Rais kadandia meli iliyong’oa nanga


John Aloyce's picture

Na John Aloyce - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version

KWA Rais Jakaya Kikwete kujitumbukiza katika mjadala wa katiba mpya wakati tayari umepamba moto, amekuwa kama anayejaribu kudandia meli iliyokwishaondoka kwa kuifuata nyuma.

Alisema katika hotuba yake ya kukaribisha mwaka mpya wa 2011, kuwa ataunda tume ya kupitia katiba upya inayolingana na umri wa taifa wa nusu karne.

Rais wa chama kikongwe kinachotawala alipaswa kuliona hili la katiba na kulitolea uamuzi mapema sana hata kama halikuwa katika ilani ya uchaguzi ya chama chake.

Wakati Kikwete na chama chake wakiingiza mahakama za kidini katika ilani yao, baadhi ya vyama vya upinzani makini, viliamua kuweka mkazo katika suala la kuandikwa kwa katiba mpya katika ilani zao.

Kimsingi Rais Kikwete amekinyima chama chake heshima ya kuwa kiongozi katika harakati za kuongoza hatua hii muhimu kwa uhai wa taifa.

Hatua yake ya kuingia kwa kuchelewa katika mchakato huu, kwa hali yoyote, inaashiria kuridhia suala hili kwa shingo upande.

Ukifikiri kwa kina juu ya hatua ya Rais Kikwete aliyoichukua kwa kuchelewa, mambo mawili ya haraka yanajitokeza.

Kwanza, katiba mpya siyo msimamo wa serikali yake wala ya chama chake. Wasaidizi wake katika suala hili, yaani Mwanasheria Mkuu wa serikali na Waziri mwenye dhamana, walikwishatoa maoni yao (na pengine ya serikali), wakipinga haja ya kuwa na katiba mpya.

Haiwezekani kuwa walikurupuka kutoa matamshi yanayogusa suala nyeti kama hili. Walikuwa na ruhusa au walisoma dalili za mkuu wao wa kazi na ndipo wakasema walichosema.

Mpaka hapa ni sahihi kusema serikali ya Kikwete na chama chake hawataki katiba mpya, na kama wanaitaka ingekuwa busara kuwawajibisha wasaidizi wake walioropoka.

Pili, kwa kuwa Kikwete, CCM na serikali wanaingia katika suala hili kwa kuchelewa na bila utashi ulio wazi, ni vigumu kuamini kuwa watatoa uhuru unaotakiwa kwa hiyo tume inayodaiwa kuundwa ili kuratibu suala hili nyeti.

Unapokuwa na rais ambaye hata katika hotuba yake neno “katiba mpya” alilitamka kwa taabu na si ajabu halikuwamo hata katika hotuba yenyewe, ni vigumu kuamini kuwa rais huyuhuyu atateua tume na kuipa uhuru unaotakiwa ili ifanye kazi yake sawasawa.

Unapokuwa na mwanasheria mkuu wa serikali, ambaye siyo tu ameisharopoka na kuweka msimamo kuwa katiba mpya haitakiwi, ni vigumu kuamini kuwa atamshauri vema rais katika uundaji wa tume hiyo na kuipa hadidu za rejea zinazoipa uhuru kamili.

Unapokuwa na waziri wa sheria ambaye ameishajichafua kwa kuonyesha kuwa hataki katiba mpya, ni vigumu kusaidia serikali ili ijilinde na majaribu ya kuingilia mchakato wa kuandika katiba hiyo.

Unapokuwa na chama tawala ambacho daima hakikubali kushindwa na kiko tayari kumwaga damu, kununua watu, na kutumia watendaji wa serikali kupotosha ukweli, ni vigumu kutumaini kuwa kitakuwa tayari kukaa pembeni na kuzuia makada wake wasivuruge mchakato wa kuandika katiba mpya.

Kwa mtiririko huu, kuna shaka hadi bungeni ambako chama tawala kina wabunge wengi. Tumeshuhudia miswada ya sheria ikijadiliwa na kupotoshwa au kughushiwa wakati inapelekwa kwa rais ili isainiwe.

Taifa limeshuhudia hoja binafsi za maslahi ya nchi zikiwekewa mizengwe ili zisiingie bungeni na kujadiliwa.
 
Tumeshuhudia Bunge likiingia katika makubaliano batili na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) ili kuzuia bosi wa taasisi hiyo asiwajibishwe huku na yeye akisitisha kuwashughulikia wabunge waliopokea posho zaidi ya moja katika majukumu ya kibunge.

Tumeshuhudia tume ya uchaguzi ikiweweseka na kufuata kila amri ya serikali kutangaza au kutotangaza hata matokeo ya uchaguzi au kuunda majimbo mapya.

Tumeshuhudia jitihada za serikali za kuua upinzani bungeni na kuzima mijadala yenye manufaa kwa taifa.

Tumeshuhudia vitisho kwa vyombo vya habari na hata baadhi ya magazeti kufungiwa  pale yalipodiriki kutumia “uhuru” wake katika kuandika habari zenye maslahi kwa taifa.

Kwa mwenye akili na kumbukumbu kama hizi ni vigumu kuamini kuwa inawezekana kuwa na tume huru katika taifa hili linalotawaliwa kwa nguvu ya fedha.

Ili kuandika katiba mpya, Rais Kikwete amesema ataunda tume huru (commission) ya kupitia na kukusanya maoni kutoka katika maeneo mbalimbali. Uzoefu tulio nao katika taifa unatufanya wengi tutilie shaka uamuzi huu au njia hii inayotarajiwa kutumika.

Hatujawahi kuwa na tume huru na wala kuwa na ripoti ya tume iliyotekelezwa kama ilivyotolewa. Kwa hiyo swali kuu ni: Je, uhuru wa tume unapatikanaje?

Je, ni kwa mteuaji kutamka kuwa tume aliyoiunda ni huru au ni kwa wateule kuamini kuwa wako huru katika utendaji wao wa kazi?

Je, ni nani anaweza kuteua na kuwafanya wadau wengi wakaamini kuwa tume hiyo ni huru?

Katika mazingira ambamo kulipana fadhila ni jambo la kawaida; anayeteua au kuteuliwa hawawezi kuwa kigezo kizuri cha kutuhakikishia uhuru. Hii ndiyo maana tayari wazo la rais la kuunda tume limekataliwa na wengi.

Moja ya mambo yanayopigiwa kelele katika katiba ya sasa ni mlundikano wa madaraka katika mhimili mmoja na kwa hiyo ni vigumu kwa akili ya kawaida kuamini kuwa mhimili huo utaongoza vema mchakato wa kupunguza madaraka yake.

Aidha, kero nyingine inayopigiwa kelele ni kukosekana kwa uhuru wa kutosha kwa vyombo vinavyopaswa kuwa huru kama vile Mahakama, Bunge, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),  TAKUKURU, Tume ya Maadili, na vyombo vingine vya dola.

Rais Kikwete kama amebakiza hata chembe moja ya ukweli, akubali kuwa vyombo hivyo vinapungukiwa sana uadilifu unaotokana na kuminywa uhuru wake.

Kama vyombo hivi viko huru je, vinaweza kumkamata mkewe au mtoto wa rais pale anapokiuka sheria?

Ushahidi wa hili ni taarifa zilizomnukuu Edward Hoseah, mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU anayelalamikia bosi wake – Rais Kikwete – kukingia kifua watuhumiwa wakuu wa rushwa nchini.

Malalamiko ya Hoseah ndiyo malalamiko yaliyopo kwa wakuu wengi wa vyombo vya dola. Wengi wanasema hawana uhuru wa kupambana na uhalifu wala ufisadi katika taifa.

Mahakama zinaingiliwa kwa njia, ama ya moja kwa moja au kisaikolojia kwa kunyimwa vitendea kazi. Matokeo yake ni kulundikana kwa kesi na kuchelewesha haki.

Je, ikiwa vyombo hivi vilivyopo havina uhuru, uhuru wa tume ambayo rais anakusudia kuunda, ingawa wananchi wengi tayari wameitilia shaka na kuikataa, utatoka wapi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: