Rais Kikwete aanze kujisafisha kwanza


editor's picture

Na editor - Imechapwa 09 February 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amewaambia wanachama wake kwamba anakusudia kukifanyia marekebisho makubwa chama hicho ili kiendane na wakati.


Ahadi hiyo aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya miaka 34 ya CCM mjini Dodoma itahusu muundo na namna ya kupata viongozi.


Baadhi ya viongozi watakaong’olewa hasa waliochoka, wasaliti na walioshindwa kukisaidia katika uchaguzi mkuu uliopita hadi kikakosa ushindi wa kishindo.


Kauli hiyo ya Rais Kikwete inakusudia kuonyesha kuwa matatizo makubwa ya chama hicho yanasababishwa na baadhi ya viongozi ama ngazi ya juu, mikoa, wilaya au matawi.


Ni jambo zuri kwa mwenyekiti kutazama upya safu yake, lakini sisi tuna ushauri wa ziada kwake. Rais Kikwete aanze kujitazama yeye kabla ya kuwarukia viongozi wengine.


Kwanza Rais Kikwete ndiye aliasisi mtandao uliofanya kazi kubwa ya kuchafua sifa za wapinzani ndani ya chama na mwaka jana ulichafua wapinzani nje ya chama. Watu wanamchukia kwa hilo.


Pili katika uongozi wake, wananchi wameshuhudia chama kikigawanyika katika makundi mawili. Moja ni la wapambanaji wa ufisadi na jingine ni linalolindwa na chama kwa vile ni la matajiri watuhumiwa wa ufisadi.


Rais Kikwete mara zote amehaha kukumbatia makundi yote mawili. Kama Rais Kikwete ameshindwa kujitenga na watuhumiwa ufisadi katika chama, hawezi kukifanyia marekebisho chama.


Mifano ipo. Alishashindwa kuwashughulikia viongozi wa juu waliotia saini mradi wa upanuzi jengo la UVCCM. Badala yake aliwashughulikia waliofichua ufisadi huo.


Alishindwa kuwaadhibu wanachama waliokumbwa na kashfa kadhaa zikiwemo za kujipatia fedha kwa njia za rushwa. Badala yake alipita kuwasafisha majimboni wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana.


Udhaifu alioonyesha ndani ya chama ndio umeonekana serikalini. Viongozi waliotuhumia kuingiza kampuni feki ya Richmond/ Dowans hawakuchukuliwa hatua na rais.


Vyombo vya habari vya kimataifa vilimkariri msaidizi wake mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa akilalamika kuwa Rais Kikwete anamzuia kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wenye majina makubwa.


Mambo hayo yamemong’onyoa heshima ya serikali na chama chake. Kwa kuwa serikali imara inategemea chama imara, kwa vyovyote chama kilichogubikwa na rushwa hakiwezi kutoa viongozi bora wa serikali.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: