Rashid Kawawa ameondoka na CCM yake


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 06 January 2010

Printer-friendly version
Gumzo
RASHID Mfaume Kawawa

RASHID Mfaume Kawawa, mmoja wa waasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na taifa, ameondoka huku akiwa bado anahitajika.

Familia, viongozi, wanachama wa CCM na taifa, walikuwa bado wanamhitaji hata katika uzee aliokuwa nao. Alikuwa kiungo chao. Baba ni baba hata kama hana uwezo tena wa kukusaidia. Hutaki atoke.

Historia yake katika kipindi cha siasa hai za kutafuta uhuru na kuongoza taifa, inaonyesha kuwa Kawawa hakuwa mbinafsi na hakuamini katika unafiki.

Kwake uongozi ulikuwa na miiko yake. Tofauti na viongozi wa sasa ambapo fitina na majungu ni sehemu ya maisha yao. Kwa Kawawa ilikuwa kinyume chake.

Hakujimlibikizia mali kama wafanyavyo baadhi ya viongozi wa sasa. Kwake na kwa sehemu kubwa ya maisha yake katika siasa, uongozi ulikuwa ni utumishi, na kwamba hakuwahi kugeuza dhamana ya uongozi kuwa sehemu ya kutafutia utajiri.

Pamoja na kwamba alishika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini na katika chama, ikiwamo waziri mkuu, makamu wa pili wa rais, waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa, Kawawa alikufa akiwa mhitaji kama wahitaji wengi.

Aliishi kwa uchuuzi. Hadi anafariki dunia, alikuwa akifanya biashara ya kuuza uyoga. Je, kwa nafasi alizopata kuzishikilia, kama angetaka kujitajirisha binafsi, nini kingeweza kumzuia?

Bali Kawawa aliishi kwa misingi ya imani iliyowekwa na chama chake –Tanganyika African National Union (TANU) na baadaye CCM, kwamba uongozi ni dhamana.

Ni kwa hali hiyo, pamoja na kwamba Kawawa ameishi hadi ametafuna “ruzuku,” bado wengi waliomfahamu vema, walishindwa kujizuia kumlilia na kutamani kuendelea kuwa pamoja naye. Wengine wamelia hadi kuzirai.

Lakini wapo waliolia kwa unafiki. Wanafahamika hata kwa majina. Ni wale ambao matendo na kauli zao havifanani na Kawawa tunayemjua.

Lakini wanaoamini kuwa alikuwa mwema na mwadilifu, wataendelea kumlilia daima. Wataendelea kutafakari kitakachofuata baada ya yeye kuondoka. Wataishi kwa kukumbuka mchango wake katika uongozi na katika chama chake.

Lakini swali moja muhimu la kujiuliza ni hili: Je, katika orodha ya sasa ya viongozi na wanachama wa CCM, nani awezaye kufafana na Kawawa? Jibu liko wazi. Ni wachache sana.

Inawezekana, baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka na CCM kuishi katika chumba cha mahututi, sasa kifo cha Kawawa kina maana ya kifo cha CCM? Kuna wanaosema na kuna ukweli ndani yake, kwamba kuwepo kwa Kawawa kulisaidia angalau, kubakisha chama hiki katika umoja, japo wa kuungaunga.

Ameondoka na kuacha viongozi wake wakiparurana hadharani, wakinyukana mchana kweupe na wakitukanana hadi kuvuana nguo hadi kuitana “wehu.”

Wala hakuna tena mashaka, kwamba CCM ya Kawawa na si hii ya Jakaya Kikwete, Yusuph Makamba, Edward Lowassa na Rostam Aziz. Chama cha Kawawa kimebaki katika ofisi za msajili wa vyama vya siasa nchini.

CCM ya Kawawa, yenye katiba yake, ambayo Mwalimu Nyerere alisema “nzuri tu,” ina kanuni zake na inakataza rushwa katika uongozi na kusisitiza viongozi kuwa waadilifu na waaminifu; inakataza viongozi kujilimbikizia mali kwa njia ya rushwa.

CCM hii tunayoiona imeshindwa kuchukua hatua kupambana na rushwa hata katika chaguzi zake. Imeshindwa kusimamia watendaji ndani ya serikali na katika chama chenyewe. Imeshindwa kurudisha umoja kwa wanachama na viongozi wake na kwa viongozi wa kundi moja dhidi ya kundi jingine.

Matokeo yake, chama kimesambaratisha umoja wa kitaifa uliokuwapo. Kimezorotesha uchumi na kimepalilia uvunjifu wa maadili.

Ni CCM hii ambayo inahusishwa na tuhuma za ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika Akauti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT), kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture Limited na makampuni kadhaa wa kadhaa.

Ni ukwapuaji huo unaomhusha rais aliyeondoka madarakani na mwenyekiti wa chama aliyestaafu, unahusisha pia baadhi ya viongozi wa juu wa chama wakiwamo wajumbe wa Kamati Kuu (CC).

Pamoja na kwamba tuhuma hizo ziko wazi, hakuna kiongozi ambaye anajihangaisha kutaka kusafisha chama chake; utadhani ukwapuaji ni moja ya sifa za uongozi.

Wachache wanaojitokeza, hasa wale waliokuwa nje ya mkondo wa ukwapuaji, wanasakamwa kila kukicha. Ndio hao ambao katibu mkuu wa chama, Luteni mstaafu Makamba anaita “wehu.”

Je, nani amefikisha chama hiki mahali hapa? Orodha ni ndefu. Kuna rais mstaafu Alli Hassani Mwinyi. Huyu ndiye aliyezika Azimio la Arusha na kuleta la kwake la Zanzibar. Ni hapo ambapo viongozi walianza kujilimbikizia mali na kuweka njia za mkato za kutafuta madaraka.

Lakini aliyekubuhu katika kuiangamiza CCM, ni Benjamin Mkapa. Huyu alishindwa kukemea rushwa kwa vitendo. Ni wakati wa Mkapa ambapo chaguzi za chama na hata serikali ziligeuka mnada wa ununuzi wa kura.

Migawanyiko ndani ya chama ikazaliwa. Mwanza wakagawanyika kutokana na baadhi ya wanachama kununua uongozi. Arusha na Singida vivyo hivyo.

Hadi sasa, CCM imegawanyika katika maeneo kadhaa. Mfano hai, ni mnyukano wa viongozi wa mkoa wa Mara ambao umeambukiza hata wanachama wa kawaida.

Mkoani humo, mjumbe wa NEC, Christopher Gachuma na mwanasiasa Enock Chambiri, hawawezi kupikika katika chungu kimoja. Kila mmoja kati ya wanasiasa hawa ana kundi lake linalomtumikia.

Ni hapa ambako makundi haya yanahatarisha hata uhai wa chama chenyewe. Kwa mfano, kundi moja likiunga mkono mgombea wake, kundi lingine liko tayari kupeleka nguvu kwa mgombea mwingine hata ikibidi kutoka vyama vya upinzani. Ni katika staili ileile ya wewe umemwaga mchuzi, mimi namwaga ugali.

Hali ni hiyohiyo katika mkoa wa Mbeya. Mkuu wa mkoa, John Mwakipesile amejenga kambi yake inayopambana na mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.

Mwakipisile na Mwakyembe walishindana katika kinyang’anyiro cha ubunge wa jimbo la Kyela mwaka 2005. Mwakyembe alishinda. Lakini tangu kumalizika kwa uchaguzi jimboni humo, Mwakipesile na Mwakyembe hawapikiki chungu kimoja.

Mkoani Tabora, Spika wa Bunge la Jamhuri hapikiki chungu kimoja na mjumbe wa NEC, Rostam Aziz na kundi lake lililobeba wanasiasa kama Profesa Juma Kapuya.

Makundi haya mawili yamegawana wanachama na viongozi. Kila kundi limebeba wafuasi wake. Kundi la Sitta limebeba wabunge wengi mkoa humo, huku wenzake wakibeba viongozi wengine wa kata, wilaya na matawi.

Je, Kawawa yuko wapi katika haya? Nani aweza kumlilia hadi kuzirai kama si kuweka mbele unafiki wa kisiasa?

Mbali na hilo, ni Mkapa aliyegeuza ikulu kuwa pango la biashara; aliyevunja misingi ya utawala bora kwa kuingia katika biashara, tena kubwa, huku akiwa bado na madaraka ya kuongoza nchi.

Ni Mkapa “aliyetoa” mali ya umma kwa makampuni ya kigeni – kwa njia ya ubinafsishaji ambao haukuwa na roho ya mwananchi.

Si hivyo tu, mwaka 2005 Mkapa alinyamazia wajumbe wa NEC kuamsha hisia za udini, ukabila na ujimbo katika nchi.

Viongozi wa CCM na wananchi kwa jumla wanakumbuka jinsi Mkapa alivyonyamazia baadhi ya wajumbe wa NEC “waliotumwa” kushambulia Dk. Salim Ahmed Salim hadi kumuita mwarabu na kumhusisha na mauaji ya rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Ndani ya kikao cha NEC na mbele ya Mkapa, mjumbe Ali Ameir Mohammed alinyanyuka na kutaka Mkapa aruhusu mjadala wa Dk. Salim, tena kinyume cha taratibu.

Kwamba wagombea tayari walikuwa wamemaliza kujieleza; huku kukiwa hakuna aliyejitokeza kuuliza swali na tayari Dk. Salim akiwa nje ya ukumbi, nyuma yake likaibuliwa zogo na shutuma.

Inaelezwa kuwa hata pale baadhi ya wajumbe walipomtaka Mkapa kufuata taratibu, hakutaka kusikiliza. Hata alipoombwa aruhusu Dk. Salim kurudi ndani ya ukumbi na kupewa fursa ya kujibu tuhuma alizoshushiwa, Mkapa aliendelea kuziba masikio.

Hadi anaondoka madarakani, si Mkapa wala CCM waliomsafisha Dk. Salim na tope walililomtwisha. Matokeo yake, dhambi ileile ambayo Mkapa aliruhusu kutwishwa Dk. Salim, leo imemgeukia yeye na wenzake katika chama.

Aidha, ni Mkapa aliyetenda kinyume na maagizo ya NEC katika kupata mgombea urais mwaka 2005. Mkapa aliruhusu kuvunjwa kwa taratibu za kura tatu mtu mmoja.

Vilevile, Mkapa aligomea kutolewa kwa ripoti ya Kamati ya maadili aliyoiunda kufuatilia mienendo ya wagombea. Taarifa zinasema mmoja wa wagombea alitajwa kuongoza kwa kutoa rushwa, kazi ambayo ilikuwa inafanywa na wapambe wake.

Hata pale mmoja wa wajumbe Anna Makinda alipohoji Mkapa: “Ripoti ya Kamati iko wapi?” Mkapa hakuitoa. Aliishia kusema, “majungu matupu.”

Alichotakiwa Mkapa ili kunusuru chama chake na kujenga misingi endelevu, ni kuitoa ripoti kwa wajumbe wa NEC au CC. Kisha wajumbe wakaijadili. Huko ndiko alitakiwa kujenga hoja yake, kwamba wajumbe wa kamati walitenda kazi zao kinyume na misingi iliyowekwa na chama.

Na kwa kuwa yeye ndiye alikuwa na vyombo vya uchunguzi, bado alikuwa na nafasi ya kueleza na kushawishi wajumbe kuwa ripoti aliyopelekewa na vyombo vyake vya usalama inaonyesha kwamba yaliyoandikwa na kamati ya maadili hayana ukweli. Hakufanya hivyo.

Mbali na Mkapa na Mwinyi, mwingine ambaye hawezi kukwepa lawama za kufikisha CCM mahali hapa, ni Rais Kikwete.

Uamuzi wa Kikwete kumteua Lowassa kuwa waziri mkuu wakati ambapo tayari alikataliwa na waasisi wa taifa – Nyerere na Kawawa, kumechangia kuzorotesha serikali na chama chake.

Tatizo kubwa lililopo ndani ya CCM ni kule kuruhusu kuundwa kwa mitandao nje ya mtandao wa chama chenyewe.

Kwa mfano, katika maneo mengi dhambi ya mtandao ndiyo chanzo cha kusakamwa kwa baadhi ya wanachama kama vile, Gachuma, Mwakyembe, Sendeka na wengine wengi ambao wanatajwa kuwa si wanamtandao wa Kikwete.

Ukichukua ya mtandao na kuchanganya na kilichotendeka wakati wa Mwinyi na Mkapa, haraka utabaini kuwa CCM imeondoka na wasisi wake.

Je, hadi hapa nani aweza kujitapa kwamba Kawawa ameondoka na kuiacha CCM bado salama? Bila uwepo wa Kawawa, nani aweza kukemea waliojimbikizia mali na wanaotafuta madaraka hadi kwa kutumia nguvu za giza?

Nje ya Kawawa nani aweza kukemea wanaohatarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar? Nani aweza kusema kuwa hawa “wanatoboa jahazi likiwa limesheni abiria, hivyo adhabu pekee wanayostahili ni kukamatwa na kutoswa?”Aliyesema hayo hayuko nasi tena.

Kuna wenye mawazo tofauti juu ya Kawawa; kwa mfano ujumbe wa simu niliopokea juzi Jumatatu:

“Ni kweli Kawawa kaifanyia nchi hii mengi na katika mazingira magumu ila kamwe hatakumbukwa kwa hayo. Kwa kizazi cha leo, Kawawa hakuwa tofauti na Kingunge (Ngombale Mwiru), wazee waliotokea kuhusudu pesa na ukwapuaji wa mali ya nchi hii uzeeni.

“Wanapotajwa viongozi wakongwe nyuma ya ‘mtandao,’ anakuwamo kwenye listi; wanapotajwa wale walipachika watoto wao kule ambako mshahara ni wa kutosha – BoT anakuwemo vivyo hivyo; wanapotajwa walioingiza watoto wao katika siasa ili kulinda himaya zao dhalimu, anakuwa mmoja wao.

“Alimwogopa Nyerere enzi hizo, ndo maana baada ya kuondoka Nyerere hakuwa na harufu ya uadilifu.”

Inawezekana huyu anamfahamu Kawawa tofauti na wengine? Nani mwingine anasema anamfahamu Kawawa wa zamani na Kawawa wa hadi anatuaga. Karibu tujadili Kawawa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: