Rais Kikwete hajamchoka Mrindoko?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 04 May 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki
Bashir  Mrindoko

WIKI iliyopita, Rais Jakaya Kikwete alifanya uteuzi wa naibu makatibu wakuu wapya 10 katika wizara mbalimbali ndani ya serikali yake. Miongoni mwa walioteuliwa, ni Bashir Mrindoko aliyefanywa naibu katibu mkuu wizara ya maji.

Kabla ya uteuzi huo, Mrindoko alikuwa kamishna wa nishati na mafuta ya petroli katika wizara ya nishati na madini.

Ndani ya serikali na hata ikulu kwenyewe, hakuna asiyemfahamu Injinia Bashir Mrindoko. Ni mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi, ama kwa kushiriki moja kwa moja vitendo vya ufisadi au kunyamazia na hivyo kubariki na, au kushabikia vitendo hivyo katika ufanikishaji wa mkataba tata wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Company (LLC).

Aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza Richmond, Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela CCM) aliliambia Bunge, 7 Februari 2008 kuwa Mrindoko alitenda vitendo vilivyosaidia “kampuni hiyo ya mfukoni kupewa kazi na serikali.”

Wengine waliotakiwa kufutwa kazi, ni aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali, Johson Mwanyika, aliyekuwa katibu mkuu wa wizara ya nishati na madini, Arthur Mwakapugi na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah. 

Katika taarifa yake bungeni, Dk. Mwakyembe alieleza mengi juu ya ushiriki wa Mrindoko katika mradi huu.

Kwa mfano, Dk. Mwakyembe alisema kamati yake ilijiridhisha kuwa “…Mrindoko ndiye aliyeiandikia Richmond barua ya kusitisha mkataba wake na serikali mwezi mmoja tu kabla ya mchakato wa zabuni ya kufua umeme wa dharula haujaanza.”

Kwamba 30 Juni 2004, Mrindoko aliijulisha kampuni hiyo iliyojiita ya Marekani kuvunjwa kwa mkataba wake wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Katika mkataba huo wa Januari 2006, serikali iliipa Richmond haki maalum na ya kipekee ya miezi 18 katika umiliki wa mradi wa huo.

Kwamba pamoja na kuandikia barua Richmond kujulisha kuvunjwa kwa mkataba wake, Mrindoko hakueleza serikali utapeli wa kampuni hii wakati wa kumtafuta mzabuni wa kufua umeme.

Kwamba ama kwa makusudi, au kwa kunyamazia, Mrindoko alishindwa kupendekeza kwa serikali umuhimu wa kuifanyia Richmond uchunguzi ili kuthibitisha uwezo wake kifedha, kiutendaji na kitalaam.

Kwa makosa hayo na mengine, Bunge likaagiza serikali “kumchukulia hatua kali za kinidhamu mtumishi huyo wa umma” kwa kushindwa kuishauri vema serikali hadi kuipa kazi kampuni hiyo iliyothibitika kutokuwa na uwezo, sifa wala hadhi ya kupewa kazi iliyoomba.

Makosa ya Mrindoko na wenzake, ndiyo yalisababisha hadi sasa serikali kukaliwa kooni na mrithi wa Richmond – makampuni ya Dowans Holding S.A na Dowans Tanzania Limited – yanayotaka kuchota kutoka serikalini Sh. 94 bilioni.

Aidha, hatua ya Mrindoko kunyamazia udhaifu wa Richmond ndiyo umesababisha serikali kulipa mabilioni ya shilingi kwa kampuni hewa; huku yenyewe ikizidi kudhoofika kwa kuingiza nchi katika miradi ya kifisadi.

Hivyo basi, kwa uteuzi huu wa Mrindoko, Rais Kikwete anagawanyika pawili: kutamu na kuchungu. Huku anasema anapambana na ufisadi kwa chama chake kutaka kuaminika kuwa kinataka “kujivua gamba” na huku anarejesha watuhumiwa wa ufisadi serikalini.

Februari 2008, Kikwete alitenda hivyohivyo. Alimteua Andrew Chenge kuingia katika baraza lake la mawaziri lililoundwa kufuatia “kujiuzulu” kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na waziri mtangulizi wake katika wizara hiyo, Dk. Ibrahim Msabaha.

Wakati Kikwete anamteua Chenge kuingia katika baraza la mawaziri, tuhuma dhidi ya mwanasiasa huyo zilikuwa tayari zimeshika kasi.

Miongoni mwa tuhuma hizo, ni kufikiwa kwa makubaliano yenye shinikizo la rushwa zilizotolewa kwa baadhi ya watendaji serikalini yaliyoazaa mkataba kati ya TANESCO na kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ambao hivi sasa umekuwa mzigo usiobebeka kwa taifa.

Hata shirika la kupambana na ufisadi duniani, Transparency International (TI), katika ripoti yake, lilimtaja Chenge kuwa mmoja wa wakubwa waliohakikisha mkataba huo unasainiwa.

Leo hii, vitendo vilivyofanywa na Chenge ndani ya serikali vimekuwa ni miongoni mwa mambo yanayomuandama Kikwete na chama chake.

Hivyo basi, hata kama Kikwete hataki kuamini kuwa Mrindoko alishauri vibaya au alishindwa kushauri vizuri serikali, hakupaswa kumteua katika nafasi yake ya sasa.

Vinginevyo wananchi wataweza kutafsri kuwa Kikwete amelenga kulidhoofisha Bunge. Lakini Kikwete hajasema mahali popote kuwa ripoti ya Bunge ilikuwa na kasoro, jambo ambalo limemfanya yeye kuipuuza.

Wala Kikwete hajaunda chombo kingine kulichunguza Bunge lililotuhumu Lowassa na wenzake kuipa kazi kampuni isiyokuwa na sifa na hajaeleza tofauti na kile kilichosemwa na Bunge.

Wala Kikwete hawezi kusema hakusoma ripoti ya Bunge. Aliisoma na kwa hakika, aliielewa vema. Wala rais hawezi kusema kilichopelekwa bungeni hakubaliani nacho. Ndiyo maana anatumia ripoti ya Bunge kutaka kufukuza wenzake ndani ya chama.

Hivyo basi, katika mazingira ya sasa ya Kikwete kutaka kuthibitishia ulimwengu kuwa yeye na chama chake wanataka “kujivua gamba,” uteuzi wa aina hii, hauwezi kufikia malengo hayo.

Bali, uteuzi huu utakuwa unachochea ufa miongoni mwa wanachama na viongozi na kati yake na baadhi ya marafiki zake. Vilevile, uteuzi huu utaweza kufukua yale ambayo yalianza kusahauliwa.

Kwa mfano, kama Kikwete ameshindwa kumfuta kazi Mrindoko, badala yake ameamua kumpa mamlaka makubwa zaidi, ina maana yuko tayari kusahau hata tuhuma za dhidi ya wale ambao CCM inaita mafisadi?

Ndipo baadhi yetu tunaona kuwa Kikwete hana dhamira ya dhati ya kuondoa mafisadi ndani ya serikali yake. Anachokifanya sasa, ni usanii wa kisiasa.

Haiwezekani Mrindoko ambaye Bunge limemtuhumu kushindwa kushauri vizuri aliyekuwa katibu mkuu wake, Arthur Mwakapugi, Kikwete akajiaminisha kuwa ataweza kufanya kazi hiyo sasa.

Vyovyote itakavyokuwa, Mrindoko atakuwa amepoteza, moja kwa moja, sifa ya kuwa msaidizi wa rais, kwani ameshindwa kutimiza majukumu yake aliyokabidhiwa na taifa.

Yuko wapi Nape Nnauye, katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye amejiapiza kuwa “baada ya kumaliza mafisadi katika chama, kazi hiyo itahamia serikalini?”

Kama Kikwete mwenyewe ambaye ndiye mkuu wa serikali haoni tatizo la kuwapo mafisadi ndani ya serikali, nani awezaye kusema ufisadi ndani ya serikali ya CCM ni tatizo?

Kama rais anataka kujenga hadhi ya serikali yake, sharti aangalie uteuzi wa watendaji wake. Sharti ajiridhishe kuwa uteuzi wowote atakaoufanya hauwezi kuzua manung’uniko miongoni mwa viongozi wake na wananchi.

Je, kwa uteuzi huu, Kikwete atapata usingizi? Je, anaweza kuacha kusema kwamba “urais wake hauna ubia?” Je, Kikwete anaweza kusema kwa uhakika kwamba yuko salama na uteuzi huu utaweza kumbakisha salama?

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: