Rais Jakaya Kikwete dhaifu?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 14 September 2011

Printer-friendly version
Ni taarifa za WikiLeaks
Adaiwa kumuogopa CDF
Rais Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete amezidi kuandamwa. Sasa anaitwa “dhaifu na anayetishwa na wasaidizi wake.”

Mtandao wa WikiLeaks unaoibua taarifa za siri za kibalozi duniani, umeandika kuwa Rais Kikwete aliwahi kumwogopa mkuu wake wa majeshi, Jenerali Mwita Waitara.

Kinachoitwa udhaifu wake ni hatua ya kukatalia Marekani kuweka nchini kituo cha majeshi ya ushirikiano – Africa Contingency Operations Training Assistance (ACOTA).

Taarifa zinasema Kikwete alighairi ahadi yake ya kuwa na mradi huo kwa kuwa ulikuwa ukipingwa na Jenerali Waitara.

Rais Kikwete anaelezwa kuwa alikuwa amekubali, mara baada ya kuingia madarakani Desemba 2005, mpango huo wa Marekani unaodaiwa ungesaidia wanajeshi wa Tanzania kupata mafunzo ya kulinda amani katika ukanda wa Afrika na serikali kunufaika kwa misaada kifedha.

WikiLeaks inamnukuu aliyekuwa balozi wa Marekani nchini, Michael Retzer akisema kukwama kwa mpango huo kulitokana na Jenerali Waitara “kuuwekea ngumu.”

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja wiki moja baada ya Balozi Retzer kunukuliwa na mtandao huo akisema Rais Kikwete, alilipiwa na Ali Albwardy, raia wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) nauli ya kwenda Uingereza na kurudi.

Alinukuliwa akisema pia kuwa Rais Kikwete “aliwezeshwa” kiasi cha dola milioni moja za Kimarekani (sawa na Sh. 1.6 bilioni), kwa ajili ya shughuli za kutafuta urais mwaka 2005.

Ali Albawardy, ambaye ni mmiliki wa hoteli maarufu jijini Dar es Salaam, Kilimanjaro-Kempinski.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu alikana madai hayo akisema, “Rais Kikwete hakuwa akikusanya fedha” za chama chake.

Ikulu ilimwita Balozi Rezter mzushi, muongo na ikasema Rais Kikwete hajawahi kufadhiliwa na bilionea mmiliki wa Kilimanjaro-Kempinski.

Taarifa zinamnukuu Balozi Retzer akisema utawala wa Kikwete ulikuwa unapitia katika wakati mgumu kati ya raia na jeshi, kutokana na hatua ya mkuu wa majeshi “kuzuia” rais na waziri wa ulinzi kuchukua hatua ya kuanzishwa kwa mafunzo hayo.

Hata hivyo, Balozi Retzer anasema, “Lakini hatukukata tamaa kwa kuwa mkuu wa majeshi alikuwa anakaribia kustaafu, 31 Julai 2006 na Rais Kikwete aliahidi kuanzishwa mafunzo hayo baada ya Waitara kuondoka.”

WikiLeaks inasema tarehe 2 Mei 2006, aliyekuwa waziri wa ulinzi, Profesa Juma Kapuya aliomba kukutana na balozi ambapo aliomba radhi kwa kucheleweshwa mafunzo hayo.

Profesa Kapuya amenukuliwa akimhakikishia Balozi Retzer kwamba mafunzo ya ACOTA yangeanza muda wowote baada ya Waitara kustaafu. 

“Kama ilivyodhaniwa, utawala wa Kikwete unakumbana na mvutano wa kiraia na kijeshi. Mkuu wa majeshi ya ulinzi Tanzania anazuia rais na waziri wa ulinzi kuchukua hatua ya kuanzisha mafunzo ya kulinda amani chini ya (ACOTA),” linaeleza WikiLeaks, likinukuu Balozi Retzer.

Balozi ananukuliwa akisema mafunzo hayo yalilenga “kufundisha vikosi vitatu vya kulinda amani ifikapo 2008, mafunzo ya kwanza yakiwa yamepangwa kufanyika Machi 2007.”

Hadi Mei 2007, mafunzo hayo yalikuwa bado hayajaanza na Balozi Rezter ananukuliwa akisema, “…ni muhimu kuelewa kwamba Jenerali Waitara anakumbatia sera za ulinzi za kijamaa na amekuwa akizuia uhusiano wa karibu wa kijeshi na Marekani kwa kupendelea Uchina na nchi nyingine za kijamaa.”

Kwa upande wake, Profesa Kapuya ananukuliwa akieleza Balozi Retzer, jinsi Rais Kikwete alivyoweka msimamo wake katika suala hilo, tangu 3 Machi 2006 wakati wa ziara ya Naibu Kamanda wa Marekani katika Muungano wa Ulaya, Jenerali William Ward.

“Kikwete alisisitiza nia yake ya dhati ya kuunga mkono shughuli za mafunzo hayo…mbele ya wakuu wake wa jeshi. Lakini sasa kuna mkanganyiko kuhusiana na ucheleweshaji huu,” Kapuya ananukuliwa akisema.

Anasema, “Tunajaribu kuzuia mgongano na CDF (Mkuu wa Majeshi) na kuvuta muda wa kama miezi miwili hadi mitatu – ili tuzuie mgongano huo usiweze kutokea."

Kwa shabaha ya kueleweka vema, Kapuya anamwambia balozi, “…tunajaribu kueleza hali halisi ilivyo ili utuelewe. Tupo katika hali mbaya sana. Tunaomba msamaha kwa ucheleweshaji huo na tunakuomba utusaidie kutoa maelezo haya nchini kwako.”

“Kwa dhati tupo tayari kuunga mkono jitahada za mafunzo haya ya kulinda amani nchini, na hatupendi kuona ucheleweshaji huu unaharibu uhusiano wetu mzuri uliopo,” anaeleza Profesa Kapuya katika hali ya kubembeleza.

Mtandao unamnukuu Balozi Retzer akimhakikishia Profesa Kapuya kuwa wanaelewa madhumuni ya serikali ya kuunga mkono mafunzo hayo pamoja na changamoto zinazomkumba rais na waziri wake wa ulinzi.

Balozi Retzer alisema anautambua mkanganyiko huo ulioanzishwa na Jenerali Waitara, na hivyo akamshauri Profesa kuruhusu mafunzo hayo kuanza kabla ya makubaliano kufungwa.

Mpaka sasa, ubalozi wa Marekani nchini haujakana maelezo ya Balozi Retzer, jambo ambalo wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, linathibitisha kilichoandikwa na WikiLeaks.

“Hizi tuhuma dhidi ya Kikwete, bila shaka zina ukweli. Vinginevyo ubalozi wa Marekani ungekuwa tayari umetoa taarifa ya kujitetea kwa sababu anayelipua jipu hili bichi ni aliyekuwa balozi wake hapa nchini, na hii ni tuhuma kati ya nchi na nchi na siyo Balozi Rezter na Kikwete,” anaeleza kiongozi mmoja mwandamizi serikalini kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.

WikiLeaks inamnukuu balozi akisema, Profesa Kapuya, akikubaliana naye kuhusu kuanza mafunzo kabla ya makubaliano, alitikisa kichwa na kisha kusema, "Tunaelewa hayo. Kila mmoja wetu anaelewa haya, kwamba hatukuhitaji makubaliano ili tuendelee na ACOTA. Lakini ni salama kusema, tunaweza kuanza mafunzo haya ifikapo Agosti 2007." 

Akijibu maelezo hayo, Balozi Retzer alisema, “Rais Kikwete alitamka hadharani msimamo wake huu wa kuunga mkono mafunzo haya ya ACOTA. Lakini hivi sasa, anaangushwa na wakuu wa jeshi.

“Najua Rais Kikwete amepiga hesabu zake za haraka ambazo hata sisi tunakubaliana nazo. Lakini wasiwasi wangu, ni jinsi anavyoshindwa kusimamia ahadi zake,” mtandao unamnukuu balozi akisema.

Mchakato huu ulianza wakati Dk. Asha-Rose Migiro akiwa waziri wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa. Balozi pia alirejea kukumbusha ahadi ya Kikwete wakati alipokutana na waziri wa mambo ya nje wa sasa, Bernard Membe.

Katika hatua nyingine, WikiLeaks linasema, mara baada ya Rais Kikwete kuingia madarakani, alimuomba Balozi Rezter kumsaidai kupeleka wasaidizi wake wawili wa karibu kupata mafunzo nchini Marekani.

Katika ombi hilo, Kikwete aliwataja wasaidizi wake hao wawili kuwa ni January Makamba, ambaye sasa ni mbunge wa Bumbuli na David Jairo ambaye ni katibu mkuu Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi.

Balozi Rezter alikubali na kumuahidi rais kuwa atafanya mawasiliano na serikali yake na hatimaye kuanza utaratibu ya mafunzo hayo kwa Januari na Jairo nchini humo.

Gazeti hili halikufanikiwa juzi kuthibitisha iwapo Makamba na Jairo walipata mafunzo hayo nchini Marekani.

Aidha, taarifa ya ikulu wiki iliyopita, ilisema Rais Kikwete alikataa ujenzi wa hoteli katika mbuga za wanyama za Ngorongoro, ikiwa na maana ya kuonyesha kutokuwepo uhusiano kati yake na Ali Albawardy.

Lakini taarifa haikusema lolote juu ya hoteli katika mbuga za Serengeti ambayo ilifunguliwa rasmi na Rais Kikwete. Hoteli hiyo inaitwa Bilila Lodge Kempinski. Ilifunguliwa tarehe 10 Julai 2009.

Katika hutuba yake ya ufunguzi, Kikwete alisema, “Najisikia kupewa heshima kubwa na upendeleo katika kushuhudia tendo hili la kihistoria la ufunguzi wa Bilila Lodge ambayo ni mojawapo ya hoteli za Kempinski.

“Nakushukuru Bw. Reto Witter, rais na mtendaji mkuu wa hoteli za Kempinski, Bw. Ali Albawardy, mwenyekiti wa ASB Tanzania Limited na Bw. Hasu Masrani mkurugenzi wa  ASB Tanzania Limited kwa mwaliko huu.

“Nina mapenzi ya dhati kwa Serengeti, lakini Bilila Lodge imekamilisha uhondo na starehe pamoja na uzuri wa Serengeti. Nakushukuru sana Bw. Ali Albawardy kwa uamuzi wako wa kujenga hoteli hii ya kifahari hapa Serengeti na katika ardhi ya Tanzania,” alieleza Rais Kikwete.

0
Your rating: None Average: 3.5 (8 votes)
Soma zaidi kuhusu: