Richmond bado yamwandama Lowassa


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 16 March 2011

Printer-friendly version
Edward Lowassa

KATIKA kile kinachoitwa “maandalizi ya kuelekea ikulu,” waziri mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya mkataba tata wa Richmond, Edward Lowassa ametungiwa kitabu cha kumsafisha.

Kitabu hicho chenye kurasa 15 kinaitwa, “Roho ya Edward Lowassa ni nyeupe kama theluji.” Mwandishi ni Ruth F. Levis Msuya.

Hata hivyo, kisichoweza kuleta ubishi ni kwamba nywele za Lowassa ndiyo nyeupe na siyo matendo yake, hasa ikizingatiwa nafasi yake katika kashfa ya Richmond.

Kwenye jalada lake, kitabu kimebeba picha ya Lowassa iliyozungushiwa duara na sehemu ya nyuma kuna maneno yanayosomeka, “Lengo kuu la kazi hii ni kuonyesha ukweli juu ya mh. Edward Lowassa kuhusu upendo wake kwa Watanzania.”

Hata hivyo, “kitabu cha Lowassa” hakionyeshi mchapishaji, wala hakina namba ya usajili kutoka maktaba ya taifa.

Naye, Ruth Msuya ambaye amejitambulisha kuwa ni mwalimu, hakuweka maeleo yake fasaha kuonyesha jinsi anavyofahamu Lowassa.

Kinachoonekana ni neno “shukurani” na kuhitimisha kwa kushukuru familia yake kwa kumpa moyo ili aendelee “kusema ukweli daima mpaka mwisho wa maisha yake.”

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja wiki moja tangu gazeti hili kuchapisha taarifa zilizofichua uhamiaji rasmi wa mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo katika mtandao wa Lowassa.

Akiandika kwa Pindi Chana, mbunge wa Viti Maalum (CCM), tarehe 14 Februari mwaka huu, Beatrice alimshawishi Chana kumuunga mkono Lowassa na kumweleza juu ya ulokole wake na “mtumishi aliyepakwa mafuta” kutoka Nigeria.

MwanaHALISI lilipowasiliana na Ruth Msuya kupitia simu yake ya mkononi Na. 0765 366222 ili kujua jinsi alivyomfahamu kwa undani Lowassa, haraka alijibu, “kijitabu kinajieleza.”

Alipobanwa kuwa kitabu hakina maelezo yanayojitosheleza jinsi yeye alivyomfahamu Lowassa, kwanza alisema, “Nakushukuru kwa kupata kitabu” na pili akasema, “…Ninakwenda msibani Morogoro.” Kisha akakata simu.

Katika ukurasa wa nane wa kitabu cha Lowassa mwandishi anasema, “…Tatizo ni kwamba wale wanaomchafua wana wivu mkubwa sana na utendaji uliotukuka. Hii ni sawa na mwanafunzi aliye wa kwanza darasani, wale wanaowania nafasi ile mara nyingi wanajenga uadui na huyo mwanafunzi…” anaeleza.

Mwandishi anasema, “Ukiuliza kisa cha wale wanaomchafua utaambiwa hafai, ukiuliza kwa nini utaambiwa ni tajiri! Inashangaza, kwani kuna mtu aliyekuzuia usifanye kazi,” anahoji.

Katika ukurasa wa tisa wa kitabu hicho, mwandishi anasema Lowassa ni mnyenyekevu na unyenyekevu ni asili yake.

Hata hivyo, mwandishi hajaeleza mahali popote katika kitabu chake kuwa Lowassa alijiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu kwa tuhuma za kuipa kazi kampuni ya Richmond huku akijua kuwa kampuni hiyo haikuwa na uwezo wa kufanya kazi iliyoomba.

Wataalam wa vitabu wanasema kama mwandishi alilenga kumsafisha Lowassa ameshindwa, kwa kuwa maudhui ya kitabu hayana hoja yoyote ya kumjenga.

Wakati hayo yakiendelea, taarifa zinasema kambi ya Lowassa imepanga kila mkakati ili kumzidi kete Rais Kikwete.

Taarifa za ndani ya kambi ya Lowassa zinasema hatua hiyo inalenga kumuimarisha mwanasiasa huyo kati ya sasa na uchaguzi mkuu wa CCM wa mwaka 2012.

Kwa mujibu wa mawasiliano yaliyonaswa ndani ya mtandao wa Lowassa,  “Kamati ya Mkakati” imekubaliana kuwa sasa ni wakati mwafaka kwa Lowassa kujitokeza hadharani na kuzungumzia masuala mazito ya kitaifa.

Masuala ambayo yamekubaliwa Lowassa ayazungumzie, ni pamoja na yale yanayohusu uongozi wa umma ambayo yalistahili kuzungumzwa na rais.

“…Viongozi waandamizi wamekutana mjini Dodoma. Jambo kubwa ilikuwa mkakati makini wa kupata nafasi ya kulikamata Bunge ili kurahisisha mambo yaweze kwenda vizuri na bila upinzani mkubwa kama ilivyokuwa katika Bunge lililopita,” inaeleza sehemu ya mawasiliano ya wajumbe wa kamati hiyo.

Sambamba na mkakati huo, kambi hiyo imeazimia kupata chuo ambacho wanafunzi wake watapatiwa kiasi cha fedha za kujikimu ili muda ukifika Lowassa aalikwe kuhutubia.

Katika kutekeleza mkakati huo, mtandao wa Lowassa umepanga kupeleka kikundi cha waandishi habari kuripoti tukio hilo.

Mkakati huo unafichuliwa katika kipindi ambacho tayari mfululizo wa matukio umeanza kujidhihirisha kuwa Lowassa anapiga hatua kujiimarisha kisiasa kwa ajili ya kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015.

Mtoa taarifa alimnukuu mjumbe wa kamati akisema, hatua ya Lowassa kufanikiwa kupata nafasi ya kuongoza kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama “ni sehemu ya mafanikio” ya mkakati huo.

Anasema, “Tunataka Lowassa kukubalika upya kimataifa ili kurahisisha safari yake ya kuelekea ikulu,” anaeleza mtoa taarifa gazeti hili.

Wajumbe wamekubaliana kuongeza jitihada za kumweka karibu mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama ili apunguze “maumivu na hasira kutokana na kunyimwa nafasi yake ya kuwa naibu spika, baada ya baadhi ya taratibu kupindishwa.”

Hofu ya kundi la Lowassa ni kwamba Jenista anaweza kutekwa na kundi pinzani.

Kwa upande wa naibu spika, mbunge wa Kongwa (CCM), Job Ndugai, mtandao wa Lowassa umepanga “kumfuatilia sana nyendo zake” kwa kuwa anaonekana, “mtu anayeyumba kimsimamo na anatekeleza anayoagizwa kutoka juu kwa malengo maalum. Wanasema Ndugai ni mfuasi wa waziri mmoja mwandamizi” ambaye anatajwa kuwa anaweza kujitosa katika kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi ujao.

Waziri huyo ametajwa kama anayeshika moja ya wizara nyeti na ambayo inamjenga kisiasa na ambaye anaonekana na kundi hilo kama mtu wa karibu na kiongozi mkuu lakini pia kama mpinzani wa kundi lao.

Mkakati wa kundi unakwenda mbali, hata kupanga kutumia vyombo vya habari kwa “gharama yoyote ile” ilimradi ikifika mwisho wa mwaka 2013 hatua nzuri ya kufanyiwa tathmini iwe imefikiwa.

Tathmini hiyo itafanywa kwa kuhusisha taasisi binafsi itakayotoa matokeo bila ya kusukumwa ili kupata sura halisi ya mambo inavyokwenda.

Taarifa zinasema kwamba matukio yote yaliyokwishatokea na kumhusisha Lowassa na mfungamano wake na umma, ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo.

Miongoni mwa matukio yanayotajwa ni lile la Lowassa kuzungumzia harakati zilizofanikiwa kumlazimisha aliyekuwa rais wa Misri, Hosni Mubarak kuachia ngazi baada ya maandamano ya umma yaliyochukua siku 18.

“Kwa kujua watu wengi wanafuatilia na hilo ndilo tukio kubwa kwa wakati ule, Lowassa alitumia fursa hiyo kuonyesha kuwa yupo na wananchi kwa kupongeza wanaharakati na ubaya wa viongozi wa nchi kujilimbikizia mali,” alisema mtoa taarifa wa gazeti hili.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: