Rais Kikwete chupuchupu


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 31 August 2011

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete amenusurika kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye, taarifa za ndani ya Bunge zimeeleza.

Hii ni iwapo angeridhia kurejea kazini kwa katibu mkuu wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka bungeni mjini Dodoma na serikalini zinasema, mara baada ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kutangaza matokeo ya ripoti ya uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zikimkabili Jairo, baadhi ya wabunge waliweka mkakati wa “kumuondoa Kikwete madarakani.”

Gazeti hili lina orodha ya wabunge wapatao ishirini ambao walikuwa wameanzisha utaratibu wa kukusanya kura ili zikikamilika wapeleke hoja yao ya kutokuwa na imani na rais.

Kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya serikali ameliambia MwanaHALISI mwishoni mwa wiki, “Wabunge waliotaka kuchukua hatua hiyo ni wale waliochoshwa na tabia ya Kikwete ya kutowachukulia hatua wasaidizi wake.”

Alisema mara baada ya Luhanjo “kumsafisha” Jairo, baadhi ya wabunge wakiwamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walijipanga kuwasilisha bungeni hoja ya kutokuwa na imani na rais.

Haijaweza kufahamika mara moja iwapo hoja hiyo ingepita. Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanasema, hata kama hoja hiyo isingeweza kupita, lakini hatua yoyote ya kumjadili rais bungeni, ingeweza kuleta mtafaruku serikalini na hata kwa Kikwete mwenyewe.

Akizungumza mara baada ya mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher ole Sendeka, Naibu Spika, Job Ndugai alisema, “…Haiwezekani, kama dharau inaweza kutokea ni hukohuko wanakofanya dharau hizi, si hapa ndani ya Bunge.”

Kauli ya Ndugai ilionekana kuwaimarisha wabunge; na kwa maoni ya wengi, kama Kikwete asingesoma alama za nyakati na kuamua kutosa maswahiba zake hao wawili – Luhanjo na Jairo – basi kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kujadiliwa bungeni.

Awali Sendeka akichangia hoja hiyo alisema, “…Yaliyoelezwa jana si tu hayawezi kukidhi matarajio ya bunge hili; kwa sababu ninavyopiga yowe kwamba nimeibiwa ng'ombe 100 na baadaye wakapatikana watatu, haiondoi ukweli kwamba aliyechukua ng’ombe zangu ni mwizi.”

Mbunge huyo machachari aliliambia bunge, “…kitendo kilichotokea jana (juzi), kwa kauli ya Katibu Mkuu Kiongozi, si tu kwamba kinaingilia haki na madaraka ya bunge, bali pia kinafedhehesha na kumdhalilisha waziri mkuu.”

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja wiki moja baada ya ikulu kupitia kwa katibu mkuu kiongozi, kutangaza kumsafisha Jairo, ambaye bunge lilimtuhumu kukusanya mamilioni ya shilingi kwa madai ya “kusadia kupitisha bajeti ya wizara yake.”

Aidha, kuibuka kwa taarifa za kuwapo kundi la wabunge waliotaka kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na rais, kumekuja katika kipindi ambacho baadhi ya viongozi wa CCM na wanachama wengine wanapendekeza kutenganishwa kwa kofia mbili za uongozi.

Mjadala wa kutenganisha kofia mbili – ile ya uyenyekiti wa chama na ile ya urais – unatokana na madai kuwa chama kimeshindwa kuisimamia serikali yake.

“Nakuambia, hali pale bungeni ilikuwa tete. Wabunge walikasirika sana na uamuzi wa Luhanjo kumrejesha kazini Jairo bila kulijulisha Bunge. Baadhi yao walikuwa wanazungumza wazi, kwamba ‘sisi hatuna haja tena na Jairo, wala Luhanjo. Hawa ni wateuliwa wa rais. Tutadili na Kikwete mwenyewe,” anaeleza mtoa taarifa.

Anasema suala la kuwasilishwa hoja ya kutokuwa na imani na Rais Kikwete lilikuwa linajadiliwa kwa uwazi na baadhi ya wabunge; kilichokuwa kinasubiriwa ni mmoja wa wabunge kuwasilisha hoja hiyo bungeni.

“Inawezekana habari zile zilifika kwa rais mwenyewe, kupitia kwa baadhi ya wapambe wake. Ndiyo maana haraka aliamuru Jairo aendelee na likizo yake,” ameeleza mtoa taarifa wetu.

Sakata la matumizi mabaya ya fedha za umma linalomkabili Jairo liliibuliwa bungeni kwa mara ya kwanza na mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo.

Alikuwa akichangia bajeti ya wizara ya nishati na madini. Siku tatu baadaye, Luhanjo alitangaza kumpeleka likizo ya malipo katibu mkuu huyo, ili kupisha kile alichoita, “uchunguzi dhidi yake.”

Shelukindo alisema Jairo amekusanya kinyume cha utaratibu, michango ya fedha kutoka taasisi zilizoko chini ya usimamizi wake kwa madai ya “kusaidia bajeti ya wizara kupita kwa urahisi.”

Wakati hayo yanatendeka, taarifa nyingine zinasema, waziri mkuu Mizengo Pinda alitishia kujiuzulu kutokana na hatua ya ikulu kumsafisha Jairo.

“Hata Pinda alitaka kujiuzulu. Alisema kama Jairo ataendelea na kazi bila uchunguzi wa maana kufanyika, basi mimi nitakuwa tayari kukaa pembeni. Ni kwa sababu, kitendo hiki kimenishushia hadhi mbele ya wananchi na taifa kwa jumla,” ameeleza mtoa taarifa akimnukuu mbunge mmoja aliyekaribu na Pinda.

Anasema, “Kikwete aliona ni heri kumtosa Jairo kwa muda huu kuliko kumpoteza Pinda moja kwa moja. Hatua ya kumpoteza Pinda ingeweza kusababisha mvurugano ndani ya chama na serikali...”

Kauli ya kiongozi huyo inashabihiana kwa kiwango kikubwa na kilichomo katika taarifa iliyotolewa na idara ya mawasiliano ya rais, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika taarifa hiyo, ikulu inasema, “Mheshimiwa rais aliamua kuwa Ndugu Jairo asirudi kazini mpaka kwanza yeye rais atapoamua namna gani ya kurudi kazini, lini na wapi.”

Kauli hii nayo inaonekana kupendekeza kuwa rais huenda asimrejeshe Jairo mahali pake, bali kumpeleka sehemu nyingine.

Mara baada ya hoja juu ya Jairo kuibuka, Pinda alilileza bunge, “Ningekuwa na mamlaka, tayari ningewaambia ndugu Jairo nimeshamfukuza kazi,” kauli ambayo inaonyesha aliridhika na tuhuma zinazomkabili.

MwanaHALISI lilipouliza mwandishi wa habari wa waziri mkuu, Saidi Nguba juu ya kuwapo kwa taarifa za waziri mkuu kutaka kujiuzulu, haraka alisema, “…Aaaah umeipata wapi hiyo kaka.”

Nguba alisema, “…siwezi kusema lolote. Hizo ni interpretation (tafsiri) tu. Lakini siwezi kubeza vyanzo vyako vya habari, ingawa sidhani kama hilo lilitaka kutokea.”

Nyaraka kadhaa ambazo MwanaHALISI imezipata zinaonyesha Jairo alikusanya zaidi ya Sh. 600 milioni kinyume cha taratibu.

Taarifa kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikulu na wizara ya nishati na madini, zinaonyesha Jairo alivyokusanya mamilioni hayo ya shilingi katika kipindi kifupi cha miezi mitatu kuelekea bajeti kuu ya taifa.

Alikusanya fedha hizo kupitia taasisi zilizo chini ya wizara yake – mamlaka ya udhibiti na nishati (Ewura), shirika la petroli la taifa (TPDC), mamlaka ya umeme vijijini (REA) na shirika la umeme la taifa (TANESCO).

Hadi sasa, si Jairo wala mtetezi wake mkuu Luhanjo, aliyeeleza wananchi na taifa, maana ya hicho kinachoitwa “kuwezesha bajeti ya wizara kupita kiurahusi.”

Kwa mujibu wa barua kutoka kwa Jairo, iliyoandikwa 23 Juni 2011, kati ya tarehe 24 na 26 Juni mwaka huu, katibu mkuu huyo wa nishati tayari aliagiza na kukusanya kinyume cha taratibu, kiasi cha Sh. 85 milioni. Fedha hizo zilitoka EWURA, TPDC, REA na TANESCO.

Barua ya Jairo iliyobeba kichwa cha maneno, “Maandalizi ya semina kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” iliagiza fedha hizo kukusanywa ndani ya siku moja. Alisema, “…Napenda kuwafahamisha kwamba ushiriki wa wizara pamoja na kukodisha ukumbi utahitaji Sh. 39 milioni na ushiriki wa wabunge utahitaji Sh. 46 milioni.”

“Kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wa wizara, tunashauri EWURA, TPDC, REA na TANESCO wagharamie gharama za semina ya wabunge kwa kuchangia Sh. 22 milioni kila mmoja,” alieleza.

Alielekeza malipo yafanywe mara moja kupitia mhasibu wa wizara, Bi. Hawa Ramadhani, simu Na. 0762 222216.”

Gazeti hili halikuweza kumpata Bi. Hawa ili kufahamu utaratibu uliotumika katika kukusanya fedha hizo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: