Rais asisemewe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 23 December 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

BAADA ya kauli za kutatanisha kuwahi kutolewa mara kadhaa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba hata kuonekana anatetea watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini, inatia uchungu kukuta bado viongozi wanadhani si sahihi kuendelea kujitapa.

Wakati Watanzania hawajaridhika na sababu zinazotolewa na viongozi wa serikali za kutodhibiti ipasavyo watuhumiwa wakubwa wa ufisadi, anatokea waziri mwingine na kueleza kile tunachoona ni kauli zinazozidi kuchefua akili za watu.

Wiki iliyopita, Waziri wa Sheria, Mathias Chikawe alinukuliwa na vyombo vya habari nchini akisema kwamba Rais Kikwete hana mamlaka ya kukamata na kufikisha mahakamani watuhumiwa ufisadi.

Anadai kuwa katika kipindi cha mfumo wa uchumi wa kibepari ambacho Tanzania inapitia, iwapo rais atafanya hivyo atakuwa anavunja misingi ya utawala wa sheria.

Waziri Chikawe anasema kazi ya kukamata na kushitaki inafanywa na vyombo vya dola kwa kufuata sheria, vinginevyo, anasisitiza, “mfumo uliopo wa serikali unatoa tahadhari dhidi ya ukamataji watu ovyo.”

Lakini pia, anasema bunge halina uwezo wa kuibana serikali hadi itekeleze inachotaka isipokuwa inachoweza kufanya ni kuishauri tu. Anasema nguvu ya bunge imemezwa kisiasa.

Maelezo haya yanaumiza roho. Pamoja na kutambua umuhimu wa serikali kuendesha shughuli zake kwa kufuata sheria na misingi ya utawala bora, hatuoni kama ni sahihi kusema rais hana mamlaka ya kukamata na kushitaki watuhumiwa.

Kwanza rais ndiye kiongozi mkuu wa dola. Na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mwenye mamlaka ya kuendesha nchi kwa niaba ya wananchi.

Tunatambua rais anaongoza kupitia baraza la mawaziri na taasisi mbalimbali zilizoundwa kisheria kwa mujibu wa Katiba zinazotambuliwa kama mihimili mingine ya dola, mbali na serikali. Hizi ni Mahakama na Bunge.

Tunajua kuna taasisi nyingine za kisheria zinazotumika kusaidia kazi ya utoaji haki. Hizi ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Jeshi la Polisi.

Rais ndiye anateua wakuu wa taasisi hizi ambao wanatumia mamlaka aliyowapa. Wanakamata, wanachunguza na kushitaki watuhumiwa kwa kuwafikisha mahakamani.

Bali inaeleweka pasina shaka kwamba rais ana mamlaka ya kiutawala yanayomwezesha kumsimamisha au kumstaafisha ofisa yeyote kazi aliyomteua kuifanya iwapo anahisi hakuna maslahi tena kwa mteule huyo kuongoza.

Na hivi ndivyo anavyoweza kutenda dhidi ya watuhumiwa ufisadi katika taasisi alizowateua kuongoza. Wapo wakuu wa taasisi wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi.

Waziri Chikawe tunauliza, basi hata hawa rais hana mamlaka ya kuwadhibiti? Si kweli hata kidogo.

0
No votes yet