Rais mtarajiwa ni mzushi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 16 March 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala
Bernard Kamilius Membe

MIONGONI mwa watu wanaotajwa kuwa kwenye mzunguko wa mwisho kuelekea ikulu katika uchaguzi mkuu ujao ni Bernard Kamilius Membe.

Mbunge huyo wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi na waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa inadaiwa analalia mlango wazi bahati ya Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete waliowahi kuwa mawaziri wa wizara hiyo.

Wakati wote, Membe amekuwa makini katika kauli zake ili asichafue ‘CV’ yake.

Lakini wiki iliyopita, ‘rais huyo mtarajiwa’, alijibebesha furushi la uzushi akaenda kulifungua mbele ya wanahabari, “Ooh kuna chama cha siasa kinafadhiliwa na nchi za nje ili nchi isitawalike!”

Membe hakutaka kuwa muwazi lakini ukweli alikuwa anaungana na Waziri wa Jinsia, Watoto na Wanawake, Sofia Simba aliyekituhumu moja kwa moja Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa kinapokea fedha kutoka nje ili nchi isitawalike.

Kwa hiyo, Membe ameendeleza upotoshaji na kulialia kama katika hotuba ya Rais Kikwete, kauli za Waziri mkuu Mizengo Pinda katika ziara ya mkoani Kagera; Waziri Steven Wassira na katibu wa uenezi, John Chiligati.

Badala ya kujibu hoja, wameona njia inayofaa ni kujaza hofu watu, kutisha, kudanganya, kuzusha kuwa CHADEMA inataka nchi isitawalike.

Tujiulize, tangu lini kupokea fedha kutoka nje ni hatari kwa usalama wa nchi? Kama hivyo ndivyo, Membe aeleze hatari ya serikali ya Tanzania kupokea misaada kutoka kwa wahisani au wafadhili wa nje.

Mbona katika bajeti ya serikali kati ya asilimia 35-40 ya fedha zake zinatoka nje—Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)? Nchi kama Uingereza, Uswisi, Ubelgiji, Uholanzi, Marekani ndizo hufadhili pia vyama vya siasa na asasi zisizo za kiserikali (NGO’s).

Je, si kweli kwamba CHADEMA inawaumbua viongozi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ufujaji na wizi wa fedha za misaada? Rada na ndege ya rais vyote vimenunuliwa kwa bei ya ‘kuruka’, halafu wakabuni mikataba ya kifisadi kama ya Richmond/ Dowans.

Wakati serikali inaziita nchi wahisani kuwa ni marafiki wa maendeleo, vyama vya siasa vinaziita nchi hizo kuwa marafiki wa demokrasia. Mbona haikuwa nongwa CCM kupokea fedha kutoka chama cha kikomunisti cha China?

Inajulikana, marafiki wakubwa wa CHADEMA ni chama cha Conservative cha Uingereza. Hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana CCM walikuwa wanadai CHADEMA imetumia vibaya misaada ya marafiki zao hao.

Wamekuwa kama Muamar Gaddafi. Ulipoibuka uasi alidai ni Marekani lakini baadaye akasema ni al-Qaeda. Watu waamini vipi?

Upotoshaji huu unafanywa kwa makusudi na serikali ya CCM iliyochoka ambayo Membe anaungana kuficha ukweli kwamba serikali hiyo inatumikia mafisadi kwa sababu inapata fedha za kifisadi.

Serikali ya CCM ndiyo imetetea makada waliovimbiwa fedha za rushwa hadi wakaenda kuziweka kwenye mabenki ya nje.

Badala ya kujibu hoja, serikali ya CCM imejiingiza katika uzushi na vitisho vya kutumia dola kuzima elimu ya uraia inayotolewa na CHADEMA na sasa NCCR-Mageuzi kuhusu udhalimu wa serikali hii.

Tujiulize, nani alifukia watu wakiwa hai katika mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu mwaka 1996 ni CHADEMA au mwekezaji kwa msaada wa serikali? Nani amesababisha maelfu ya vijana kukosa ajira baada ya kuporwa maeneo ya kuchimba madini Nzega, North Mara na Bulyanhulu ni CHADEMA au serikali?

Vitabu vya Mungu vinasema alaaniwe mwenye kuabudi mafisadi, mwenye kuabudu fedha, mwenye kupunguza mipaka ya ardhi ya watu wengine. Yuda alimsaliti Yesu kwa sababu ya vipande vya fedha akalaaniwa akajiua, vipi serikali?

Hata kama serikali itatumia dola kupiga watu, kuwatia ndani kwa madai ya uchochezi, kuwazushia uongo, ukweli utabaki serikali ya CCM wanayotumikia Sofia, Membe iko kwenye kwapa la mafisadi.

<p> 0753 626 751</p>
0
Your rating: None Average: 4.7 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: