Rais bora hapimwi kwa mambo madogo


Mulokozi Eligius's picture

Na Mulokozi Eligius - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

NIMEVUTIWA na mjadala ulioanzishwa na Salva Rweyemamu katika gazeti hili, kwamba ni Rais Jakaya Kikwete pekee aliyefanikiwa kuleta maendeleo, ikilinganishwa na marais waliomtangulia, ukiondoa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Salva alikuwa akijibu kauli ya Profesa wa uchumi, Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF).

Kwanza, Nyerere aliamini kwamba taasisi ya urais ni ngumu na si kila mtu anaweza kuishika. Alisema urais ni mzigo, na kwamba ikulu ni mahali patakatifu. Alitahadharisha kuwa ikulu si mahali pa kukimbilia kwa mtu mwadilifu.

Lakini nionavyo sasa, Rais Kikwete amewafanya Watanzania waamini kuwa urais si jambo gumu, na kila mtu aweza kuwa rais. Chini ya utawala wake, wananchi wameshuhudia mambo mengi yasiyo na maana kuliko ilivyokuwa kwa watangulizi wake, Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi.

Angalau Mkapa na Mwinyi walileta maendeleo, ikilinganishwa na Kikwete. Chini ya utawala wa Mkapa miradi mingi ya barabara ilitekelezwa, tena kwa kiwango cha lami. Si hivyo tu, serikali ya Mkapa angalau ilikusanya kodi na ilifanikiwa kusimamia mapato yake, huku ikiboresha vituo vya afya, zahanati na kusimamia ujenzi wa shule za msingi na sekondari.

Ni kipindi kile ambacho Mkapa aliteua waziri mwenye kujua kazi yake wa kusimamia barabara, John Magufuli. Karibu asilimia 75 ya miradi yote mikubwa ya sasa ya barabara, ilianza kipindi kile. Mfano ni barabara ya Dodoma-Singida-Shelui hadi Mwanza.

Wengi wanakumbuka ndoto za Magufuli, za kutaka magari madogo yatoke Mtwara mpaka Mwanza na pengine Kagera bila ya kukanyaga barabara ya vumbi. Tunazungumzia kilomita 3,000.

Hata barabara zilizokwishajengwa na zinazojengwa sasa jijini Dar es Salaam, kama vile barabara ya Mandela-Sam Nujoma na ile ya Kilwa, zote ni mikakati iliyoandaliwa na serikali ya Mkapa, ingawa kuna watu wanataka mafanikio hayo kuyakimbizia kwa Kikwete.

Maboresho kwenye sekta ya elimu nayo yalianzia wakati wa Mkapa. Binafsi nakumbuka jinsi Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ilivyoanza kufanya kazi mwishoni mwa mwaka 2005 kwa lengo la kuongeza idadi ya wasomi nchini.

Ni Mkapa aliyeteua Nimrod Mkono kuwa mwenyekiti wa Bodi hiyo na mara moja alianza kupigia debe wanafunzi kwenda kukopa katika bodi hiyo kwa maelezo kwamba kuna fedha za kutosha.

Waliobahatika walipata mikopo kwa asilimia 100. Hayo yalifanyika kabla ya Kikwete kuingia madarakani. Lakini angalia jinsi wanafunzi walivyonyanyasika kusotea mikopo chini ya serikali ya rais Kikwete.

Suala la kusema kwamba tunasomesha wengi lakini bila kukidhi mahitaji yao, halisaidii. Kujenga madarasa mengi huku yakikosa walimu si maendeleo, wala kuwa na walimu wengi wanaopunjwa maslahi yao siyo kutoa elimu bora.

Pamoja na upungufu mwingine, lakini angalau Mkapa alisimamia vizuri hayo ikilinganishwa na sasa.

Watanzania watamkumbuka Mkapa kwa jinsi serikali ilivyosimamia Mpango wa Elimu Maalum kwa Walioikosa (MEMKWA), Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA), MKURABITA, MKUMBITA na TASAF.

Wakati Mkapa anamwachia kijiti Kikwete, kilo moja ya sukari ilikuwa kati ya Sh. 550 na Sh. 600. Leo hii, sukari inauzwa kati ya Sh. 1,200 na 1,300. 

Unga wa sembe ulikuwa ni kati ya Sh. 250 na 300, sasa ni kati ya Sh. 700 na 1,000. Hali ni hivyohivyo katika maharage, nyama na sabuni na mafuta ya kupikia.

Pamoja na ahadi yake ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania, maisha ya wananchi kwa miaka minne ya Kikwete yamepanda maradufu kuelekea kubaya.

Inaonekana Salva na wenzake wanashindwa kumwambia ukweli Kikwete, kwamba hali za wananchi mijini na vijijini ni mbaya kuliko ilivyokuwa kabla ya yeye kuingia madarakani.

Badala yake wateule wake wanamwongopea na vitu vidogo kama vile kuwa rais wa kwanza wa Afrika kuonana na Rais wa Marekani, Barrack Obama; rais mwenye mvuto zaidi Afrika Mashariki; kuongea na wananchi kupitia luninga na radio moja kwa moja na kuleta kocha wa kuinoa timu ya taifa (Taifa Stars).

Rais bora hapimwi kwa kuleta kocha au kukutana na Obama. Kipimo ni uongozi wake uliotukuka na uwezo wake wa kubadilisha maisha ya wananchi anaowaongoza. Kikwete, hata kama ataonana na Obama kila siku, kama mikutano yake hiyo haina tija kwa taifa, basi ni kazi bure.

Tunapokwenda Marekani na kujisifu kwamba sisi ndiyo nchi pekee yenye madini ya Tanzanite katika bara la Afrika na duniani, lakini ikiwa madini hayo hayawasaidii wananchi, tunapata nini?

Au ikiwa tunajisifu kwa kuuza vitalu vya uwindaji wakati watoto wetu hawana madawati shuleni, hospitali hazina dawa; majigambo hayo yana faida gani?

Eh, tunajisifia kwa kuwa na ardhi kubwa yenye rutuba na maji ya kutosha wakati watu wetu wanakufa kwa njaa? Tunajisifia kwamba Kikwete ameleta maendeleo kuliko watangulizi wake, wakati watu wetu vijijini Loliondo wanachomewa nyumba zao; kisa tunataka kumpa nafasi mwekezaji wa kigeni?

Kitu pekee ambacho Kikwete mpaka sasa anaweza kujivunia ni kule angalau kupeleka mahakamani baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi. Pamoja na kwamba vita dhidi ya ufisadi haviendi kama wananchi wanavyotarajia au rais alivyoahidi, katika hili angalau kuna maendeleo kidogo, kama itathibitika kuwa hatua hizo siyo za kiini macho.

Waswahili husema, "Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni." Katika hili ametenda. Hata kule kukubali kwa shingo upande kujiuzulu kwa swahiba wake mkuu, aliyekumbwa na kashfa ya mradi tata wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond, Edward Lowassa, ni kitu kinachoweza kupigiwa mfano.

Mjadala unaendelea.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: