Rekodi ya aibu ikulu


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 23 November 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

IKULU ni mahali patakatifu. Lakini rekodi zilizopo sasa zinathibitisha kuona pamegeuzwa “pango la wanyang’anyi.”

Ikulu ni makao na ofisi ya Rais Jakaya Kikwete na ndiyo ofisi ya mkuu wa utumishi nchini yaani Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo. Hivyo, rushwa ikiingia ikulu, walioifungulia milango ni watu hao wawili.

Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, chini ya Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Injinia Ramo Makani, imeonesha ikulu inalea rushwa na ufisadi. Ikulu ilitajwa na mtandao wa WikiLeaks ulipomkariri aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini, akisema Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah alizuiwa na bosi wake kuwashtaki vigogo wa wizi wa fedha za EPA.

Dk. Hoseah ni mteule wa Rais Kikwete, hivyo bosi wake hapa aliyemzuia asifikishe kortini mapapa wa wizi huo na wengineo kama Deep Green, Kagoda, Meremeta ni Rais.

Rais alihusishwa katika sakata la muda mrefu lililohusu uteuzi wa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond/Dowans.

Kwa nini? Kwa sababu mwenyekiti wa vikao vyote vya Baraza la Mawaziri vilivyokataa kampuni zenye sifa na kuidhinisha Richmond ipewe zabuni licha ya kukosa sifa, alikuwa Rais Kikwete mwenyewe.

Halafu, serikali yake ikaidhinisha Dowans inunuliwe na Symbion Power na ikalazimisha Tanesco waingie nayo mkataba.

Ikulu ilitajwa tena lilipoibuka sakata la uwindaji haramu na uuzwaji wa wanyama wapatao 116, akiwemo twiga, na kusafirishwa kwa ndege ya Jeshi la Qatar. Serikali inasema haikuwa na habari, lakini anayetoa kibali ndege za jeshi la nchi nyingine kuingia nchini ni ikulu.

Katikati ya sakata hilo, ikanaswa katika uidhinishaji wa ujenzi wa hoteli za kitalii kwenye mapito ya faru katika Hifadhi ya Ngorongoro. Mwenyekiti wa Bodi ya hifadhi hiyo ni makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pius Msekwa ambaye alidai alipokea maelekezo kutoka juu “mbinguni”.

Kabla kadhia hiyo haijatulia, mtandao wa WikiLeaks ukatonesha kidonda ikulu. Ukimkariri aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini ulisema aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mwaka 2005, Jakaya Kikwete, alihongwa suti tano na mmiliki wa iliyokuwa hoteli ya Zamani Kilimanjaro Kempinski.

Ikulu ikaja juu ikakanusha vikali. CCM ilipata kukanusha kutumia fedha zilizoibwa EPA katika kampeni za mgombea wake wa urais 2005, lakini ilikuwa ni ukanushaji wa lazima tu; ukweli ulibaki palepale kwani baadhi ya makada waliochotewa walithibitisha kupokea na kuelekezwa kwa kupeleka – kwa makatibu wa mikoa wa CCM.

Safari hii ikulu imeumbuliwa tena na ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyowasilishwa wiki iliyopita bungeni kuhusu hatua ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo kuchangisha fedha za kupitisha bajeti ya wizara hiyo.

Luhanjo alimpa kazi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG), Ludovick Utouh ambaye kwa kasi kubwa akamsafisha Jairo, na Luhanjo akamrejesha kazini. Waziri Ngeleja akacheza ngoma kufurahia kumpokea Jairo wizarani.

Bunge limempa Rais Kikwete kazi ya “kizushi”; kuwafukuza wateule wake hao – Jairo, Luhanjo, Utouh, Ngeleja na wakurugenzi wa taasisi zilizochanga fedha wakati wakijua sheria inawakataza.

Ikulu inayotuhumiwa kwa rushwa itamfukuza nani kwa kosa la rushwa?

0658 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet