Rais Kikwete na msalaba aliojichongea


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 27 May 2008

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

KUONGOZA nchi ni sawa na kubeba msalaba. Rais ndiye Mkuu wa nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.

Pia ni sehemu ya Bunge (la Wawakilishi), maana muswada ukishapitishwa bungeni, unahitaji saini yake kuwa sheria. Pia ana uwezo wa kuvunja Bunge likimkatalia muswada wake.

Rais ndiye kichwa na mabega yanayobeba uzito wa nchi. Baadhi ya maamuzi yake ni yake. Ni kisima cha uzima na uhai wa taifa na watu wake.

Ndiyo maana, katika utendaji wa kazi na shughuli zake, Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri wa mtu, isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba kulingana na ushauri huo.

Tofauti na Yesu Kristo aliyesaidiwa (kidogo) kubeba msalaba njiani na waliomhurumia akielekea Golgota, Katiba inampa Rais uwezo kuteua mawaziri wamsadie shughuli za kila siku; lakini bado, kama kichwa na mabega ya nchi, hawezi kukwepa majukumu au kuwajibika kwa utendaji mbovu wa aliowateua.

Rais ajijutie na kujilaumu iwapo, kwa udhaifu, ameteua "wasanii" wa kurukia msalaba mabegani mwake na kujining'iniza mithili ya tumbili na hata kutaka "kubembea" na kuongeza uzito mabegani kwake.

Ni heri awe "dikteta mwema" kuliko kuteua Baraza la Mawaziri mafisadi, wababaishaji, wanaojipendekeza kwa nidhamu ya woga, maana kwa kufanya hivyo atakuwa amefungwa nira nao; mzigo utamlemea, nchi itayumba.

Atafika Golgota amechoka, majeraha na jasho la damu yamejaa mwilini. Na kama kweli msalaba aliojichongea ni mzigo wa dhambi kwa uzembe unaoepukika, umma utamsulubu, mafisadi watapona.

Wanadharia wa kisiasa, kutoka mwanafalsafa Aristotle na wengine mfanowe, hadi mwanzoni mwa karne iliyopita, walisema mengi kuhusu dhana na hatima ya serikali, lakini wameandika machache mno kuhusu watawala.

Plato alijihusisha zaidi na uteuzi wa wawatala bora, Machiavelli kuhusu mbinu zao na Montesquieu kuhusu idadi yao, lakini wote hawa, waliona suala la kutawala na aina ya utawala, jambo dogo.

Na pengine ni kwa sababu wamezingatia Katiba, leo tuna watawala wasioambilika na wasiolazimika kufuata ushauri (Katiba yetu Ibara 37). Wana kinga hata wanapohalifu dhamana waliyopewa.

Hawashitakiki mahakamani kwa kosa lolote la jinai (Katiba, Ibara 46).

Katiba pia inamkingia kifua Rais dhidi ya mtu yeyote anayetaka kumshitaki mahakamani kwa jambo lolote alilotenda au alilokosa kutenda binafsi (na msalaba wake) kama raia wa kawaida, kabla au baada ya kushika Ikulu.?

Taasisi ya urais ni msalaba mzito, pana na ngumu kuiendesha, hasa katika mazingira ya kukosa Katiba toshelezi huku mifumo na miundo mingi akiipanga yeye.

Tofauti na wenye Katiba makini na imara, uteuzi wa wasaidizi wa Rais (dhana ya Plato), mbinu za kutawala (dhana ya Machiavelli) na idadi ya mawaziri (dhana ya Montesquieu) hutegemea utashi wake. Hiki ndio kigezo kwa uamuzi wake na kwa vipi angependa ajichongee msalaba wa uzito gani.

Tumbili waning'inia msalabani wako tele kwa kila serikali. Uteuzi wao ni ishara ya udhaifu wa Rais na ukosefu wa umakini katika kuchagua kwa vigezo na viwango maslahi kwa Taifa.

Wakiendelea kuwapo, hususani katika Baraza la Mawaziri, huongeza uzito wa msalaba na huwa mzigo kwa wananchi na taifa. Asipofungwa nira nao, rahisi kuwaondoa.

Ni kazi ngumu. Wananchi wakilalamikia ufisadi uliokithiri, atawapapasapapasa kwa kuwafuta jasho usoni, akiwaambia waondoke huru ili kumpunguzia bughdha.

Atalipamba tukio la kuondoka kwao kama "ajali ya kisiasa" wakati wameharibu. Mafisadi watarudi majimboni na kupokewa "kishujaa."

Rais, mkuu wa nchi asiyehojika, anapaswa kuonyesha njia kwa utaratibu makini. Atumie mbinu bora za uongozi kuepusha chombo kupinduka au kuzama. Hapaswi kufungwa nira na tumbili waovu. Ikitokea, ana haki ya kuwaadabisha. Tunakumbuka awamu mbili za kwanza.

Mhanga wa kwanza kwa vita dhidi ya ufisadi alikuwa Waziri wa Sheria wa kwanza Tanganyika, hayati Chifu Abdallah Fundikira mwaka 1962, alipotimuliwa na Rais Julius Nyerere kwa kubainika amepokea rushwa.

Alifuatia Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Augustine Mwingira aliyetimuliwa mwaka 1981 alipokodi ndege mbovu kwa mfanyabiashara wa Lebanon, George Hallack, iliyotakiwa na Shirika la Ndege nchini (ATC). Matukio ya kifisadi yakiitwa ni uhujumu uchumi.

Rais Ali Hassan Mwinyi alifungua milango. Ingawa alionyesha makeke kidogo mwanzoni kwa kuvunja Baraza la Mawaziri, kilichofuata ni kuangalia wasaidizi wakipora na kubinafsisha raslimali za taifa.

Awamu ya tatu iliridhia hayo, na ikaanzisha yake, chini ya bilhamu "utandawazi." Wabembeaji msalaba wa Rais walipata washirika wageni na kuibua tabaka "Mibaka-Uchumi."

Wanyonge waliitwa "wavivu wa kufikiri" na "wenye wivu" ambao haidhuru hata wakila nyasi.

Sehemu kubwa ya uzito wa msalaba sasa ni mapokeo ya awamu hizo mbili: Sakata la rada, ndege ya Rais, IPTL, EPA n.k. Ni sehemu ya msalaba aliojichongea Rais Kikwete.

Wananchi hawana tatizo na Rais wao, ila huumwa anapolinda tumbili wala mahindi. Amebeza ya Plato, Machiavelli na Montesquieu? Je, si Rais huyu, ambaye wakati akitaja Baraza la Mawaziri la kwanza, alisema, "wengine siwaelewi vizuri." Kama hakuwaelewa vizuri, alichaguliwa?

Je, si yeye aliyesema, katika hali iliyoonyesha wazi hakupata muda wa kujiandaa kuteua, "majina rasmi ya Baraza la Mawaziri, sanjari na wizara zao, nimeyaandika kwa mkono na nimefutafuta."

Haraka ya nini hata kusababisha kashfa na mawaziri wabovu kujiuzulu wakati wameshahujumu Taifa na uchumi? Ni haramu kuita mashujaa.

Kubakiza mawaziri wa kubahatisha kunaliweka Taifa rehani au kuchezea Watanzania. Kumbe semina elekezi za Ngurdoto ziliangamiza tu kodi.

Rais ataendelea kuteua hata wahuni. Iweje wakati ubunge sasa unanunuliwa? Sababu kubwa, kama alivyosema Mwalimu Nyerere mwaka 1995, ni rushwa.

Hakuna anayeshinda bila kuhonga, na kwa sababu hii, CCM imeonyesha mwelekeo mbaya katika kupata wagombea kuliko chama chochote.

Huu ushahidi. Licha ya jina langu kupitishwa na ngazi zote za juu za Chama kuwa mgombea nafasi, joto la "takrima" lilinitoa nje maana sikuhonga. Uchaguzi ni msimu wa kuvuna!

Kwa sababu tayari ni utamaduni unaokubalika, chama kinakwenda wapi? Rais anapaswa kubeba vyema msalaba aliojichongea, vinginevyo "Golgota" yake itakuwa chungu na ngumu.

Badala ya kuyafumbia macho maovu, ya sasa na yaliyopita, angeiga wenzake wanaotawala katika mazingira kama haya.

Levy Mwanawasa alipoingia madarakani Zambia, aliweka wazi hatahurumia mafisadi. Thabo Mbeki wa Afrika Kusini hakumstahi Makamu wake, Jacob Zuma, alipogundua alikula rushwa. Bingu wa Mutharika hakunyamazia wala rushwa Malawi wakati wa Rais Bakili Muluzi.

Haya yote ni kutambua kuwa wanaotawala ni watoto wa wakulima na wafanyakazi; wanajua babu zao, baba zao na ndugu zao wanahitaji kulindwa badala ya kuingizwa utumwani.

Na huo ndio msalaba aliojichongea Rais Kikwete ambao anapaswa kuubeba salama si kwa visingizio vya "ajali ya kisiasa."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: