Rais Kikwete atibua nyongo


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 21 December 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki
NISHANI ZA UHURU

RAIS Jakaya Kikwete ametunuku nishani 57 kwa alioita, “Watu waliotoa mchango mbalimbali ya kutukuka katika nchi kwenye miaka 50 ya uhuru wake. Nishati hizo ni ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mwenge wa Uhuru daraja la kwanza na Mwenge wa uhuru daraja la pili.

Miongoni mwa waliotunukiwa nishani hizo, ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais mstaafu, Ali Hassani Mwinyi na mrithi wake kwenye nafasi hiyo, Benjamin Mkapa.

Wengine waliotunukiwa, ni Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, Idrissa Abdul Wakili na waliowahi kuwa makamu wa rais wa Jamhuri, Dk. Omary Ali Juma na rais wa sasa wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein. Hawa wametunukiwa Nishani ya Mwenge wa Uhuru Daraja la Pili.

Katika orodha hiyo, wapo waliowahi kuwa mawaziri wakuu, Rashid Kawawa, Edward Sokoine, Cleopa Msuya, Dk. Salim Ahmed Salim, Joseph Warioba na Fredrick Sumaye.

Wengine ni spika wa Bunge, Anne Makinda, Pius Msekwa, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, Mkuu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) Jenerali David Mwamunyange na Kamishina Mkuu wa Magereza, Agustino Nanyaro.

Mwamunyange, Mwema na Nanyaro wametunukiwa nishani kwa kuwa ni wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Sherehe za kutunuku nishani hizo zilifanyika ikulu jijini Dar es Salaam na zilihudhuriwa na watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Kuna mambo mawili makubwa yaliyojitokeza katika utoaji wa “nishati za Kikwete.” Kwaza, kuna watu waliotunukiwa nishati hizo, lakini wakionekana kwa wengi kuwa hawakustahili. Pili, kuna wanaoonekana kuwa walistahili, lakini hawakutunukiwa.

Ambao wanatajwa kutostahili lakini wametunukiwa, ni pamoja na rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Huyu anatuhumiwa kupuuzia na, au kunyamazia mikataba ya maangamizi ya taifa kiuchumi wakati alipokuwa madarakani kati ya mwaka 1995 na 2005.

Ni wakati wa utawala wa Mkapa, kinyume kabisa na utashi wa wananchi, uliasisiwa mpango wa kuuza mashirika na makampuni ya umma kwa “gharama ya kutupa.”

Miongoni mwa taasisi zilizoliza wananchi wengi na hata wataalam wa fedha wa ndani na nje ni uuzaji Benki ya Taifa ya Biashara (NBC); nayo kwa bei ya kutupa kwa madai kuwa ilikuwa inaleta hasara.

Ni Mkapa aliyeshinikiza shirika la umeme la taifa (Tanesco) kukubali menejementi ya kukodi – kampuni ya Net Group Solution kutoka Afrika Kusini – kufanya kazi zake.

Ndani ya menejementi hiyo, taarifa zilivuja, kuwa mmoja wa wakurugenzi alikuwa mwanawe. Net Group ilishindwa na kukimbia na kuacha matatizo mengi zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Ufisadi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Akaunti ya Fedha za Nje (EPA) ulitokea wakati Mkapa akiwa madarakani. Ama alipuuza, alikataa, alizembea kufanya kazi yake ya kusimamia rasilimali za taifa kama mkuu wa nchi, au alishiriki moja kwa moja katika ufisadi huo.

Ni wakati wa utawala wa Mkapa, baraza la mawaziri alilokuwa mwenyekiti wake linadaiwa kuamua kuuza nyumba za serikali, jambo lililosababisha watumishi wa umma kuishi hotelini; naye kujiuzia moja ya nyumba hizo.

Si hivyo tu: Wakati Mwalimu Nyerere aliifanya Tanzania kuwa kimbilio la wakimbizi, ni wakati wa Mkapa ilipoandikwa historia chafu ya kuwa taifa linalozalisha wakimbizi.

Utawala wa Mkapa ulishindwa kuzuia mauaji ya wananchi wapatao 40, hapo Januari 26 na 27, mwaka 2001, kwenye maandamano ya amani Unguja na Pemba.

Mauaji ya Pemba, siyo tu kwamba yameipaka doa Tanzania mbele ya jumuiya ya kimataifa; bali yamelitumbukiza taifa katika orodha ya mataifa ambayo hayaheshimu haki za binadamu na uhuru wa kutoa maoni.

Hata hivyo, ni Rais Kikwete na timu yake wanaojua ni vigezo vipi vilitumika kumpa kiongozi huyo wa zamani nishani ya Mwalimu Nyerere.

Anne Makinda: Huyu ni spika wa Bunge la Jamhuri. Kabla ya kushika wadhifa huo alikuwa naibu spika wa bunge.

Makinda hajamaliza hata nusu ya kipindi chake cha uongozi ndani ya Bunge. Hata hapo alipo tayari ameonyesha kushindwa kazi.

Kwa mfano, wakati wa kuwasilisha na kujadili muswada wa mabadiliko ya katiba wa mwaka 2011, Makinda alinyamazia mapungufu mengi na makubwa katika muswada.

Tayari wanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wameishaanika mapungufu hayo hata kwa rais. Yeye, spika, hakujihangaisha kueleza serikali kilichomo katika muswada usio na mafao kwa taifa.

Ni Rais Kikwete na timu yake, wanaojua vema Makinda anatunukiwa kwa lipi. 

Yaliyofanyika kwa Mkapa na Makinda ndiyo hayohayo yaliyofanyika kwa Pius Msekwa, Mwema, Mwamunyange na Nanyaro. Wengi wanaendelea kujiuliza mchango wao ni upi na vigezo gani vilitumika.

Wachunguzi wa mambo wanasema minong’ono ya kusuta na kutokubaliana ingekuwa michache au isingekuwepo kabisa kama nishani kwa polisi ingekwenda kwa aliyekuwa mkuu wa kwanza wa jeshi hilo Elangwa Shaidi.

Au kama nishani ya jeshi ingekwenda kwa Mirisho Sarakikya na ile ya magereza kwenda kwa mkuu wa kwanza wa jeshi hilo,+ Obadia Lugimbana.

Hakuna shaka yoyote kwamba viongozi hao walikuwa na sifa ya kupewa tuzo hizo kutokana na utumishi wao uliotukuka na uzalendo kwa taifa lao.

Wengi wanajiuliza, Dk. Shein “wapi na wapi” na medali ya Nyerere? Haijawahi kufafanuliwa Dk. Shein ametokea wapi na hata rais mstaafu Benjamin Mkapa alipomtaja kuwa makamu wake, wengi walidhani “ameazimwa kutoka nje ya nchi.”

Bali uchaguzi au uteuzi wa Rais Kikwete wa nani apewe nishani ipi, umewapa wananchi fursa ya kulinganisha waliopata na ambao hawakupata.

Tayari wanajiuliza kwa nini John Malecela, aliyekuwa waziri mkuu na makamu wa rais hakupewa nishani. Tayari yeye amewaambia waandishi wa habari kuwa waulize ikulu.

Amani Karume, rais mstaafu wa Zanzibar, naye hayumo. Edward Lowassa wa Richmond, hayumo. Rais wa pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, Spika wa kwanza wa Bunge la Muungano Chifu Adam Sapi Mkwawa na aliyekuwa spika wa Bunge la tisa, Samwel Sitta, nao hawamo.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa njia bora na sahihi ya utawala Zanzibar ni kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa. Amani Karume ameondoka madarakani akiwa ameweka misingi madhubuti ya kuundwa kwa serikali hiyo.

Hakuishia kuweka misingi tu, alihakikisha serikali inaundwa na wananchi wote wanakuwa wamoja. Wengi walitarajia, kwa kazi hiyo tu, angeweza kusikika miongoni mwa waliopata nishani. Hayumo.

Je, tunzo hizi zitamwachia usingizi Rais Kikwete? Je, zinaweza kumaliza minyukano ndani ya chama chake au zitaamsha upya makundi ya uhasama na kutibua nyongo?

0
Your rating: None Average: 2.3 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: