Rais Kikwete usimpe kazi ‘Ocampo’


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Gumzo

KWA haya, hakuna atakayeepuka kukamatwa na Fatou Bensouda “Ocampo” wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC) mjini The Hugue, Uholanzi. Fuatana nami.

Fatuma “Ocampo” aweza kuchunguza wahusika katika kutekwa, kupigwa na kujeruhuwa kwa Dk. Steven Ulimboka, mwenyekiti wa jumuiya ya madaktari nchini.

Dk. Ulimboka – mtetezi wa maslahi ya madaktari na haki za wagonjwa – alitekwa, kuteswa, kupigwa na kisha kutupwa katika msitu wa Majipande, nje ya jiji la Dar es Salaam na wanaoitwa na serikali, “watu wasiojulikana.”

Katika hili, “Ocampo” aweza kuchunguza Rais Kikwete ama kubariki au kunyamazia; au ama kuzembea kiapo chake cha kulinda uhai wa raia.

Aweza kuchunguzwa pia kwa uzembe wa kushindwa kupata suluhu kwenye mgogoro kati ya serikali na madaktari.

Uchunguzi unaweza kuanzia pale Dk. Ulimboka anapotaja jina la mtu aliyemteka na kusema ni “mwajiriwa wa Ikulu.”

Dk. Ulimboka anasema anamfahamu aliyemteka; na aliwahi kukutana naye wakati wa mgogoro wa kwanza wa madaktari.

Kikwete ameliambia taifa kuwa serikali yake haihusiki na kutekwa kwa Dk. Ulimboka. Akatuhumu madaktari kuendesha mgomo kwa kile alichodai “ni kinyume na maagizo ya mahakama.”

Serikali ikamkamata kiongozi wao, Dk. Namala Mkopi. Ikamfungulia mashitaka ya jinai mahakamani kwa madai ya “kukiuka amri halali ya mahakama.”

Katika mgogoro huu, ni serikali iliyokimbilia mahakamani kuzuia mgomo; lakini haikurudi huko kuiridhisha mahakama kuwapo kwa ukiukwaji wa amri yake.

Aidha, “Ocampo” aweza kuchunguza kigugumizi cha rais cha kunyamazia wito wa kutaka kundwa kwa tume huru.

Ni tofauti na ilivyokuwa kwenye mauwaji ya wafanyabiasahara watatu wa madini mkoani Morogoro mwaka 2006. Hapa rais aliunda kwa haraka, tume huru ya Jaji Mussa Kipenka.

Orodha ya wanaoweza kuchunguzwa ni ndefu. “Ocampo” aweza kuchunguza minendo ya siri ya kachero Na. 2 katika idara ya usalama wa taifa, Jack Zoka anayetajwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ndiye aliyepanga mpango wa siri wa mauaji, utekaji na utesaji wa Dk. Ulimboka.

Aweza kuchunguza mauaji ya raia katika kipindi cha kuelekea chaguzi ndogo za Arumeru, Igunga na baadhi ya kata.

Katika chaguzi hizo, ndiko wabunge wawili wa CHADEMA mkoani Mwanza, Salvatory Machemli (Ukerewe) na Highness Kiwia (Ilemelela), walijeruhiwa kwa mapanga.

Inadaiwa kuwa wabunge hawa walishambuliwa mbele ya askari polisi; na gari iliobeba washambuliaji inamilikiwa na mmoja wa viongozi wa CCM.

Kazi ya uchunguzi ya kifo cha Mbwana Masoud aliyefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha wakati wa kuelekea uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Igunga, yaweza kufanyika. Mbwana alikuwa mfuasi wa upinzani.

Katika kipindi hicho, ndipo pia mwenyekiti wa CHADEMA katika kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo alichinjwa kama kuku na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika.”

Mbwambo alikuwa mkosoaji mkuwa wa serikali na alikuwa mwiba kwa viongozi wa chama kilichopo ikulu.

Mauwaji ya 5 Januari 2011, jijini Arusha yaliofanywa na jeshi la polisi, nayo yaweza kuchunguzwa.

Vurugu za kisiasa za kisiasa za 26 na 27 visiwani Zanzibar, nazo zaweza kuchunguzwa na kumpa kazi “Ocampo.”

Katika mauaji hayo ya Januari 2001, visiwani Zanzibar, polisi kwa kushirikiana na vikosi vya serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wanaripotiwa kutumia risasi za moto kuondoa maisha ya raia. Hadi leo hii, hakuna hatua zilichokuliwa.

Si hivyo tu: Katika kipindi cha utawala wa Mkapa, watu zaidi ya 52 wanadaiwa kufukiwa chini ya mgodi wa dhahabu wakiwa hai, huko Bulyanhulu, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.

Ukatili huu dhidi ya mwanadamu ulifanyika kati ya 30 Julai hadi 7 Augosti 1996. Watu wengine wanaokadiriwa kufikia laki nne, walifukuzwa kwenye makazi yao na wamiliki wa mgodi.

Ilifahamika baadaye kuwa polisi walitekeleza ukatili huu baada ya kulipwa ujira wa kiasi cha dola za Kimarekani 3,000 (sawa na Sh. 13.5 milioni wakati huo) na kampuni ya Sutton Resources Limited ya nchini Canada.

Kampuni hii ilidai kumiliki mgodi huo kupitia kampuni ya Kahama Mining Corporation Ltd.

Jeshi la polisi lilifanyakazi ya kuhamisha watu kwa nguvu, licha ya kuwapo zuio la mahakama kuu kanda ya Tabora. Hapa “Ocampo” aweza kuangalia ushiriki wa Mkapa na serikali yake katika mauaji na ukatili huo.

Mbali na Mkapa mwingine anawajibika kuulizwa hili, ni Tuamini Kiwelu, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga wakati mauaji yanafanyika.

Huyu ndiye anayethumiwa kusimamia zoezi la uhamishaji watu, wakati kukiwa na amri halali ya mahakama.

“Ocampo” hapa aweza kuchunguza juu ya tuhuma za kubariki; au kunyamazia vitendo vya ukatili vilivyofanywa na polisi dhidi ya binadamu, matumizi mabaya ya madaraka hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Awezaye kuulizwa hili, ni Omari Mahita, aliyekuwa mkuu wa jeshi la polisi wakati wa utawala wa Mkapa.

Kiongozi huyu wa polisi, kinyume na kiapo chake, alijipa kazi ya kupigia kampeni CCM. Siku moja kabla ya uchaguzi mkuu wa 2005, huku akijua kuwa ni uwongo, Mahita alilitangazia taifa kuwa Chama cha Wananchi (CUF) kimeingiza silaha aina ya visu na majambia.

Mwingine ambaye “Ocampo” anaweza kuanza kuuliza, ni aliyekuwa rais wa Zanzibar, Dk. Salimin Amour.

Pamoja na kwamba kiongozi huyu hakuwa na dola, lakini ndiye aliyekuwa anatoa kauli zilizochochea uhasama visiwani Zanzibar.

Katika kipindi cha utawala wake – Oktoba 1990 hadi Januari 2001 – Salimin aliliongoza taifa hilo kwa njia ya kibaguzi. Baadhi ya kauli zake ndiyo chimbuko kuu la mauaji ya haraiki ya Januari 2001 Unguja na pemba.

Naye Adadi Rajabu, aweza kuchunguzwa juu ya ushiriki wake wa moja kwa moja; au kushindwa kutimiza wajibu wake, katika kipindi achoshika nafasi ya mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai.

Adadi ambaye sasa, ni balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, aweza kujibu tuhuma za uhalifu zilizofanywa na baadhi ya polisi waliokuwa chini yake.

Hivyo hivyo kwa Robert Manumba. Aweza kuhojiwa kwa uzembe au kubariki yale yaliokuwa yanafanywa na Adadi na mengine ya sasa.

Katika mshololo huu, mtu pekee anaweza kuikoa serikali kuchunguzwa, ni rais Kikwete pale atakaporidhia uundwaji wa tume huru kuchunguza, pamoja na mambo mengine, waliomteka Dk. Ulimboka.

Kwa haya, mwendesha mashitaka mkuu wa ICC, aliyechukua nafasi ya Luis Moreno Ocampo, bila shaka amepata kazi nchini.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: