Rais na serikali wanalidharau Bunge?


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 28 December 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

SAKATA la David Jairo linaelekea kusahaulika. Hii si bahati mbaya bali ni mpango mahsusi. Kwa bahati mbaya, mkakati wa kupunguza makali ya ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoshughulikia suala hili unafanana sana mikakati mingine ya huko nyuma.

Tunaikumbuka Richmond; kamati teule ilitoa ripoti na kusababisha baraza la mawaziri kujiuzuru na kuundwa upya. Baada ya pigo hilo ambalo lilisababisha Rais Jakaya Kikwete alaumiwe sana na marafiki zake, alijuta moyoni na kuasisi mkakati wa kuchelewesha utekelezaji wa mapendekezo mengine ya tume hiyo.

Vikao vya bunge vilikaa na kila wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipotakiwa kutoa taarifa ya utekelezaji wa maazimio 23 ya kamati teule ya Richmond, aliibuka na maelezo yaliyojaa siasa na ahadi hewa.

Matokeo yake, baadhi ya watuhumiwa wakuu wa ripoti hiyo wakastaafu, wengine wakabadilishwa kazi na wengine kuhamishiwa nafasi nyingine. Watuhumiwa wengine kama mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hoseah mpaka leo bado anakalia kiti chake licha ya Bunge kuigiza awajibishwe.

Baada ya bunge kuvunjwa na uchaguzi mkuu kufanyika, Chama Cha Mapinduzi (CCM) walionyana juu ya kuchokonoa tena utekelezaji wa maazimio yale 23. Hivi sasa huwezi kumsikia mbunge wa CCM akidiriki kuhoji utekelezaji wa maazimio yale.

Mkakati huu ulifanya kazi vizuri hata kama uliacha majuto kwa Lowassa anayeonekana kuwa mhanga wa uamuzi wa haraka wa kujiuzulu. Mpaka leo, wapambe wa Lowassa wanaamini kuwa kama asingejiuzuru mwenyewe, hakuna ambaye angemlazimisha kujiuzuru na si ajabu angekuwa bado ni waziri mkuu.

Spika Samwel Sitta ni mhanga wa pili wa mkakati wa serikali kulikwamisha Bunge. Baada ya serikali kushtuka kuwa ilikuwa ni makosa kumruhusu Lowassa kujiuzuru, rais Kikwete alitumika vema kumlainisha Sitta.

Kulikuwa na hofu kubwa kuwa Sitta alikuwa na weredi wa kutosha kujenga hoja juu ya uhuru wa bunge mbele ya serikali. Hali hii iliitisha sana serikali na kuamua kumtumia Kikwete ili amlainishe. Lugha nzuri ya kiungwana na ahadi kem kem zilimlewesha Spika huyu wa viwango na kasi hadi kumfanya alegeze msimamo wake wa kuitaka serikali itekeleze maazimio 23 ya Bunge. Sitta alianza kugeuka na kuanza kuwashambulia waliokuwa wanadai maazimio yale yatekelezwe.

Kwa kitendo hiki, Sitta akapata malipo ya aina mbili. Kwanza, alipojengewa hoja ya kufukuzwa kwenye chama chake kwa kuidhalilisha serikali bungeni, alikingiwa kifua kwa ujanja na Kikwete.

Pili, alijengewa hoja ya jinsia na kuenguliwa katika kinyanganyiro cha uspika. Mpaka leo anajuta kumjua Kikwete kwa ustadi wake kuwatumikia mafisadi huku akiigiza kuwaunga mkono wapambanaji wa ufisadi. Hadi leo hii, Sitta bado anauguza vidonda vya majeraha ya dhambi hiyo.

Hivi majuzi CCM kupitia vikao vyake ilipatana kujivua gamba na kuwataka mafisadi ndani ya chama hicho wajiondoe, vinginevyo chama kingewafukuza ama uanachama au uongozi. Hata orodha iliandaliwa ndani ya vikao vya siri.

Rostam Aziz, aliyekuwa mbunge wa Igunga, mtuhumiwa muhimu wa ufisadi na kada maarufu wa chama hicho, kwa haraka na jazba kama ya Lowassa, akatangaza kuachia ubunge na nafasi nyingine za uongozi. Muda mfupi baada ya Rostam kujiuzuru, CCM na serikali walijipanga na kuibuka na mkakati wa kukwamisha azma ya kujivua gamba.

Ilifika mahali hata mtu wa kuandika kwa watuhumiwa alikosekana. Alipopatikana wa kuandika barua, akakosekana wa kuisaini. Alipopatikana wa kuisaini, akakosekana wa kuwapelekea; mwisho barua hiyo imeishia kabatini kwa Kikwete!

Huku nyuma mzozo ukazuka wa nani ni fisadi na kujivua gamba maana yake nini. Vikao vilikaa na hata miniti za vikao vilivyopita na mapatano yake kuhusu kujivua gamba hazikupatikana ikabidi watafute magazeti kukumbuka waliazimia nini. Mpaka leo hakuna anayejua kwa hakika nini kinaendelea kuhusu kujivua gamba. Mkakati wa kuchelewesha maamuzi magumu umefanya kazi.

Likafuata sakata la Jairo, katibu mkuu wa wizara sugu ya nishati na madini. Mbunge Beatrice Shelukindo akasimama bungeni na barua mkononi, akamtuhumu Jairo kuagiza ukusanywaji wa fedha kutoka mashirika yaliyo chini ya wizara hiyo kwa kazi ya “kuwezesha” bajeti ya wizara yake kupitishwa na bunge. Nje ya Bunge, Jairo alisikika akiwabeza wabunge kuwa “hawajui wafanyalo.”

Serikali ikaliingia suala hili kwa jazba kama Lowassa wa Richmond na Rostam wa kujivua gamba. Ikamsimamisha kazi na kuagiza achunguzwe. Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali (CAG) akamkagua na kutoa ripoti kuwa Jairo hana hatia yoyote.

Katibu mkuu kiongozi wa Ikulu, Philemon Luhanjo, akapiga vijembe na kusema Jairo hana kesi. Akamtaka kurejea kazini mara moja. Kesho yake akalakiwa ofisini kwake kwa shangwe.

Huku Bunge likifuta mavumbi ya kugaragazwa na kundi la wakiritimba wa ikulu, likaja juu na kuagiza kamati teule iundwe kuchunguza sakata hilo. Kamati ikateuliwa na hatimaye ikatoa ripoti yake. Ikatamka kuwa Jairo ana hatia pamoja na waandamizi kadhaa wa ikulu na serikali. Kamati ikaagiza wachukuliwe hatua. Mpaka sasa hakuna hatua iliyochukuliwa.

Kuna mgogoro unaendelea wa nani achukue hatua – rais? Katibu mkuu kiongozi (mtuhumiwa), waziri mkuu, katibu mkuu wa wizara? Hii si bahati mbaya bali ni mkakati ule ule wa kulihujumu bunge na kulidhalilisha.

Ukimwuliza Jairo atasema acha lidhalilishwe maana limekuwa kigeugeu. Wabunge walipokea fedha za “posho” wakiwamo wakubwa kama Pinda na Spika Anne Makinda na wengine wengi, lakini sasa wanajifanya kuja juu na kujifanya ni waadilifu!

Je, nani anaweza kutuondoa hapa tulipokwama? Haijulikani, lakini kiongozi wa serikali anajulikana. Huyo achukue hatua haraka na kuonyesha yeye na si serikali. Analiheshimu bunge lisilo na heshima. Halina heshima kwa sababu linapokea posho (rushwa) ya kupitisha bajeti, halafu linageuka na kudai aliyewapa posho awajibishwe.

Itakumbukwa kuwa mara baada ya mbunge Shelukindo kuibua sakata hili bungeni kwa kutoa ushahidi wa barua ya Jairo, Pinda alisimama na “kulialia” akisema kama angekuwa yeye ndiye rais, angechukua hatua mara moja maana suala lenyewe “halikuwa na njia ya kulitetea” likaeleweka.

Ikiwa Pinda alitamka wazi kuwa Jairo alikuwa chini ya mamlaka ya rais kwa kuwe ndiye aliyemteua, kwa nini sisi tunashuhudia watu kutupiana mpira katika suala la kutekeleza maazimio ya kamati teule iliyomchunguza?

Katika hali ya kawaida, mtu aweza kuhisi rais ambaye ndiye mteuzi wa nafasi hii, ana maslahi binafsi yanayotishiwa na maoni ya Bunge. Kuchelewa kutekeleza mapendekezo ya kamati teule ambayo baada ya kufikishwa mbele ya bunge yanageuka kuwa maagizo ya bunge, si kudhalilisha bunge tu: Ni kuidhalilisha serikali yenyewe na taasisi ya urais inayotegemewa kuwa mfano wa kuheshimu mamlaka ya wananchi walioliweka Bunge.

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: