Rais Kikwete anazungumzia Tanzania ipi?


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 05 October 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

RAIS wetu, Jakaya Kikwete alituhutubia Watanzania na kutueleza mengi juu ya ya mafanikio aliyoyapata hivi karibuni katika safari yake ya ughaibuni huko Marekani. Huko pia alipata fursa ya kulihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN).

Katika hotuba yake, Rais wetu alitueleza juu ya umoja wa Watanzania wenzetu waishio Marekani uitwao Diaspora Community of Tanzania in America (DICOTA), ambao alikutana nao 23 Septemba 2011 wakati wa mkutano wao mkuu wa mwaka.

Rais Kikwete alisema katika hotuba yake kwamba alipata bahati ya kuwahutubia Watanzania wenzetu wale waishio Marekani, kwa maana ya wanachama wa DICOTA, ambapo aliwakumbusha mambo matano muhimu.

Kwanza alisema, pamoja na kuwapongeza kwa mafanikio yao katika kipindi kifupi, aliwaomba wawe raia wema katika nchi ya watu na kwamba aliwasihi sana wajiepushe na vitendo vya kihalifu kama vile wizi, ujambazi, kutumia au kufanya biashara ya dawa za kulevya, ubakaji na kadhalika.

Alisema katika hotuba yake kuwa aliwatahadharisha kuwa wakijihusisha na vitendo vya kihalifu wasitarajie serikali yetu tukufu “kuwatetea kwa sababu hata sisi huku nyumbani watu wanaofanya makosa hayo wanakamatwa, kushtakiwa na kufungwa.

Jambo la pili ambalo Rais wetu aliwaasa wenzetu waishio ughaibuni huko Amerika ya Rais Barack Obama ni kwamba wasisahau nyumbani kwao; wakumbuke kujenga nyumba nzuri makwao ili wawe na mahali pazuri pa kufikia na hivyo watakuwa wamechangia kuwaendeleza wazazi wao.

Jinsi Rais wetu alivyo muungwana, alisema katika hotuba yake kuwa aliwaeleza anavyolitambua tatizo la wao kupata viwanja na kupata watu waaminifu wa kuwasimamia ujenzi na kwamba anafahamu watu waliodhulumiwa na watu waliowaamini kuwatafutia viwanja au kusimamia ujenzi.

Rais wetu pia alieleza jinsi alivyowaahidi waungwana wale kuwa “nimeagiza Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa washirikiane kuwasaidia kupata viwanja kwa urahisi na uhakika.

Kwa kifupi, mengine aliyozungumzia rais katika hotuba yake kuhusu Watanzania hao waishio Marekani ni pamoja na kuwaomba kuwekeza nyumbani kwao Tanzania na kuchangia maendeleo kwa  kuweka fedha zao katika benki za nyumbani Tanzania.

Kwa bahati nzuri, hotuba ile ya Rais wetu ilitangazwa na runinga zetu usiku wakati watoto na wajukuu wamelala kwa hiyo niliisikiliza na kuitazama kwa utulivu na umakini sana. Lakini kwa bahati mbaya sana pia, sikuielewa. Nilijitahidi sana kumwelewa Rais wetu lakini hakueleweka nadhani kwa wengi, si mimi pekee.

Mimi sikumwelewa Rais kwa sababu mpaka sasa sijaelewa alikuwa anaizungumzia Tanzania ipi! Tanzania hii tunayoishi ambayo Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi ni mama yetu, Prof Anna Tibaijuka? Au alikuwa anaizungumzia Tanzania nyingine ya kufikirika? Tanzania ipi ambayo mtu unaagiza tu unapata kiwanja?

Sintofahamu yangu ilidhihirika siku iliyofuata niliposoma magazetini kwamba eti mpango wa kuvunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam umeingia dosari. Eti kumbe kulikuwa na mpango wa kulivunja jiji na kuanzisha majiji mawili ya Kigamboni na Bunju huku katikati ya Jiji nako kukiwa Jiji!

Sasa mimi nikabaki nimeduwaa, Rais anawaita Wamerekani wenye asili ya Tanzania waje kuwekeza, kujenga nyumba zao na za baba zao, kuweka mapesa yao katika benki zetu na kusafirisha maiti zao (kama wakifa) kuja Tanzania kuzikwa wakati mambo hayaeleweki hapa nyumbani?

Mji mpya wa Kigamboni umekwama. Wenyeji na wakazi wa Kigamboni wanaishi kwa shaka. Nyumba zao hazinunuliki, haziuziki, hazifai kama dhamana. Hata zikifaa hazikubaliki kama dhamana na mabenki yetu na watu wenyewe wamekata tamaa. Hao Wamerekani weusi ndio watakubali viwanja vya Kigamboni kusikojengeka wala kuuzika.

Kwa miaka mitatu, wakazi wa Kigamboni hawaruhusiwi kujenga, kuuza, kutumia majengo yao kama dhamana wala kukarabnati nyumba zinazobomoka au kupata nyufa. Watu hao hawapewi viwanja wahame wala kujengewa nyumba wakaishi, isipokuwa , kwa mujibu wa Rais, viwanja kwa ajili ya Wamerekani vipo nchini!

Huko Bunju tumeambiwa hali ni mbaya sana ya kugombea viwanja na mashamba. Hata mtu mmoja kauawa na wengine kadhaa (mabaunsa wa dalali wa mahakama) kujeruhiwa wakigombea ardhi na viwanja. Hivyo viwanja vya Wamerekani Watanzania vitapatikana wapi? Huko huko Bunju? Wana mbavu za kupambana kugombea viwanja?

Waliobomolewa nyumba zao na mabomu Gongolamboto nao hawajajengewa nyumba kwa sababu eneo lililopatikana na kupimwa huko Kinyerezi jirani ya Tabata jijini Dar es Salaam lina mgogoro. Sasa Rais Kikwete atawezaje kuwapatia viwanja wageni hao kabla ya waliobomolewa nyumba na mabomu ya jeshi lake?

Miezi miwili iliyopita tulisikia kuwa maeneo yaliyopimwa Gezaulole yana mgogoro kwa sababu kila wapimaji wakiweka mawe, wenyeji wanayang’oa kwa sababu eti hawajalipwa fidia! Na pale walipolipwa fidia basi walipewa shilingi laki mbili kwa shamba la eka moja na kutozwa shilingi milioni saba kwa kiwanja kilichopimwa kwa anayetaka kubaki mjini!

Bado waliovunjiwa nyumba Kipawa kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere wamehamishiwa Pugu ambako wanapigwa mapanga na kufukuzwa kwa sababu, kumbe serikali ilikuwa haijalipa fidia kwa mashamba ya watu kule inakowahamishia wa Kipawa.

Kumbe sasa mtu wa kusaidiwa kupata kiwanja ni nani? Mmarekani mwenye asili ya Tanzania au mkazi wa Gongolamboto aliyebomolewa nyumba yake na mabomu? Mmarekani mweusi au mkazi wa Kipawa aliyebomolewa nyumba yake na serikali ili kupanua uwanja wa ndege? Nani asaidiwe kupata kiwanja na rais wake?

Na wakazi wa Jangwani je? Wao wahamie wapi kwa sababu kila siku tunasikia hawatakiwi kuishi pale kwa sababu hawastahili kukaa katikati ya jiji. Rais wao atawasaidia kupata viwanja, au yupo tayari kuwatafutia viwanja au wao nao wasafiri waende Marekani ndipo wafikiriwe viwanja?

Yaani kila nikifikiri sana naona kama Rais wetu mpendwa anaota vile. Hivi Rais Kikwete anapowaahidi watu viwanja ili waje kujenga na kuwekeza anakuwa na mawazo wakagawiwe viwanja wapi na nani? Wakagawiwe viwanja Kigamboni kunakopangwa kujengwa mji mpya wa kisasa?

Au rais wetu anataka wenzetu hao wakagawiwe viwanja Kigamboni nyingine ambayo kulikuwa na mpango wa kuanzisha jiji la pili pamoja na Bunju? Na je ziko Kigamboni ngapi na Rais wetu amepanga hao wenzetu wagawiwe viwanja Kigamboni ipi?

Niseme wazi kuwa rais wetu kaamua kuwadanganya wenzetu hao wa ughaibuni. Hakuna hata mmoja kati yao ambaye atakuja Tanzania katika siku moja, wiki au mwezi akapata kiwanja pale Wizara ya Ardhi ya akina Patrick Rutabanzibwa, hakuna.

Uzoefu na historia vimetuonyesha kuwa mtu ambaye katika majina yake matatu hakuna jina la Kikwete, Msuya, Mramba, Msekwa, Mkapa, Makamba, Mukama, Mgonja, Manji, Lowasa, Mwinyi, hapati kiwanja kuanzia Arusha, Moshi, Mbeya na hata Mwanza.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: