Rais Kikwete usikwepe majukumu


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 05 August 2008

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete amemaliza ziara ya "kikazi" ya siku 10 mkoani Tanga, wiki mbili zizopita. Hivi sasa yupo mkoani Iringa kwa ziara ya siku nane.

Bila shaka hii, rais Kikwete atakuwa rais wa kwanza wa Tanzania kutembelea mkoa mmoja kwa muda mrefu.

Nimetaja ziara ya "kikazi" inayohusisha ukaguzi wa miradi ya maendeleo, pamoja na kukutanana na wananchi. Sijazungumzia ziara za mapumziko, kama alivyowahi kufanya mkoani Mwanza miezi michache baada ya kuchaguliwa kuwa rais.

Najua si kosa hata kidogo kwa kiongozi kutembelea mkoa anaoutaka, kwa wakati anaotaka na kwa urefu wa muda aupendao.

Hata hivyo, utaratibu wa kiongozi kuzuru mkoa mmoja kwa siku 10 ni utaratibu mpya nchini. Viongozi wote waliopita walikuwa wanafanya ziara ya mkoa mmoja si zaidi ya siku tatu.

Sasa tujiulize: kwa nini Kikwete anafanya ziara ndefu kama hii katika mkoa mmoja?

Wapo wanaosema kwamba anafanya hivyo kutokana na kutopenda kukaa Ikulu. Ndiyo maana wanasema ameamua kufanya safari ndani na nje ya nchi.

Wapo wenye mashaka kwamba hatua ya Rais Kikwete kutopenda kukaa Ikulu kwa muda mrefu, inatumiwa vibaya na baadhi ya wasaidizi wake.

Wananchi wanaamini kwamba kushindwa kutoa maamuzi mazito na makini kwa rais Kikwete kunatokana na kuwa mbali na wananchi wake.

Tangu alipochaguliwa kuwa rais Desemba mwaka 2005, Kikwete amefanya safari nyingi nje ya nchi, hadi kufikia hatua ya vyombo vya habari na wananchi kulalamika kwamba rais wao hakai nchini.

Ni vema rais anaposhindwa kutoa maamuzi pengetolewa maelezo ili wananchi wabaki na imani kwa kiongozi na serikali yao. Kukaa kimya kunajenga hofu na uvumi.

Sasa hali inaharibika zaidi inapoonekana wasaidizi wake " kwa maana ya washauri na watendaji wa rais " wanatoa kauli zinazozidi kukanganya badala ya kurekebisha kasoro.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ni mfano hai. Alipotoa maelezo kuhusu umiliki wa kampuni ya Meremeta na suala la Zanzibar kama ni "nchi" au la; wanaompinga Pinda wametoa hoja nzito katika masuala hayo.

Pinda pia anabebeshwa lawama za kutotoa maamuzi kuhusu utekelezwaji wa mapendekezo ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza utata wa mkataba wa Richmond.

Kamati hiyo iliyoongozwa na mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, ilitaka serikali iwachukuwe hatua wote waliohusika na mkataba huo.

Hao ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea. Wengine ni maofisa wa ngazi ya juu katika serikali.

Wananchi wengi waliona kwamba rais angepaswa kutoa uamuzi katika suala hili. Hakupaswa kuwapa kazi nyingine ya kuchunguza ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Hii ni kutokana na ukweli kwamba wenyewe walitakiwa kuwajibishwa kwa mabaya waliyohusishwa nayo.

Wengi waliona rais angeweza, pasina shida yoyote, kuwaondoa kwenye mamlaka aliyowapa ili kulinda maadili na heshima ya serikali katika ahadi yake ya kupambana na rushwa na ufisadi.

Lengo kuu hapa ni kuona nchi inastawisha watumishi waadilifu na wenye kuheshimu misingi ya utawala bora. Lakini, inashangaza rais kuamua kubaki kimya juu ya jambo hili.

Mtendaji mwingine wa rais aliyejikanganya ni Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo ambaye ameliambia Bunge kwamba fedha za EPA si za serikali.

Hoja nzito zimetolewa kupinga kauli ya Mkullo. Miongoni mwa waliopingana na Mkullo, ni gavana wa kwanza wa BoT na aliyepata kuwa waziri wa fedha mzalendo, Edwin Mtei.

Hatua kubwa ambayo imeleta heshima ya serikali, ni ile ya kumkataza Mkuregenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, kutoa taarifa kwa wananchi, taarifa ambazo zilikuwa hazionekani kuwa ndio msimamo wa rais. Badala ya taarifa kumjenga rais, zilikuwa zinamuangamiza.

Sasa swali kubwa hapa, ni kipi kinachomsinda rais kuchukulia hatua watendaji wake wanaomuangusha na kuangamiza serikali yake? Tunataka kuona hatua zinachukuliwa sasa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: