Richmond: Kufunga mjadala bungeni ni kukejeli umma


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 03 March 2010

Printer-friendly version

BUNGE la Jamhuri limetishwa. Spika Samwel Sitta “ameng’olewa meno” na kurejeshwa katika “dini” yake ya asili.

Viwango na kasi – Standard and Speed – alivyosema ni mwongozo katika kutenda kazi zake, vimepingwa kikumbo kabla kipindi chake cha ofisi hakijamalizika.

Wiki tatu zilizopita, Sitta alifunga mjadala wa Richmond bungeni kwa kile alichodai “serikali imetekeleza maazimo 21 kati ya 23 yaliyotolewa na bunge.”

Spika alionekana na kusikika akisema maazimio mawili yaliyosalia yamekabidhiwa kwa mamlaka zinazohusika.

Hakuishia hapo. Sitta alionya wabunge kuwa yeyote atakayeibua mjadala huo upya, atamshughulikia kwa mujibu wa kanuni za bunge. Haya yana maana gani?

Sitta amesema serikali imetekeleza maazimio ya bunge 21 kati 23. Siyo kweli. Ni azimio moja tu la bunge ambalo limetekelezwa na serikali ipasavyo.

Azimio lililotekelezwa ni lile lililotaka Wakala wa Usajili wa Leseni za Makampuni na Biashara (BRELA) kuifuta Richmond katika daftari lake la usajili. Mengine yote hayajatekelezwa.

Kwa mfano, serikali ilitakiwa kutotumia mawakala katika kufanya manunuzi ya umma na kuiondoa mamlaka ya manunuzi ya umma (PPRA) katika minyororo ya wizara ya fedha.

Katika taarifa yake bungeni, serikali inasema, “…Marekebisho ya Sheria ya PPRA (sura ya 410) na muswada husika, vitawasilishwa bungeni katika mkutano wa Aprili mwaka huu, kulingana na ratiba ya vikao vya bunge.”

Hapa serikali haijasema kama muswada umepelekwa bungeni. Inasema, “unatarajiwa” kupelekwa. Wala haijasema kwa nini imeshindwa kufanya hivyo miaka mitatu iliyopita.

Je, kule kusema kwamba inatarajia kutekeleza, kunatosha kuaminisha Sitta kuwa serikali imetekeleza? Kuna mangapi ambayo serikali hii imeahidi na ambayo hayajatekelezwa hadi leo, zikiwamo hata hukumu za mahakama.

Azimio jingine ni lile lililotaka serikali kupitia upya mikataba kati ya TANESCO na makampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond/Dowans, IPTL, Songas, Aggreko na Alstom.

Hili nalo halijatekelezwa. Badala yake serikali imekuja na visingizio lukuki, kwamba “kuna mashauri mahakamani yaliyokwamisha utekelezwaji.”

Hapa kuna hoja mbili kubwa. Kwanza, serikali imekiri kutotekeleza kile ilichoagizwa. Pili, imeshindwa kueleza uhusiano kati ya mashauri yaliyopo mahakamani na upitiaji wa mikataba.

Kama kuwapo kwa kesi mahakamani ndiko kulikozuia kupitiwa mikataba, kwanini serikali imekubali kusitisha malipo ya Richmond/Dowans? Je, hatua hiyo haingiliani na kesi iliyopo mahakamani?

Si hivyo tu, ni serikali hiyohiyo iliyositisha uzalishaji wa umeme; iliyoagiza TANESCO kununua umeme wa IPTL – wakati nayo iko mahakamani.

Ni serikali iliyotumia mamilioni ya shilingi kununulia mafuta ya mitambo ya kampuni iliyoshitaki serikali na ambayo mkataba wake unalalamikiwa kutolewa katika mazingira ya rushwa.

Hata maazimio Na. 4, 5, 7 na 9 yaliyotaka serikali kuwajibisha watendaji wa umma waliohusika na mchakato za zabuni, hayakutekelezwa.

Ripoti ya serikali katika ukurasa wa 26 inasema, “…Baada ya serikali kupitia tena tuhuma zilizotolewa na Kamati Teule… imeridhika na maamuzi ya Mamlaka za nidhamu za kuwafutia mashtaka watuhumiwa.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waliofutiwa mashtaka ni Julius Sarota (nishati na madini), Mwita Wagwe (TANESCO), Lutengano Mwakahesya (wakala wa nishati vijijini- REA) na James Mwalilimo (TANESCO).

Azimio Na 8 lililotaka serikali kuwajibisha viongozi wenye dhamana ya kisiasa na kuwachukulia hatua za kinidhamu, halikutendwa kama bunge lilivyoelekeza wala umma ulivyotaka.

Waliokuwa mawaziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, walijiuzulu hata kabla maazimio kutolewa.

Hadi leo hawajafikishwa mahakamani kwa kuisababishia serikali hasara kwa kuipa kazi kampuni isiyokuwa na sifa.

Badala yake, serikali imesema “haijaona jinai iliyotendwa na viongozi hao.” Inasisitiza kuwa vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi wake nje ya nchi.

Je, serikali inahitaji miongo mingapi kukamilisha kazi hii? Mbona Kamati Teule iliweza kukamilisha uchunguzi wake kwa wiki mbili kwa kwenda Marekani na kugundua kuwa Richmond ilikuwa kampuni ya mfukoni?

Je, serikali yenye vyombo vyote vya dola inashindwa nini kufanya hivyo? Kama uchunguzi unaendelea, kwanini Sitta amezimwa, kung’olewa meno na kulazimishwa kufunga mjadala?

Hata azimio Na. 10 halikutekelezwa. Katika azimio hili, bunge lilitaka serikali ichungunze uhalali wa malipo ya dola za Marekani 4,865,000 (karibu Sh. 6 bilioni) yaliyofanywa kwa Richmond/Dowans.

Kwanza serikali, kwa mara ya kwanza, imekiri kuwa kuna malipo yamefanywa kwa Dowans na dada yake Richmond. Mara kadhaa imekuwa ikisisitiza kuwa hakuna hata shilingi iliyotolewa kwa kampuni hiyo.

Pili, serikali imethibitisha kuwa hata gharama za usafirishaji wa mitambo ya kampuni binafsi, zilibebwa kwa fedha za umma.

Tatu, serikali imesema ukweli kwamba kiasi cha dola 30.9 milioni (Sh. 40 bilioni) zimechotwa kinyume cha taratibu kwa kuonyeshwa kuwa zilitumika kugharamia usafirishaji wa mitambo kwa njia ya meli, wakati mitambo imesafirishwa kwa ndege.

Katika kujitetea, serikali inasema madai hayo ya dola za 30.9 milioni yamejumuishwa katika hoja za TANESCO katika shauri lililofunguliwa na Richmond katika mahakama ya kimataifa nchini Ufaransa.

Je, hapa Sitta anapata wapi ujasiri wa kufunga mjadala wakati Bunge limechezewa na Richmond?

Inakuwaje serikali iliyosafirisha mitambo ya kampuni binafsi ifikishwe mahakamani kwa kudai mali yake na Sitta akubali kuziba wabunge midomo?

Jingine ambalo halikutekelezwa ni Azimio Na. 11 ambalo lilitaka serikali ifanyie marekebisho sheria ya maadili ya viongozi wa umma ya mwaka 1995.

Serikali imesema tayari kikundi kazi kimeandaliwa na muswada uko katika ngazi ya makatibu wakuu (IMTC).

Hata hapa haikusema muswada uko tayari mbele ya bunge; imesema “mipango ya kuuandaa imekamilika.” Ni miaka mitatu ya maendelezo ya ngonjera.

Kama hili nalo halijatekelezwa, nani anaweza kujitapa kwamba bunge limefanikiwa kuzima Richmond?

Azimio Na. 13 nalo limepigwa mweleka. Katika azimio hili, bunge lilitaka serikali kulihusisha katika maandalizi yote ya mikataba mikubwa ya kibiashara na hasa ile ya muda mrefu ili kuondokana na kile kilichoitwa “siri” katika mikataba.

Hata hivyo, serikali katika taarifa yake inasema itapeleka kila mkataba bungeni na kuuweka katika “maktaba maalum ya bunge.”

Kinachowekwa hapa ni mkataba, si rasimu ya mkataba. Je, nini faida ya bunge katika hili? Kule kujua kwamba kuna mkataba wa kinyonyaji, lakini ikiwa haina meno ya kubadilisha chochote?

Mbona hata mkataba kati ya serikali na kampuni ya reli ya India (RITES), iliyopewa kuendesha shirika la reli la taifa (TRC) unafahamika, na bunge limeshindwa kuchukua hatua?

Je, bunge lilitaka kuona mikataba inawekwa katika maktaba huku likiwa halina meno kuijadili, au ilitaka kushirikishwa katika hatua zote zikiwamo zile za maandalizi?

Kilichotakiwa na bunge, kwa manufaa ya taifa, ni kuona kila hatua ili hatimaye kuliepusha taifa na hasara inayotokana na mikataba ya kinyonyaji.

Serikali inafika mbali zaidi: Inasema imeunda “Timu ya wataalamu” walewale walioshiriki katika kuigamiza nchi, kujifunza katika mabunge mengine ya Jumuiya ya Madola katika hatua za awali za uandaaji wa mikataba.

Katika kuonyesha “ubutu wa bunge” Spika Sitta anakubali kuundwa kinachoitwa, Kamati ya Masuala ya Biashara itakayopitia mikataba “mikubwa ya kibiashara bila kuathiri taratibu za serikali na zile za mikataba husika.”

Je, bunge linaweza kujigamba kuwa azimio hilo limetekelezwa?

Azimio Na. 14 nalo limekufa kifo cha mende. Serikali ilitakiwa katika azimio hili, kuwajibisha wote waliohusika katika kupitisha mkataba wa Richmond.

Lakini aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali, Johnson Mwanyika na katibu mkuu wa wizara ya nishati na madini, Arthur Mwakapugi wameachia ofisi za umma baada ya kufikisha umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria.

Taarifa zinasema tayari wamelipwa haki zao zote wanazostahili kazini na uwezekano wa kuwachukulia hatua hauonekani.

Hata aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa, bado anaendelea kupeta na kuchukuliwa kama mstaafu wakati yeye anajua vema kuwa hajawahi kustaafu wala kustahili mafao ya wastaafu.

Je, hapa napo Sitta anaweza kusema kuna kitu kimetekelezwa hadi kuapiza na kufunga mjadala?

Angalia Azimio Na. 15 ambalo halikuwa gumu kutekeleza; nalo serikali imegoma kulitekeleza.

Katika hili, serikali iliagizwa na bunge kuachana na utaratibu wa kuteua wakurugenzi na makamishina katika wizara kuwa wajumbe wa bodi za mashirika ya umma kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha misingi ya utawala bora.

Lakini taarifa ya serikali inasisitiza, “bado inaona utaratibu huu uendelee katika baadhi ya bodi ili kusaidia mipango ya serikali.”

Je, nani hapa anasema serikali imetekeleza yaliyoelekezwa na bunge?

Azimio Na. 18 liliagiza serikali kuchukulia hatua za kisheria wamiliki wa Richmond waliofanya udanganyifu na “ujanja wa kuibia serikali.” Hili nalo halikutekelezwa.

Mohammed Gire ambaye ameithibitishia Kamati Teule kuwa ni mmoja wa wabia katika Richmond, bado anapeta uraiani.

Naye Rostam Aziz, ambaye bunge limehusisha na Richmond, bado hajaguswa.

Aliyepelekwa mahakamani na kubebeshwa mzigo wa Richmond, si mmiliki halisi. Ni wakala aliyepewa kazi ya kutafuta waandishi wa habari na maofisa wa serikali kupoza machungu ya kukosekana kwa umeme.

Katika hili, serikali inasema imeunda kamati maalum ya uchunguzi kutafuta wamiliki wa kampuni ya Richmond; hivyo “kazi ya uchunguzi bado inaendelea.”

Je, hatua ya Sitta ya kufunga mjadala ina maanisha kuwa mmiliki wa Richmond ameshapatikana? Maazimio yameshatekelezwa?

Azimio Na. 20 lililosisitiza kuwapo kwa taarifa mbili za uchunguzi na hivyo kutaka Mkurugenzi wa TAKUKURU, Edward Hoseah awajibishwe; nalo limezimwa.

Serikali inasema, “vyombo vya dola vilivyofanya uchunguzi vimebaini kuwa hakukuwa na taarifa mbili za ripoti ya Ricmond.”

Sitta anajua kwamba wakati kinachoitwa uchunguzi kinafanyika, Hoseah hakutoka ofisini. Hivyo, haki haikutendeka.

Je, hatua ya Hoseah kubaki ofisini wakati uchunguzi unaendelea, haikutosha kughairisha ufungaji wa mjadala?

Kilichomfanya Sitta kufunga mjadala si kutekelezwa kwa maazimio ya bunge, bali ni vitisho vya chama chake. Ndani ya bunge, Sitta hakuwa Sitta wa awali.

Wiki moja kabla ya mkutano wa bunge, ni Sitta aliyekaripia Mathias Chikawe, waziri wa sheria na katiba aliyesema “Bunge halina mamlaka ya kusimamia serikali.”

Sitta alisema, tena kwa utulivu, “Chikawe azungumzie hayo bungeni.”

Lakini haikuchukua muda, serikali iliwasilisha taarifa yenye kurasa 30 kwa Kamati ya Nishati na Madini ikipinga bunge kuagiza serikali.

Serikali ilisema, “…Kwa mujibu wa Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 maagizo ya bunge ni ushauri kwa serikali na siyo maagizo.”

Kama bunge haliwezi kusimamia serikali, huku Sitta akikubali mjadala ufungwe, wako wapi wanaojitapa kwamba serikali imetekeleza maagizo ya bunge na hivyo bunge linahitaji kupongezwa?

Hakuna ubishi kwamba bunge limetishwa. Limezibwa mdomo. Sauti za wanaowakilishwa zitapitia wapi?

Mjadala huu utaendelea wiki ijayo: Nini kilisababisha Sitta kufunga mjadala kabla maji hayachemka?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: