Rais Kikwete amefanya mengi


Emmanuel Shilatu's picture

Na Emmanuel Shilatu - Imechapwa 08 September 2009

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

NAUNGANA na Salva Rweyemamu, John Kibaso na Dunia Ibrahimu, kupinga kauli ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kazi.

Ni Jambo la kushangaza tena linalotia simanzi kuona kiongozi mkubwa kama Profesa Lipumba anasema Kikwete ameshindwa kazi.

Mwenye macho haambiwi tazama wala wenye masikio haambiwi sikia.

Kikwete amefanikiwa kupambana vilivyo na maadui watatu, ujinga, maradhi na umasikini. Katika hali ya kuhakikisha kuwa kila mtoto anapatiwa elimu ya msingi na ya sekondari, serikali ya Awamu ya Nne imefanikiwa kuongeza idadi ya shule katika kila kata ili kurahisisha upatikanaji wa elimu.

Mwaka 2005 kulikuwa na jumla ya shule 1210 ambapo mpaka kufikia 2008 zilionmgezeka na kuwa na jumla ya shule 3372. Haya ni mafanikio makubwa.

Wapo wanazikebehi shule hizi kwa kusema, hazina sifa za kuitwa shule kutokana na kukosa vitendea kazi vikiwamo vitabu na walimu wa kufundisha.

Lakini lazima kuwe na mipangilio katika maisha. Haiwezekani kuanza kuvaa kiatu halafu soksi ikafuata. Mtu mwenye akili timamu ataanza na soksi na kisha viatu hufuata. Hivyo ndivyo serikali ya Kikwete ilivyoamua kufanya kazi zake.

Imeanza na majengo. Imemaliza na sasa inahakikisha upatikanaji wa waalimu, vitabu na maabara. Mfano halisia ni ufunguzi wa maabara ya kisasa katika chuo cha MUHAS.

Serikali ijenga chuo kikuu kipya mkoani Dodoma katika hali ya kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya ngazi ya chuo kikuu. Tayari wanafunzi 8,000 wamesajiliwa, lengo likiwa kufikisha wanafunzi 40,000.

Licha ya taifa letu kuwa na uhaba wa fedha, serikali imeendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa asilimia 100.

Wapo wanaonufaika moja kwa moja na mkopo huo kama vile wanaosomea masomo ya sayansi, ualimu na sayansi ya jamii. Ingawaje kuna madaraja 10 kuanzia asilimia 10 hadi 100 yaliyowekwa kwa ajili ya kila mwanafunzi kupata mkopo.

Madaraja haya ya mikopo huwanufaisha hata wale wanaosomea uhasibu, uanasheria, ustawishaji wa jamii na teknolojia ya mawasiliano.

Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) haipo nyuma katika mapambano dhidi ya maradhi. Kwenye mkakati wa kupambana na malaria, serikali imehakikishia wananchi upatikanaji wa madawa sahihi na ya kutosha na imetoa vyandarua bure kwa mama na mtoto.

Katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi, serikali imetenga zaidi ya Sh. 600 bilioni kwa kila mwaka kwa ajili ya mapambano ya ugonjwa huo.

Fedha hizo hutumika kwa ajili ya kununulia madawa mbalimbali ya ukimwi na magonjwa nyemelezi ARV’s. Fedha hizo hutumika pia kwa ajili ya kuendeshea kampeni ya upimaji kwa hiari, uendeshaji wa makongomano warsha na semina mbalimbali za kutoa elimu juu ya ukimwi.

Kumekuwa na maboresho ya Afya ya mama na mtoto, upunguzaji wa vifo vya uzazi kwa utoaji wa elimu ya uzazi, kuongeza idadi ya wakunga na utoaji wa huduma ya kujifungua. Haya yamefanyika kwa kiwango cha hali ya juu na takwimu zipo.

Serikali imekabiliana hata na magonjwa ya mafua ya ndege, kipindupindu na homa ya bonde la ufa.

Kwenye eneo la tatu la umasikini, kikwete amefanya makubwa kwenye kukabiliana na umasikini. Ameboresha miundo mbinu ikiwamo njia zote za uchukuzi kama reli, bandari, njia za mabomba, tovuti na simu.

Kwenye suala zima la barabara, wizara ya miundombinu inatembelea kifua mbele kwa kufanikisha kuunganisha nchi kupitia barabara.

Kutokana na hali ya mtikisiko wa uchumi duniani, naungana na John Kibaso katika kumuunga mkono rais Kikwete, kwamba amechukua hatua kama ile iliyochukuliwa na rais Obama. Kikwete alitoa Sh. 1.7 trilioni katika kukabiliana na mtikisiko wa kiuchumi.

Kuhusu demokrasia, Kikwete amepiga hatua kwa kuruhusu kwa wazi mijadala mbalimbali. Vyombo vya habari na wananchi wamekuwa huru kuibua hoja mbalimbali zikiwamo hata zile zinazodhalilisha serikali. Haya si mafanikio madogo.

Si hivyo tu, Kikwete amefanikiwa kutimiza ahadi yake kwa wanawake na taifa. Ni pake alipotoa fursa kubwa ya uongozi kwa wanawake.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: