Rais ameshindwa 'kumaliza kiu'


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 15 September 2009

Printer-friendly version
Gumzo

MUDA wa saa mbili uliotengwa kwa Rais Jakaya Kikwete kujibu maswali ya wananchi kupitia vyombo vya habari haukutosha.

Ni Alhamisi iliyopita, pale rais alipowasiliana na wananchi kupitia njia iliyoitwa, "maswali ya moja kwa moja." Huu ni utaratibu mpya. Ni tofauti na ule wa awali wa kuhutubia taifa kila mwisho wa mwezi.

Maswali saba yaliulizwa na wasikilizaji kupitia njia ya simu, 2,500 yaliwasilishwa kupitia ujumbe mfupi wa simu za mkononi (sms) na 500 yaliulizwa kupitia barua pepe.

Ni maswali machache sana kati ya hayo yaliyoulizwa kwa njia ya simu na barua pepe yaliyopata nafasi ya kujibiwa. Mengi hayakujibiwa ingawa rais aliahidi kujibu wote waliouliza.

Baadhi ya wananchi waliotaka kuuliza hawakupata fursa ya kufanya hivyo; wachache waliobahatika maswali yao hayakupata majibu yaliyotarajiwa.

Badala yake, majibu mengi ya rais kwa baadhi ya maswali yamezalisha maswali mapya na kuibua mjadala mwingine mpana zaidi.

Ni kweli kwamba rais aliyajibu kwa ufasaha baadhi ya maswali yaliyoulizwa kwa njia ya simu, sms na barua pepe.

Hakuna uhakika hadi sasa, kwamba majibu yale yalitokana na kile kinachodaiwa kuwa baadhi ya waulizaji kuandaliwa kabla na baadhi ya maswali kupelekwa kwa rais mapema na hivyo yeye kuwa ameyatafutia majibu.

Miongoni mwa maswali ambayo rais alijibu kwa ufasaha ni kuhusu tatizo la baadhi ya mikoa kuwa nyuma kimaendeleo hasa ya barabara, ikiwamo ile iliyopo pembeni mwa nchi.

Katika hili, rais alieleza kuwa kuna miradi mbalimbali ya barabara inayotarajiwa kujengwa na inayojengwa sasa nchini, iko wapi, nani anaifadhili, kiasi gani na lini mradi utaanza au kukamilika.

Lakini miongoni mwa maswali ambayo hayakupata majibu au majibu yake hayakuzima kiu ya baadhi ya wananchi na ambayo sasa yamefungua mjadala mpya, ni kuhusu suala la serikali kushindwa kufikisha mahakamani baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi.

Rais alijitetea kwamba kazi ya kufikisha au kutofikisha mahakamani watuhumiwa, haiko katika mamlaka yake. Ni kazi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Hoja ilitokana na hatua ya serikali kushindwa kufikisha mahakamani watuhumiwa wa ufisadi wa kampuni ya Richmond Developement Company (LLC) na Kagoda Agricuture Limited.

Inatamkwa katika maongezi ya wengi kuwa kigugumizi cha serikali katika hili kimetokana na baadhi ya watuhumiwa kuwa na urafiki na rais.

Ni kweli kwamba DPP akijiridhisha na ushahidi uliokusanywa na vyombo husika, sheria inampa mamlaka kuelekeza muhusika kufikishwa mahakamani. Asipojiridhisha basi. Hakuna mwenye mamlaka ya kuhoji uamuzi wake.

Hata hivyo, wakati hilo likiwa ndilo jukumu la msingi la DPP linalotambulika kisheria, kuna kila dalili kuwa baadhi ya kazi zinazofanywa na ofisi hiyo zinaathiriwa na utawala.

Kwa mfano, katika sakata la fedha zilizokwapuliwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), aliyeamuru nani ashitakiwe na nani asishitakiwe alikuwa ni rais.

Ni Rais Kikwete aliyesema wakati akihutubia Bunge la Jamhuri mjini Dodoma, katikati ya mwaka jana, kuwa watakaorudisha fedha wasifikishwe mahakamani.

Alisema fedha hizo hazikuwa za serikali, bali zilikuwa za wafanyabiashara wa nje waliokuwa wanawadai wafanyabiasahara wa Tanzania na hivyo serikali haina ilichopoteza.

Aliamuru watuhumiwa kurejesha fedha hizo serikalini. Aliunda kamati ya watu watatu kuratibu kazi hiyo na aliagiza wale watakaoshindwa kufanya hivyo, ndiyo wafikishwe mahakamani.

Hata tarehe ya mwisho ya watuhumiwa kurejesha fedha ilitolewa na rais mwenyewe.

Hivyo basi, katika mazingira haya, wananchi wana kila sababu ya kujenga mashaka iwapo rais hakushauri au kushinikiza baadhi ya watuhumniwa wasifikishwe mahakamani.

Kwamba, pamoja na kuwapo kwa jinai inayotokana na tendo la kughushi nyaraka, kudanganya na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, agizo la rais limezuia wahusika waliorudisha fedha kufikishwa mahakamani.

Kutokana na hali hiyo, rais hawezi kusema kwamba agizo lake hilo lililotolewa kwa kisingizio cha "tunataka fedha zetu kwanza," halikuathiri utendaji kazi wa DPP.

Wala hawezi kusema kuwa ofisi ya DPP katika hali hii, ilitenda kazi zake kwa uhuru na ilitumia mamlaka yake kutimiza wajibu wake. Wala rais hawezi kukwepa lawama kuwa hapa alivuka mipaka kwa kufanya kazi za DPP.

Hivyo aliyeamua nani afikishwe mahakamani na yupi asifikishwe, si DPP. Ni rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tayari kuna madai kuwa kauli ya rais ya kutetea watuhumiwa waliorudisha fedha, ndiyo iliyotumika kama msahafu katika ofisi ya DPP katika kuamua nani ashitakiwe na nani asishitakiwe.

Kwanza, kauli ya Kikwete ya kusamehe watuhumiwa ni kinyume na katiba ya Jamhuri inayompa rais uwezo wa kutoa msamaha.

Katiba haitoi fursa kwa rais kusamehe bila wahusika kwanza kufikishwa mahakamani, kusomewa mashtaka na kupatikana na hatia.

Pili, kwa kutoa "misamaha," rais ameingilia kazi za mamlaka nyingine. Amekwenda tofauti na katiba inavyoagiza na ametenda kinyume na misingi ya utawala bora.

Tatu, hata usiri uliofuata juu ya nani amerudisha fedha, yupi hakurudisha au nani anastahili kufikishwa mahakamani na nani hakustahili, kumechangiwa kwa kiwango kikubwa na amri hiyo ya rais.

Nne, kuruhusu baadhi ya watu kushitakiwa na baadhi kutoshitakiwa ni kufanya ubaguzi. Ubaguzi unakatazwa na katiba ya nchi.

Haya ni katika ukwapuaji wa fedha za EPA ambapo kampuni ya Kagoda pekee ilichotewa na serikali na washirika wake, zaidi ya Sh. 40 bilioni katika mazingira tata.

Ukiacha hilo, kuna suala lililohusu kile kinachoitwa sasa, "Zigo la Richmond." Rais alisema ni yeye aliyezuia malipo ya awali kufanywa baada ya waziri wake kutaka kufanya hivyo.

Amekiri kuwa Richmond haikufanyiwa uhakiki na serikali haikuweza kubaini kama Richmond ilikuwa kampuni ya kitapeli, hadi pale Kamati Teule ya Bunge ilipoundwa na kuichunguza.

Lakini rais akafika mbali zaidi pale aliposema kuwa serikali haijaweza kubaini iwapo kulikuwa na mazingira ya rushwa katika kufikia mkataba huu.

Sasa swali la kujiuliza: Nani ambaye anaweza kugundua rushwa, iwapo watuhumiwa wote wameachwa katika nafasi zao mpaka sasa?

Serikali haiwezi kusema kwamba hakuna ushahidi wakati Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Edward Hoseah na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na baadhi ya watumishi wengine wa ngazi za juu katika serikali, hawakuwa wameondolewa wakati uchunguzi ukifanyika.

Serikali inakiri kwamba Hoseah hakutenda kazi zake inavyotakiwa. Kwamba kabla ya kutoa taarifa yake kwa umma, hakujiridhisha kama kweli kampuni ya Richmond ilisajiliwa nchini au hapana.

Kwamba hakuwa makini katika uchambuzi wa taarifa zinazowasilishwa kwake na wasaidizi wake; alitoa taarifa kuwa Richmond haikuwa katika kashfa yoyote ya rushwa.

Rais Kikwete anajua kuwa ni Hoseah huyuhuyu ambaye amepewa jukumu la kutambua mianya ya rushwa, ndiye aliyekaririwa akisema kuwa bunge halina mamlaka ya kufanya kazi ya uchunguzi bali taasisi yake.

Je, mtu wa aina hii, anawezaje kuona mianya ya rushwa wakati tayari aliishaonyesha kulalia upande mmoja?

Hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali hawezi kuwa mtu muhimu katika kuangalia suala hilo.

Mwanyika huyu ndiye aliyeshindwa kuishauri serikali katika mkataba wa Richmond, hivyo hawezi kujihangaisha kutafuta taarifa juu ya ukweli wa kampuni kuhonga baadhi ya watendaji serikalini.

Kikwete angalau angeeleweka iwapo angeweka pembeni wahusika wote wakati uchunguzi ukifanyika. Kusema tu, kwamba hakuna rushwa wakati wahusika bado wanaendelea na nafasi zao, hakuwezi kusaidia serikali kujisafisha.

Swali jingine ambalo limeanzisha mjadala ni lile lililoulizwa na Jacob Mkama wa Ukerewe, mkoani Mwanza ambaye alimueleza rais kuwa serikali inaonekana imeshindwa kupambana na rushwa na ufisadi.

Katika hilo, rais alisema serikali yake imeimarisha utendaji kazi wa TAKUKURU kwa kuajiri watumishi zaidi na kuwapa mafunzo pamoja na vifaa vya kufanyia kazi.

Lakini bado tatizo ni lilelile. TAKUKURU ambayo rais anasema ameimarisha inaendelea kuwa chini ya uongozi uleule ulioshindwa kubaini "madudu" ya wazi katika sakata la Richmond.

Hapa haraka wananchi wanaweza kudhani kuwa rais, kama taasisi isiyokuwa na meno, hawezi kutekeleza kile alichoahidi.

Hoja hii inapata nguvu hasa katika hili, kwamba, hata baada ya bunge kumaliza kazi, rais ameshindwa kuwaweka pembeni watuhumiwa angalau kuruhusu uchunguzi huru na wa haki.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: