Rais Kikwete, CCM hawataki Katiba Mpya


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 30 May 2012

Printer-friendly version

VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake, hawataki katiba mpya. Wanataka kubakiza katiba iliyopo na kuiita “Katiba Mpya.”

Hili lilianza kuonekana tangu Rais Jakaya Kikwete aliposema, “…serikali yangu itaanzisha mchakato wa kuitazama upya katiba ya nchi yetu kwa lengo la kuihuisha ili hatimaye tuwe na katiba inayoendana na taifa lenye umri wa nusu karne.” Hawakumuelewa.

Lakini limejidhihirisha baada ya Kikwete kuendesha mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama chake mjini Dodoma na kuazimia kipi kiingizwe katika katiba mpya na kipi kiachwe.

Nyaraka kadhaa zinaonyesha Kikwete, ambaye ndiye aliunda kamati ya kukusanya maoni, ndiye aliyesimamia kikao kilichoweka masharti hayo. Je, uko wapi hapa moyo wa kuleta katiba mpya?

Kwa mfano, Jakaya Kikwete na chama chake wameweka “pendekezo” kuwa rais apatikane kwa wingi wa kura (simple majority).

Wanasema, “Siyo kweli kuwa mshindi anayepata kura chache anakuwa amekataliwa na wananchi…fursa iliyotolewa kwa wagombea wengine kupigiwa kura ni kielelezo cha kuwapo demokrsia.”

Hili ni moja ya mapendekezo yalilosukuma wananchi kuchukia katiba iliyopo na kudai katiba mpya. Kikwete anajua hili. CCM wanajua hili, viongozi wanajua hili na wanachama wanalijua pia.

Lakini ndani ya chama cha Kikwete, mshindi hupatikana kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura halali. Je, kama utaratibu wa yule mwenye kura nyingi ndiye mshindi, hata kama aliyeshinda amezidi kura tano, kwa nini CCM wasiutumie utaratibu huo kwenye chaguzi zao? Au Kikwete anataka kusema CCM ni bora kuliko taifa?

Kisingizio kinachotolewa na chama hiki, ni kwamba Tanzania ni nchi maskini; hivyo ikiwa kutakuwa na duru mbili za uchaguzi, baada ya kushindwa kupatikana mshindi katika duru la kwanza, nchi haitaweza kumudu gharama zake. Huu ni mchoko wa kufikiri.

Kwanza, lini uchaguzi wa Tanzania umeendeshwa kwa fedha za ndani peke yake? Hata kabla ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, sehemu kubwa ya gharama za uchaguzi imetoka kwa wafadhili.

Pili, kama kigezo cha kutaka uchaguzi ufanyike mara moja ni ukosefu wa fedha unaotokana na umasikini wa taifa, mbona CCM ambayo ndiyo masikini zaidi inaendesha chaguzi mbili pale mshindi anapokosekana kwenye duru la kwanza?

Ndivyo ilivyotokea kwenye uchaguzi wa kutafuta mgombea ubunge wa jimbo la Arumeru Mashariki, Februari mwaka huu. Siyoi Sumary ambaye alishinda kura za maoni kwenye duru la kwanza, hakutangazwa mshindi hadi duru la pili la uchaguzi lilipofanyika na kushinda. Hivi CCM na Tanzania nani masikini?

Tatu, ni aibu kwa mtu mwenye akili timamu kusema Tanzania ni masikini. Utajiri upo lakini umasikini wa taifa hili unaletwa na watawala. Angalia magari wanayotumia viongozi wa serikali – wingi na gharama yake.

Angalia anasa za watawala? Angalia utajiri walionao baadhi ya watumishi wa umma na familia zao – watumishi wa nyumbani, watoto, wazazi na nyumba ndogo – kila mmoja na kigari chake.

Tanzania imejitwisha zigo la mawaziri na naibu mawaziri 55 kutoka 50 waliokuwapo awali. Kwa viwango vya India vya waziri mmoja kuhudumia watu 35 milioni, Tanzania ingeweza kuwa na mawaziri wawili tu au mmoja na nusu.

Haki na utashi wa raia haviwezi kuwekwa rehani kwa madai kuwa hakuna fedha. Kitendo cha kumtangaza aliyeshinda kwa kura chache kuwa ndiyo rais – bila kurudiwa uchaguzi – chaweza kuingiza nchi kwenye machafuko.

Jingine ambalo linaonyesha CCM hawataki katiba mpya – wanataka kuweka viraka katiba ya sasa na kuita mpya – ni kule kung’ang’ania  muundo wa sasa wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Chama hiki kinajua vema kuwa kwa muundo wa sasa wa Muungano, hicho wanachokiita Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kimeshakufa siku nyingi. Kilichobaki sasa ni jina tu – Serikali ya Muungano.

Viongozi wa serikali ya Zanzibar wamenyofoa kila kitu kwenye Muungano na kukifanya chao binafsi.

Serikali ya Muungano imeshindwa kuchukua hatua yeyote kuidhibiti Zanzibar. Imeishia kuunda kamati ya kutatua inachoita, “Kero za Muungano,” badala ya suluhisho la matatizo.

Nayo kamati iliyoundwa kutatua kero za Muungano imegeuka kero nyingine. Viongozi wake wakuu, wote wawili – Dk. Mohammed Gharib Billal, makamu wa rais wa Jamhuri na Balozi Seif Iddi, makamu wa pili wa rais wa Zanzibar – ni “raia wa kutoka Zanzibar.”

Wasaidizi wao wengine wawili wakubwa, Samia Suluhu, waziri wa nchi ofisi ya makamu wa rais (Muungano) na Mohammed Aboud, waziri ofisi ya mkamu wa pili wa rais Visiwani, pia ni “raia wa kutoka Zanzibar.”

Wazanzibari hawa wanne wamejifungia kwenye kivuli cha Muungano na kuondoa kile ambacho Zanzibar na Wazanzibari wanataka kiondoke.

Ndivyo ilivyofanyika kwenye suala la mafuta na gesi ya Zanzibar. Limetolewa kwenye Muungano. Kilichosalia sasa ni serikali kuwasilisha muswada bungeni utakaoruhusu Zanzibar kuchimba mafuta yake.

Wakati Zanzibar wakiondoa gesi yao, ile inayochimbwa kutoka bara imebaki kuwa mali ya pamoja. Madini na vito vilivyoko bara ni mali ya Muungano. Mafuta yaliyopo bara, nayo ni mali ya Muungano.

Ndani ya Muungano kuna marais wawili – rais wa Jamhuri na rais wa Zanzibar. Ndivyo katiba ya Zanzibar inavyoeleza. Lakini katiba ya Muungano inasema, “Zanzibar ni nchi ndani ya Muungano.”

Je, hapa kuna Muungano au usanii? Hicho kinachoitwa na CCM, “Muungano ulianzishwa kwa hiari na umetazama faida za kiuchumi, kibiashara na kijamii,” kinatoka wapi?

Au ni kule upande mmoja kufaidi mapato ya upande mwingine, wakati upande mwingine ukikumbatia kila kilichochake?

Vilevile, CCM wamependekeza na watahubiri kwa wananchi kwamba mawaziri watokane na wabunge kwa madai kuwa utaratibu huo umekuwa “chachu kati ya mihimili ya Bunge na serikali.”

Kazi ya Bunge ni kusimamia serikali. Sasa mbunge ambaye amekula kiapo cha kusimamia serikali atawezaje kutimiza wajibu wake huo wa kikatiba wakati yeye ni waziri?

Haya ni miongoni mwa mengi ambayo wamependekeza yabaki kama yalivyo.

Muhimu hapa ni wananchi kukataa baadhi ya mapendekezo ya CCM, chama ambacho kimetawala kwa miaka mingi kwa kutegemea mitaji mikuu: ujinga na umasikini.

Wananchi wasimame kidete kutaka Katiba Mpya na siyo viraka.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: