanafurahia sana tabasamu lake kiasi kwamba akawa anajulikana kama “Kijana Mtanashati” japo kwa kweli ujana alikuwa ameshaupita.

Hii ilimlazimu hata katika hotuba yake mojawapo kuwaonya watu kuwa yeye ni mtu makini sana na hana mchezo katika uongozi hivyo wasidanganywe na “tabasamu” lake. Lakini mvuto wake huo bila shaka haukuanzia kwenye urais bali ni wa muda mrefu, hivyo anajua kuwa anapendwa.

Ndiyo maana Kikwete hataki kujitengenezea maadui. Matokeo yake ni kuwa hata zilipotokea changamoto kadha wa kadha za kitaifa hakuwa mkali jinsi ilivyostahili bali alijipima na kufanya maamuzi ya wastani.

Kuanzia jinsi alivyoshughulikia suala la Buzwagi au kashfa za Benki Kuu au matatizo mengine ya kiuongozi, Rais Kikwete hakutaka kuchukua hatua kali zilizotakiwa, badala yake aliamua kutafuta njia za katikati ili asionekane adui.

Hili lilijidhihirisha zaidi wakati wa mgogoro uliowekwa kiporo ndani ya CCM kati ya pande mbili za wabunge wake. Mgogoro ule ulimweka pagumu kuchagua upande mmoja na kuukana mwingine.

Lakini baada ya kugundua kwamba akichagua upande mmoja waziwazi, upande mwingine utamwona adui aliamua kutokuwa na upande wowote.

Matokeo ya kutaka kupendwa daima Rais Kikwete hawezi sasa kuzungumzia ufisadi kwenye majukwaa ya siasa au hata kutumia neno hilo. Katika kampeni zake, kwa kiasi kikubwa hajasikika akitambua kuwa ufisadi ndilo tishio kubwa zaidi kwa nchi wakati wa amani kuliko vita (kama alivyosema Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere).

Hawezi kusema hivyo, maana akithubutu atawaudhi mafisadi, makuwadi wa ufisadi au vikaragosi wa ufisadi wakati yeye hataki kuonekana adui yao.

Ni kutokana na haya mawili, watu wanakuwa kama swala aliyemulikwa kwa tochi kizani. Itawezekana kumnyima upendo huo Rais Kikwete kwenye sanduku la kura?

Je, wale ambao wanampenda kwa sababu ya tabasamu lake, uvumilivu wake na utulivu wake lakini hawakubaliani na jinsi anavyoongoza hawatajisikia kama wanamwonea kwa kumnyima kura?

Je, yumkini si wapo ambao watapiga kura kumchagua si kwa sababu wanafurahia matokeo ya uongozi wake miaka mitano iliyopita bali kwa sababu wakimwona wanajisikia “burudani” katika mioyo yao na roho zao zinasuuzwa?

Je, mtu anaweza kumkataa mwanasiasa ambaye anampenda lakini hakubaliani na sera zake? Maswali haya yanahitaji kujibiwa na kujibiwa kabla ya kufika kwenye sanduku la kura.

Kwamba, ndiyo unampenda Rais Kikwete na unaamini ni mtu mzuri na mchangamfu, mwenye haiba na mvuto wa binafsi na kisiasa, lakini, je, unataka atawale tena miaka mitano ukiangalia miaka mitano iliyopita?

Kwa vile Kikwete hajasimama na ajenda ya mabadiliko katika kampeni hii (siyo kupigana na ufisadi wala kufanya mabadiliko katika sekta mbalimbali) bali kuendeleza yale aliyoyaanza au waliomtangulia, je, uko tayari kukaa chini ya miaka mingine mitano ya uongozi ule ule, wenye ajenda ile ile na sera zile zile ambazo zimetufikisha hapa tulipo? Fikiria sana.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: