Rais Kikwete ajinasue Dowans


editor's picture

Na editor - Imechapwa 05 January 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SERIKALI ya Rais Jakaya Kikwete imejipambanua sasa kuwa ina ubia au inafadhili miradi ya kifisadi, ukiwemo huu wa kutaka kuichotea kampuni feki ya Dowans Sh. 185 milioni ambazo ni kodi ya wananchi.

Ushahidi ni huu. Serikali hii ndiyo iliingia mkataba wa kifisadi wa kufua umeme wa dharura na kampuni ya Richmond Development Company (LLC) mwaka 2006.

Tangu mwaka huo, wananchi wamekuwa wakipinga mkataba huo ambao ulikuwa unalilazimisha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuilipa kampuni hiyo kiasi cha Sh. 152 milioni kila siku kwa madai ni gharama za uendeshaji.

Serikali ya Rais Kikwete ilipoona kuwa imeng’ang’aniwa katika hilo, ikaratibu njama nyingine mkataba huo wa Richmond, kampuni iliyokuja kujulikana kuwa feki, uhamishiwe katika kampuni nyingine feki ya Dowans.

Serikali ikavunja mkataba, lakini katika mazingira ya kutatanisha, ikajiruhusu kushindwa katika kesi ambayo Dowans ilifungua katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) na sasa inataka ilipwe fidia ya Sh. 185 bilioni.

Kitu cha kushangaza ni kwamba, pamoja na kesi hiyo kuendeshwa Dar es Salaam, serikali ilishindwa kutuma mawakili wake kujitetea, lakini iko mstari wa mbele kutaka kampuni hiyo feki iliyorithi mkataba feki kutoka Richmond ilipwe mabilioni hayo ya shilingi bila hata kesi kusajiliwa Mahakama Kuu ya Tanzania, kama sheria inavyotaka.

Ushahidi mwingine unaotufanya tuamini kuwa serikali ina ubia wa kifisadi ni hatua ya Rais Kikwete kukwepa kuzungumzia msimamo wa serikali.

Hata katika salamu zake za Mwaka Mpya, Rais Kikwete alifanya ushawishi wananchi wakubali maumivu ya bei mpya ya umeme lakini hakugusia malipo.

Hapa anaonyesha haguswi na umaskini wa Watanzania, kwani wakati Rais anakwepa suala hilo, tayari Dowans imewasilisha ankara hazina ikisubiri taratibu za kuchotewa mamilioni ya shilingi.

Tunamwomba Rais Kikwete ajinasue, ajiondoe kwenye sakata hili, asijipake matope; atumie mabilioni ya fedha za kodi ya Watanzania katika shughuli za maendeleo; kuboresha elimu na afya na siyo kuwachotea mafisadi kwa kisingizio chochote. Wananchi hatutamwelewa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: