Richmond mpya wizara ya nishati


Jacob Daffi's picture

Na Jacob Daffi - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version
KATIBU  Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi anakabiliwa na lundo la tuhuma ikiwa ni pamoja na kilichoitwa kujipa mamlaka ya kuendesha Shirika la Umeme la Taifa (Tanesco), imefahamika.

Aidha, Maswi anatuhumiwa kushinikiza kusimamishwa kazi Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, William Mhando bila kufuata taratibu na kanuni za ajira yake.

Katibu mkuu huyo anatuhumiwa pia kukiuka baadhi ya taratibu, ikiwamo kufanya manunuzi kinyume cha sheria na kuingiza shirika katika mikataba tata.

Taarifa zinasema Maswi ndiye aliyeshinikiza Mhando kusimamishwa kazi kwa maslahi binafsi.

Uchunguzi wa MwanaHALISI unaonyesha kuwa bodi ya wakurugenzi ya Tanesco haikutaka kumfukuza Mhando hadi ipate kwanza baraka za mamlaka ya uteuzi (rais); lakini shinikizo lilitoka kwa Maswi.

Mwenyekiti wa bodi ya shirika hilo, Jenerali Robert Mboma amethibitisha kufanyika maamuzi hayo bila kufuata taratibu.

“Ni kweli, kulikuwa na hoja ya kumsimamisha kazi Mhando, lakini nilisema uamuzi usitangazwe mpaka nimpe taarifa Mhe. Rais Jakaya Kikwete; naye anipe kibali kwa sababu yule ni mteuliwa wake…lakini ndiyo hivyo tena. Ikatangazwa kabla ya Jumatatu ya 16 Julai,” ameeleza.

Lakini kiongozi mmoja ndani ya bodi ya Tanesco ameeleza, “Huyu bwana ndiye amekuwa mtendaji wa Tanesco. Jambo hili na mengine ambayo bado hayajafumuka, yamemuudhi sana mwenyekiti.”

Akitaka kuthibitisha madai hayo, mtoa taarifa amesema Maswi ndiye anahusika na kuipa kazi kampuni ya BP (T) Ltd., ya kusambaza mafuta ya kuzalishia umeme wa IPTL, yenye thamani ya zaidi ya Sh. 28 bilioni.

Taarifa zinasema ni Maswi aliyeagiza BP kuuza mafuta yake kwa Tanesco wakati kampuni hiyo ilienguliwa kwenye zabuni; jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma (PPRA) ya mwaka 2004.

Sakata la Richmond ambalo linaendelea kuitesa serikali, lilitokana na kampuni hiyo kupewa mkataba wa kufua umeme kwa upendeleo baada ya kushindwa kwenye zabuni.

Inadaiwa Maswi alifanya maamuzi kama hayo kwa BP, tena bila kushirikisha Mhando.

Taarifa zinasema pia ni kwa “vitendo vya hatari vya aina hiyo, vya kuingiza shirika katika mgogoro wa kisheria,” Jenerali Mboma ameamua kuripoti kwa Rais Kikwete.

Bali Maswi aliwaambia waandishi wa habari juzi Jumatatu, ofisini kwake, Dar es Salaam kuwa hahusiki na tuhuma hizo kwa vile alipoingia wizarani hapo mchakato huo ulikuwa tayari umeanza.

Lakini alipoulizwa na MwanaHALISI, aligoma kuzungumzia suala hilo, badala yake alitaka mwandishi kwenda ofisini kwake kuchukua taarifa aliyosambaza kwenye vyombo vya habari.

Hata hivyo, nyaraka zilizopo zinathibitisha jinsi Maswi alivyokuwa wakala wa BP, mratibu, msimamizi, mlipaji na mnunuzi wa mafuta hayo yaliyonunuliwa kwa fedha za umma.

“Ndugu yangu, katika mazingira haya, ni nani anayepaswa kuchunguzwa kati ya katibu mkuu wizara ya nishati na madini, Eliakim Maswi na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando,” amehoji mjumbe mmoja wa bodi ya Tanesco.

Taarifa zinamuonyesha Maswi akipokea hati ya kabla ya malipo – Profoma Invoice – iliyoambata na ujumbe wa barua pepe kutoka meneja masoko ya BP (sasa Puma Ltd), Machumani Shebe uliosema, “…itakuwa ni vema zaidi kama utaweza kutupatia nyaraka rasmi za jambo hili kiofisi.”

Anasema, “Naomba tupate barua ya uthibitisho wa malipo kutoka wizarani kwako ili kuwa na uhakika wa malipo. Tunataka pia utupatie LPO (ankara ya malipo) ya kiwango cha mafuta kitakachosambazwa.”

Akiandika kwa njia ya kushukuru, Shebe anasema, “Tunakushukuru kwa kutupatia biashara hii na tunatarajia kusikia kinachoendelea kutoka kwako hivi mapema iwezekanavyo.”

Mara baada ya kupata ujumbe huo kutoka BP, Maswi alimwandikia ujumbe naibu mkurugenzi mtendaji wa Tanesco anayeshughulikia uzalishaji, Boniface Njombe, tarehe 12 Julai 2012 kumwamuru kuandaa malipo hayo haraka iwezekanavyo.

Barua ya Maswi kwenda kwa Njombe, ilinakiliwa kwa Mhando na Decklan Mhaiki, ambaye ni naibu mkurugenzi wa shirika anayeshughulikia usambazaji umeme.

Kwa kasi ya aina yake, siku hiyohiyo ya 12 Julai, Njombe alimwagiza Anetha Chengula wa idara ya uhasibu, kuandaa malipo kwa kile alichoita, “Utekelezaji wa maelekezo ya Maswi.”

“Bila shaka unakumbuka juu ya jambo hili. Tupo wizarani hapa na tumepokea hati malipo kutoka kwa katibu mkuu wa wizara ya nishati na madini iliyotoka Puma (BP) watakaosambaza HFO kwa ajili ya mitambo ya IPTL,” ameeleza Njombe katika barua yake kwa Chengula.

Amesema, “Malipo hayo yatafanywa na wizara ya nishati na madini kama ambavyo tulikubaliana. Hivyo unatakiwa kuandaa malipo ya mafuta hayo haraka kwa msambazaji na unijulishe.”

MwanaHALISI lilipomuuza Mboma kuhusu madai hayo, alikiri kuwa shirika lake halijawahi kuipa kazi kampuni ya BP.

Alisema, “Mimi ninachofahamu ni kwamba TANESCO ina-deal (inashughulika) na makampuni yale matatu yaliyokuwa na sifa. Sifahamu jingine nje ya hapo.”

Mbali na kulazimisha kulipwa fedha hizo, Maswi amedaiwa kuzuia Sh. 36 milioni kutoka Wizara ya Fedha (Hazina) ambazo ni sehemu ya fedha zilizoombwa na Tanesco serikalini.

Tanesco iliomba, tarehe 22 Septemba 2011, Sh. 136 bilioni kwa ajili ya gharama za kuendesha mitambo ya dharura ya umeme. Ilitarajia kuzirejesha baada ya kupata mkopo wake mkubwa wa Sh. 408 bilioni ambazo shirika hilo liliahidiwa.

Akiwa kaimu katibu mkuu wa wizara hiyo, Maswi anadaiwa kukata Sh. 36 bilioni na kuipa Tanesco Sh. 100 bilioni. Inadaiwa alitoa maelezo kuwa kiasi kilichokatwa kitafuta mkopo wa Sh. 20 bilioni katika benki ya CRDB.

Katika barua yake ya 28 Septemba 2011 yenye kumb. Na. AB.88/286/01/15 kwenda kwa mkurugenzi mtendaji wa Tanesco, Maswi anaeleza kuwa kiasi kilichobaki cha Sh. 16 bilioni kingetumika kununulia mafuta mazito kwa mitambo ya IPTL kwa mwezi Oktoba 2011 kutoka Puma/BP.

Mhandisi Mhando alisimamishwa kazi 13 Julai 2012  pamoja na maofisa watatu waandamizi – Naibu Mkurugenzi, Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi Manunuzi, Harun Mattambo kwa kilichoitwa “madai ya matumizi mabaya ya madaraka na ubadhilifu.”

0
Your rating: None Average: 3.9 (11 votes)