Rais Kikwete na Waandishi: Wasiokula rushwa wako wapi?


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 03 March 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi
Rais Jakaya Kikwete

WAKO wapi waandishi wa habari wa Tanzania? Wamelala? Wamepigwa kafuti? Wamenyauka? Rais Jakaya Kikwete amesema waandishi wa habari wanakula rushwa? Wote? Hakuna anayepinga; anayekana? Hakuna anayechefuka kwa kutaja rushwa?

Wako wapi wasiokula rushwa? Hawana sauti? Zimekwenda wapi? Au wanakula? Au wanataka kula? Au waliishakula au kulishwa? Mbona kimya?

Mbona waandishi-walimu vyuoni hawakani kula rushwa? Wako wapi wa TIME, DSJ, ROYAL, MSJ, MAMET?

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – taasisi ya uandishi na mawasiliano ya umma; kwenye asasi nyingine za habari – TAJA, AJM, MISA, MCT, TAMWA – mbona kimya? Huko rushwa inaliwa?

Twende kwenye vyumba vya habari – penye wahariri, maripota na wasaidizi wao –mbona hakuna sauti kuwa hawali rushwa? Kimya hicho ni kukubali au kukataa kauli ya rais?

Kama kuna mwenye woga wa kujisemea, basi ajue kuwa rais aliyesema waandishi wanakula rushwa, anamfahamu naye pia kuwa ni mlarushwa.

Hivi wasiokula rushwa wana woga gani? Si wanaweza kusimama na kujihesabu na kupaza sauti wakisema, “Sisi wasimamao hapa, hatuli rushwa?”

Yako wapi maandamano ya waandishi wa habari wasiokula rushwa ya kumpasha rais, kumkosoa, kumuumbua na hata kumnyamazisha? Kimya?

Wako wapi wasiokula rushwa – waseme hadi mbingu ipasuke. Wapinge. Wakane. Wakatae kutuhumiwa na kuhusishwa na rushwa. Wapo?

Kama wapo wamepigwa wakapigika. Wamebaki na mishahara ileile ya tangu kuondoka kwa Kristo Yesu – haishibishi, haiwekeki, haitumiki kimantiki – imebaki mkia wa mbuzi.

Kama wapo hawana vyombo vya kupitishia maoni yao. Vile vya wanaowatumikia vimeshikwa na wenyenavyo na hao mabaunsa walinda “sera” na matakwa ya wamiliki.

Kama kuna wasiokula rushwa wanaitwa walalamishi. Wanaambiwa wachokozi waliojaa fitina. Wanaambiwa ni shauri ya umasikini wao. Wanaitwa “maskini jeuri” wasagalami watakaodondoka mitaani matumbo wazi.

Rais Kikwete alisema hata hawa wanakula rushwa? Hawa? Hakuwatofautisha na wala rushwa awajuao – wale ambao ni sehemu ya mkia uchipukao kwenye nyayo zake?

Hapana. Kauli ya rais haikuwatendea haki wale wasiokula rushwa. Si wasimame sasa na kupinga; na kukana; na kueleza uadilifu wao?

Si wasimame na kujitofautisha na mkia umfuatao rais na mawaziri lakini uliojaa majigambo na ndweo?

Na kauli ya rais ina maana nyingi. Inaweza kuwa imelenga kulegeza misuli ya waandishi wasiokula rushwa. Si sasa wamwambie kwa sauti na ujasiri kuwa hawali rushwa?

Inaweza kuwa imelenga kuwaambia wala rushwa kuwa wajihadhari; kwani wanaandika wasichoamini na hivyo wataumbuliwa.

Ama wanyamaze; huo mwanga wa “ukombozi” uliokuwa umeanza kuwajia waukimbie; au wajiunge na upande wa rais na kutetea asemacho na kuacha “chokochoko.”

Kauli ya rais inaweza kuwa imelenga kuwaweka kapu moja, walarushwa na wasiokula rushwa. Hii yaweza kulenga kuleta mfarakano miongoni mwa waandishi na asasi zao.

Rais anaposema anajua kitu, siyo “vizuri sana” kumbishia. Aweza kuwa anajua. Kasema waandishi wa habari wanakula rushwa na anawajua. Hakuwajua leo au jana. Bila shaka ni matokeo ya uchunguzi au ufuatiliaji.

Kauli ya rais yaweza kuwa imelenga kulinda “wenzake” – waandishi vipenzi na swahiba – ili wasishambuliwe na wenzao, kwani wakati wa kuwatumia kama vipaza sauti ndio umewadia.

Bali rais hataji walarushwa. Anawalinda. Anawahifadhi kama nyenzo maalum ingawa ni nyenzo dhalili. Kutowataja kunamsaidia yeye. Akiwataja itafahamika kuwa wako karibu na ana uhusiano nao.

Kwani kuna aliowapa nafasi katika utukufu wake wa kisiasa. Baadhi wameshindwa kazi na wengine wanajikongoja. Baadhi wamesukumwa katika vyombo vya habari ili, kila siku, waandike “kumtukuza bwana.”

Miongoni mwa walarushwa ambao rais hataki kutaja ni waandishi waliojaa majigambo kuwa wanaendesha magari ya kifahari. Wanawacheka wenzao kwa kusema “wana misimamo mikali isiyoweza kuwasaidia.”

Waandishi walarushwa ni pamoja na wale wanaojigamba kwa kujenga nyumba kubwa na za kifahari.

Jaribu kukaa karibu nao; utasikia mmoja akimwambia mwenzake kuwa nyumba yake ina ghorofa; siyo kama ya mwenzake isiyo na ua na geti.

Mwingine atasikika akisema kwamba nyumba yake ina “vyumba vya ardhini” kama mapango na Kandahar na kwamba huwezi kuingia kwake bila kumulikwa na kamera.

Mishahara yao inafahamika. Wako karibu na watawala – marafiki wa rais, mawaziri na wabunge. Rais anawajua. Si awataje?

Kuna orodha ndefu ya waliojigamba tangu Kikwete anaigia madarakani kwamba atawapa ukuu wa mkoa au wilaya. Wameatamia mawazo hayo hadi yamezeeka.

Yawezekana kwa hao, kauli ya rais ililenga kuwataarifu kuwa hana nafasi tena. Bali yawezekana pia ililenga kuwafahamisha kuwa kazi walizofanya kuelekea ushindi wake mwaka 2005, ndio sasa zinaanza.

Kuna waandishi ambao wamenunua laini nyingi za simu. Wamezitumia kutuma ujumbe (sms) au kuita waandishi wa habari wanaodai kuwa uandishi wao “hauonyeshi sura nzuri ya watawala.”

Wamewatukana kwa madai kuwa wanawachafulia mipango yao na mahusiano na “wakubwa” wanaowadondoshea makombo.

Wanawakebehi, kuwakejeli na hata kutishia kuwaua.

Baadhi ya waandishi wa aina hiyo walikuwa kwenye orodha ya wachagizaji upande wa watawala katika mbio za uchaguzi za 2005. Rais hawataji kwa majina walarushwa hao.

Rushwa iliyohusishwa na waandishi wa habari ndiyo imeleta mgawanyiko mkubwa miongoni mwa vyombo vya habari na piga-nikupige ya maneno na hisia.

Wakati chombo kimoja cha habari kimeapa kuhakikisha kinafichua ufisadi na kuanika wahusika; kingine kimekuwa kichaka cha waliodaiwa na, au waliothibitika kuwa mafisadi.

Siyo siri tena kwamba vyombo vya habari, vyumba vya habari na hata waandishi mmojammoja, wanajitambulisha katika makundi mawili makubwa.

Makundi hayo ni lile la waandishi walioapa kutetea mtuhumiwa au mthibitika kuwa fisadi; na lile ambalo linasema “piga ua” litamwanika fisadi.

Kauli ya Rais Kikwete kuwa waandishi wanakula rushwa, bila kuwataja majina, kusema mahali walipo na kuonyesha hatua aliyochukua kuwakabili, haiwezi kusaidia kung’oa aina ya gugu lililoshambulia shamba la waandishi.

Ufisadi mkuu uliofanywa kwa ushirikiano wa watawala, wawakilishi wao, makampuni ya nje na wafanyabiashara – ule wa kukwapua mabilioni ya shilingi kutoka benki kuu – unafunikwa na watawala na sehemu ya waandishi.

Upande mmoja wa mwandishi wa jamii umeoza kwa kutopea katika ombaomba na ulaji makombo ambao unajisifia kwa kujenga nyumba kubwa, kuweka umeme na kuwa na magari ya kifahari.

Upande uliobaki unanyimwa hewa na lishe. Unapigwa vijembe, kejeli na kusakamwa kwa vitisho vya kuuawa. Lakini wasiokula rushwa si waje mbele na kuwa wazi kwamba hawakubaliani na rais?

Wako wapi waandishi wa habari wasafi na asasi zao? Hakuna maandamano au taarifa ya kupinga rais kuwaita wote walarushwa?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: