Rais Kikwete amesahau ahadi zake nyingi


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 17 June 2008

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

SASA imedhihirika wazi kwamba serikali ya Rais Jakaya Kikwete haina ubavu wa kutenda yale ambayo rais aliahidi kabla ya kuingia madarakani.

Kabla na baada ya kuingia madarakani, Rais Kikwete aliahidi wananchi na jumuiya ya kimataifa kuwa serikali yake itaboresha mashirika ya umma yaliyosalia. Aliahidi kuyapa mtaji mashirika hayo na kuweka usimamizi bora na wenye tija.

Aliahidi kupambana na rushwa na umangimeza ndani ya serikali yake. Alisema pia kwamba serikali yake haitabinafsisha kwa kasi mashirika yaliyosalia.

Si hivyo tu, bali rais Kikwete aliahidi kurudisha nyumba za serikali zilizouzwa kinyume cha taratibu na kwa "bei ya kutupwa" na watawala waliopita. Alisema atafanya hayo kwa Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu mpya.

Kimsingi hadi sasa, ikiwa ni zaidi ya miaka miwili na nusu tangu Kikwete atoe ahadi hiyo, serikali yake haijaonyesha kama inaweza kusimamia yale yaliyoahidiwa.

Badala yake Kikwete na serikali yake wameendelea kukumbatia viongozi wa mashirika ya umma walioyageuza mashirika hayo mali yao binafsi.

Serikali ya Kikwete kama ilivyokuwa ya mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, imeendelea kukodisha mashirika ya umma yaliyosalia kwa wawekezaji matapeli na wasio na uwezo.

Kimsingi kama ilivyokuwa kwa utawala uliopita, utawala wa sasa umeendelea kutokuwa makini katika kutenda kazi zake. Pamoja na serikali kushindwa kurudisha nyumba za umma, imeshindwa hata kuchukua hatua dhidi ya wafanyakazi wake walioshiriki katika uuzaji wa nyumba hizo.

Lakini wakati wananchi wakisubiri kurudishwa kwa nyumba hizo, Kikwete mwenyewe ameanza kujenga upya nyumba aliyoinunua serikalini iliyoko Mtaa maungano ya mitaa ya Ursino/Migombani, jijini Dar es Salaam.

Hii ina maana kwamba, Kikwete amesahau alichoahidi, au hakukiamini, au yalikuwa "maneno ya kisiasa." Na hivyo ndivyo ilivyo katika mashirika mengine likiwamo Shirika la Bima la Taifa (NIC) na Shirika la Ndege Tanzania (ATC).

Mengine ni Shirika la Posta (TPC), Shirika la Ugavi wa Umeme la Taifa (Tanesco), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Shirika la Biashara ya Nje (BET) na Benki ya National Microfinance (NMB).

Shirika la ndege la ATC: Ukiondoa videge viwili vilivyoletwa na serikali kwa ajili ya kile kinachoitwa, "kuimarisha ATC," hakuna lolote la maana ambalo serikali inaweza kujivunia katika shirika hilo.

Wakati mashirika mengine ya ndege, kama vile Kenya Airways, linazidi kujiimarisha, kuingia ubia na makampuni mengine na kufanya kazi zake nje ya bara la Afrika, ATC limeishia kushindwa kusafirisha hata abiria ambao limeahidi kuwasafirisha.

Kwa mfano, mwishoni mwa mwaka jana, ATC liliingiza taifa katika aibu ya karne baada ya kuwasotesha mahujaji kwa zaidi ya siku kumi na hatimaye kushindwa kuwasafirisha kwenda Hijja huko Jidah Saudi Arabia.

Ilibidi serikali iingilie kati kuwaokoa mahujaji hao. Hata hivyo, hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa ATC aliyewajibishwa kutokana na sakata hilo.

Na hili baadhi ya watu wanalihusisha na uswahiba wa Kikwete na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, David Mattaka.

Utendaji wa Mattaka huko nyuma unafahamika. Awali alikuwa mkurugenzi mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF). Aling'olewa na Benjamin Mkapa kwa kile kinachotafsriwa na wengi kama "kushindwa kutekeleza majukumu."

Kilichomfanya Kikwete kumteua tena Mattaka kuongoza shirika lililomahututi, halifahamiki isipokuwa kwa Kikwete mwenyewe na Mattaka.

TANESCO: Hili ni miongoni mwa mashirika nyeti na muhimu kwa uchumi wa taifa, ustawi na usalama wa wananchi. Lakini badala ya serikali kuliimarisha, inazidi kulitokomeza. Ni utawala wa Kikwete ambao umechonga jeneza kwa Tanesco, baada ya serikali ya Mkapa kuchimba kaburi.

Hakika Kikwete ameikuta Tanesco ikiwa hoi; ikielemewa na mizigo ya mikataba mibovu iliyofungwa katika tawala zilizopita, kama vile, IPTL, Songas, Kiwira na Net Group Solution.

Lakini la kushangaza ni kwamba ni serikali ya Kikwete ambayo imeipeleka Tanesco tena katika mikataba ya kufua umeme wa dharula ya Richmond, Alstom na Aggreko ambayo nayo ni ya kinyonyaji.

Shirika la Bima la Taifa (NIC): Hili ni shirika ambalo kwa sasa liko katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). NIC limetoka kuwa shirika kubwa lililokuwa na mtaji, wateja, vitegauchumi na mtandao nchi mzima, limeishia kuwa hohehahe.

Kila mwenye nia njema kwa shirika hilo na taifaa na ambaye hana ubia na menejementi na NIC, anakubali kwamba viongozi wa sasa wa NIC wameshindwa kuliongoza shirika hilo na wanadaiwa kushiriki katika vitendo vya kuangamiza hata kidogo kilichobakia.

Miongoni mwa hujuma za wazi ni hatua ya viongozi kushindwa kuwalipa wateja madai yao. Baadhi yao wamo hata wateja wa bima za maisha na bima za kawaida.

Haya yanafanyika huku shirika likiwa linakusanya ada za bima kutoka kwa wateja wake. Mbali na hilo, viongozi wa NIC wanakusanya mapato makubwa yanayotokana na vitegauchumi vyake viliyotapakaa karibu nchi mzima.

Haya yanafanyika kwa wazi kabisa. Lakini serikali inajifanya kiziwi na bubu. Hisia za wananchi ni kwamba, "Kikwete ameshindwa kuchukua hatua ya kushughulikia mabuku" yanayolitafuna shirika hili kutokana na baadhi ya wakurugenzi kudai kuwa na uswahiba na rais. Hayo rais atakuwa ameyasikia.

Na kuthibitisha kwamba serikali haina dhamira ya kurekebisha hali hiyo, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo, ameliambia Bunge la Muungano kwamba "mchakato wa kurekebisha na kubinafsisha Shirika la Bima la Taifa unaendelea kwa utaratibu wa kutenganisha majengo na biashara ya bima, badala ya utaratibu wa mwanzo uliokuwa unachanganya biashara ya bima na majengo ya shirika."

Hii maana yake ni kwamba, serikali itaendelea kuuza mashirika yake, lakini pia, menejementi ya sasa itaendelea kulindwa hadi kuhakikisha NIC inabaki magofu.

Kufikia hapo, kila mmoja atakuwa ameshavuna alichotaka. Shirika litauzwa kwa bei ya kutupwa, na kwa walewale walioshindwa kuliendesha. Mwisho, shirika litarudi serikalini kama ilivyokuwa kwa ATC na kuliwekea mtaji mpya, kabla ya kuliuza tena.

Haitashangaza kusikia kuwa shirika limekodishwa kwa mwekezaji asiye na uwezo wa kulipa madeni ya wateja, au kuliimarisha. Na hili limeshafanyika katika Shirika la Reli la Taifa (TRC). Aliyeitwa mwekezaji kumbe alikuwa hana uwezo hadi ikafikia asaidiwe na serikali kulipa mishahara kwa miezi mitano ya mwanzo.

Badala ya kuimarisha shirika, mwekezaji amekuwa anavichukua vipuri vya injini za reli na kuvipeleka kwao India; kisha anachukua vile vya India, ambavyo vimechoka zaidi na kuvileta nchini.

Wakati menejementi ya NIC ikiendelea kulalama kwamba haina fedha na kuitaka serikali kutoa fedha kwa ajili ya kuendesha shirika, ikiwamo kulipa wateja wake, hakuna mtu mwenye ubavu wa kuiuliza menejementi hiyo, fedha zilizokuwapo huko nyuma zimekwenda wapi?

Nani aliyezikwapua? Je, biashara ya Bima imedorora? Kama imedolola, kwa nini makampuni mengine ya nje yaliyongia nchini majuzi yanazidi kushamiri siku hadi siku?

Au vitega uchumi vya shirika hili vimekwenda wapi? Nani anayelinda utawala wao na kuwapa kiburi kiasi hicho mpaka inadaiwa sasa kwamba wanatembea kifua mbele huku wakijitapa kwamba wameiweka serikali mfukoni?

Na kama madai haya si ya kweli, nani anayehoji uongozi wa NIC kwamba linawezaje kuendesha kesi kwa zaidi ya miaka kumi, huku likiendelea kuwalipa mishahara wafanyakazi wasio na tija ndani ya shirika? Hasara yote hii analipa nani, kwa faida ipi na ya nani?

Miongoni mwa minong'ono mitaani ni kwamba menejementi ya NIC ilichangia kampeni zaRais Kikwete wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais ndani ya chama chake na kwamba leo hii inalindwa kwa sababu hiyo. Rais anaamini hayo?

Yote haya yawe kweli au si kweli, kwa nini serikali inaendelea kuwabebesha mizigo wananchi wake kwa kuwapa shirika watu wasio na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma?

Taarifa za ndani ya shirika zinazothibitishwa na ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu wa Ndani, zinasema kwamba menejementi hiyo inatumia mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwalipa mawakili kuandaa "kesi hewa."

Benki ya NMB: Hii ni benki ambayo ilikuwa inaipa gawio serikali kila mwaka. Taarifa zinasema katika mwaka wa fedha wa 2007/2008, serikali ilipata gawio la zaidi ya Sh. 8.8 bilioni kutokana na faida ya biashara iliyofanywa na NMB.

Serikali ina asilimia 25 ya hisa ndani ya benki hiyo. Lakini badala ya serikali kuiimarisha benki yake, inaishia kuipiga bei. Inasema inakusudia kuuza asilimia 21 ya hisa zake.

Kwa mujibu wa Mkullo, zoezi hilo litakamilika mwishoni mwa mwaka huu, ambapo serikali inatarajia kupata Sh. 58 bilioni baada ya kuondoa gharama zinazokadiriwa kufikia Sh. 5 bilioni.

Hata hivyo, serikali haijasema wazi kwamba hicho kinachoitwa "gharama za Sh. 5 bilioni" ni kitu gani hasa. Na wala haijajulikana iwapo wabunge wataweza kumhoji waziri Mkullo wakati huu wa bajeti juu ya matumizi ya feha hizo.

Hizi ni fedha nyingi zinazotosha kupunguza makali ya maisha kwa wananchi na ambazo zinaweza kupunguza ukamuaji wananchi kwa njia ya michango holela ya ujenzi wa shule, zahanati na vituo vya afya.

Hata kama fedha hizo haziwezi kumaliza tatizo moja kwa moja, lakini "kidogo chako kitunze, kuliko kingi cha mgeni." Kiasi hicho si haba; angalau kinatosha kujenga matundu ya vyoo katika baadhi ya shule na hivyo kupunguza safari za kuwapigia magoti wafadhili.

Biashara ya Nje-BET: Hapa nako hapako salama. Mkurugenzi mtendaji wake anatuhumiwa na baadhi ya wafanyakazi kununua magari yaliyochokaa.

Tume imeundwa, lakini kabla haijamaliza kazi inadaiwa kwamba "wakubwa wameingilia kati." Kuingilia kati kwa wakubwa, kunaelezwa kwamba kunatokana na kile kinachodaiwa kuwa ni "kulinda ndugu."

Mkurugenzi wa BET, ni Ramadhani Khalfani, mbunge wa zamani wa Bagamoyo. Wakati serikali ilitangaza nafasi hiyo kwenye magazeti, inadaiwa Khalfani alitangazwa kushika wadhifa huo. Malalamiko yanaendelea.

Shirika la Posta (TPC). Hili limepewa mtaji na serikali baada ya kubeba deni la mabilioni ya shilingi liliyokuwa linadaiwa. Hakuna ajuaye kilichosababisha shirika kushindwa kulipa deni hilo isipokuwa waliokuwa wakiliendesha na labda watawala.

Lakini kilichowazi ni kwamba wapo baadhi ya wafanyakazi ambao wanalihujumu shirika hilo. Wengine wameshirikiana na watendaji ndani ya serikali na katika chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Inasemekana serikali inawajua kwa majina wakwapuaji hao. Lakini badala ya kushughulikia suala hilo, inaamua kunyamaza na kuruhusu utafunaji kuendelea.

Sasa tuulize kwa pamoja. Rais Kikwete anayaona haya? Je, ahadi zake za kusafisha uchafu huu zimefutika, zimezeeka au amezisahau? Je, hili laweza kuwa angalizo?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: