Rais wetu Kikwete unajitakia chuki dhidi yetu


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 05 May 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

ANNE Anney ni mlemavu wa miguu anayeishi Arusha. Siku moja alifunga safari hadi ikulu kukulilia ili uweze kurudisha Azimio la Arusha – azimio lililowafanya wananchi kuishi kwa upendo, amani, umoja na mshikamano.

Lakini hakufanikiwa kukuona. Polisi walipoona mlemavu na kibaiskeli chake anakaribia lango lako (nyumbani kwa baba yake) kulalamikia pamoja na mambo mengine utendaji mbovu wa baadhi ya polisi na watendaji walio chini yako, ‘walimchangamkia’ kama kibaka au jambazi asiye na pesa.

Walimkamata na kumtia mahabusu kwa siku nne kabla ya kumfungulia mashtaka. Alipofikishwa mahakamani, polisi wakasema upelelezi haujakamilika. Akapelekwa gerezani alikokaa kwa miezi minne.

Anne ameshtakiwa kwa kile wanachodai, “alikukashfu,” na kwamba sasa ni miezi sita toka adhaminiwe na amekuwa mtu wa kiguu na njia kutoka Arusha hadi Dar es Salaam kufuatilia kesi yake.

Je, rais wangu Jakaya Kikwete haiwezekani kesi hii kuhamishiwa Arusha au mlalamikaji kufuta shauri lake? Mbona tunaambiwa kuwa mlalamikaji anaweza kufuta shauri lake kortini? Si useme basi, “yaishe jamani” maana ameshitakiwa kwa kosa la kukukashifu wewe!

Rais wangu, taifa limeona ulivyoshughulikia mambo mazito kama yale ya watuhumiwa wa wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT).

Ni wewe uliyesamehe vinara wa ukwapuaji – kampuni za Kagoda Agriculture na Deep Green. Je, kama haya uliweza, hili la huyu mlemavu ambalo ni dogo zaidi linakushinda vipi?

Baba ninaposema anatembelea kibaiskeli cha miguu mitatu usidhani ni zile baiskeli za minyororo halafu mlemavu ananyonga kwa mikono, hapana. Hiki kibaiskeli kametengenezwa ili asukumwe na mtu.

Kwa kuwa hana mtu wa kumsukuma, anazungusha mwenyewe matairi ya nyuma kwa mikono yake. Huyu anatembelea makalio yake.

Rais wangu Kikwete, tumesoma na kuelezwa, kwamba kila nafsi itaonja umauti. Ni kweli. Maana tayari wengi wametangulia na baadhi yao ulikuwapo katika kuwasindikiza katika nyumba ya milele.

Wengine wameacha kumbukumbu njema kwa kazi nzuri waliyoifanyia jamii yao. Wapo walioacha simulizi za ukatili, mateso, dhuluma na hata ufisadi.

Je, wewe umejiandaa kuacha kumbukumbu gani kwa watu wako wa nyumbani na jamii kwa jumla? Ni kwa sababu, uzito wa wajibu wako, unalingana na dhamana uliyopewa.

Watanzania walikuchagua kwa matumaini makubwa kuwa ungewatatulia kero zao, ungepambana na dhuluma, uonevu na ungesimamia misingi ya utawala bora. Lakini sivyo ilivyo.

Fimbo ya mchungaji inaonyesha matatizo ya wananchi yamezidi kuongezeka badala ya kupungua. Miaka mitano yote hii, umeitumia kusherekea ushindi badala ya kushughulikia matatizo yao.

Badala yake unaanza kuokoteza kazi njema iliyoanzishwa na kusimamiwa kwa umahiri mkubwa na akili za wengine. Kwa mfano, nani asiyejua kuwa mradi wa shule za kata ni kazi iliyofanywa kwa umahiri mkubwa na aliyekuwa msaidizi wako, Edward Lowassa?

Ndiyo maana Lowassa alipoondoka, ameondoka na kila kitu chake. Hakuna tena moyo wa kujenga shule mpya. Hata mwamko ambao serikali iliujenga kwa wananchi, umekufa mithiri ya ng’ombe aliyekwama katika tope.

Shule zilizojengwa kwa gharama kubwa ya muda na fedha, zimegeuzwa vijiwe vya watoto kukulia na kujifunza kuvutia bangi.
Miaka mitano imemalizika si kwa maendeleo.

Ndani ya serikali na chama chako – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – kumejaa majungu, fitna na malumbano yasiyokwisha. Hakuna tena amani, upendo, mshikamano na umoja ulivyovikuta kabla ya kuingia madarakani.

Wapo wanaosema kwamba kisa cha haya yote ni matukio ya ufisadi yaliyoibuka katika siku za hivi karibuni, ambapo ndani ya Bunge na katika chama kumejengwa makundi mawili, moja likipinga ufisadi na jingine likiunga mkono. Inawezekana.

Lakini toka zamani ufisadi ulikuwapo, bali hakukuwahi kutokea chuki kubwa kama ilivyo sasa. Leo watu wanahubiri chuki dhidi ya wenzao usiku na mchana huku wewe ukinyamazia.

Katika baadhi ya maeneo umekuwa ukitajwa hata kuyabariki makundi ndani ya chama chako. Baadhi ya wasaidizi wako wanahusishwa na kutawanya taarifa za chuki, majungu na fitina katika baadhi ya vyombo vya habari.

Mfano hai unaotolewa ni taarifa iliyoandikwa katika gazeti la serikali – Habari Leo – iliyotuhumu wabunge wa chama chako kutaka kukuhujumu.

Kuna madai yanayoweza kuthibitishwa kwamba taarifa ile ambayo ilileta kizaa zaa hadi bungeni, ilitoka ndani ya ofisi yako na iliandikwa na mmoja wa wasaidizi wako wa karibu.

Lengo la kuchapishwa kwa habari ile kunatajwa kuwa ni kutaka kudhoofisha vita dhidi ya ufisadi ambavyo baadhi ya wabunge walikuwa wamejipambanua navyo.

Kama hapo ndipo tulipofika, taifa hili linaelekea wapi? Mbona uchaguzi unakuja na sisi kama taifa tunaonekana kama nyani jangwani, tukipanda vichuguu tukidhani tunakwea miti?

Rais wangu, taifa limetoka katika enzi za kufikiri na sasa linaelekea kucheza ngoma. Tukiambiwa huyu ana mvuto tunatimka. Hatuangalii hata historia ya huyo tunayeelezwa.

Tukiambiwa huyu fisadi tunaitikia na kumshambulia bila kufikiri kuwa maisha ya huyu anayetuambia hayo ni ya anasa sawa sawa na ya tunayeambiwa ni fisadi au ana mvuto.

Rais wangu, nitaendelea kusema ukweli kwa yote yaliyo ya haki. Wananchi wameanza kukata tamaa na utawala wako. Wanasema ndani ya serikali na hata katika chama, hakuna tena umakini.

Mfano wa wanaoutoa ni hatua yako ya kusaini kwa mbwembwe sheria ya Gharama za Uchaguzi wakati ulikuwa hujaisoma vizuri. Matokeo yake ikalazimika kurudishwa bungeni kujadiliwa tena.

Ni kweli kwamba wewe ni mkuu wa nchi, na hivyo siyo lazima uchambue mwenyewe kila sentensi. Umewaweka watu wa kufanya kazi hiyo.

Lakini kilio cha wananchi kwako ni juu ya kushindwa kwako kuchukulia hatua dhidi ya wasaidizi wako waliokuingiza mkenge hadi kusaini sheria ambayo haikupitishwa na Bunge.

Baada ya sheria kurudishwa bungeni wahusika wote walipaswa kuwajibishwa kwa kukuvunjia heshima rais wa nchi na kukufanya uonekane kituko.

Je, rais wangu kama unashindwa kuwawajibisha wanaotenda kosa kubwa kama hilo, kwa kulinda heshima ya kiti cha urais, kwa nini usiwajibike wewe?

Heshima ya kiongozi haitoki kwa wananchi tu, bali inatokana na uadilifu na umahiri wa uongozi wa rais mwenyewe. Kama utendaji wako ni dhaifu wawaachie wengine watende. Wasing’ang’anie madaraka.

Mfano, unaye mtendaji mkuu wa polisi anayepaswa kuangalia maisha ya raia, lakini umejionea kwa macho yako raia alivyokufa kama kuku mikononi mwa polisi kutokana na kinachoitwa, “dozi ya mahojiano.”
Hakuna anayeulizwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani naye ameamua ‘kuuchuna’. Wote wanaingia ofisini asubuhi na vimulimuli vyao na wanatoka jioni watakavyo.

Simama uwaambie Watanzania ni nini kilichotokea katika kituo cha polisi Chang’ombe. Na wewe ukiwa kimya wananchi watasema rais hatufai maana waliishasema Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurence Masha hawafai na wewe ukaamua kunyamaza!

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: