Richmond nyingine yaiva


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 24 August 2011

Printer-friendly version
Peter  Noni

SERIKALI iko mbioni kufunga mkataba wa kufua umeme ambao tayari umeonekana utakuwa na utata. Mkataba huo ni kati yake na kampuni ya Karpowership Limited ambayo inamilikiwa na Peter Noni.

Noni ni mmoja wa watuhumiwa wakuu wa wizi wa fedha za umma kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kwa sasa, Noni ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Rasilimali nchini (TIB), ambako Rais Jakaya Kikwete alisema zitahifadhiwa fedha zilizoibwa kwenye akaunti ya EPA ambazo zinarejeshwa kwa mkataba maalum kati ya wezi na serikali.

Wakati fedha hizo zinakwapuliwa BoT, Noni alikuwa mkuu wa idara ya fedha za nje iliyohusika na fedha hizo.

Taarifa zinasema mradi huo kwa sasa uko katika hatua ya majadiliano kati ya serikali, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya Noni – Karpowership Ltd.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo gazeti hili limepata, serikali na kampuni ya Noni wamepanga kufunga mkataba wa kutumia jenereta zinazofungwa kwenye meli eneo la Bandari za Dar es Salaam na Tanga.

Utekelezaji wa mkataba huo umepangwa kuwa kati ya miezi 24 (miaka miwili) na miezi 36 (miaka mitatu) kutegemea makubaliano ya mwisho yatakavyoelekeza.

Kampuni ya Karpowership Limited imeahidi kuzalisha megawati 160 jijini Dar es Salaam na megawati 90 mkoani Tanga.

Msisitizo wa TANESCO katika muda huo unakuja kwa kuzingatia kuwa shirika hilo limelenga utekelezaji wa mkataba huo uendane na muda ambao serikali imeahidi kumaliza tatizo la uhaba mkubwa wa umeme nchini – Desemba mwaka huu.

Utekelezaji wa mkataba huo, hata hivyo, utahusisha pia idhini za matumizi ya miundombinu ya njia ya reli na bandari.

Hii ina maana ya kuwepo mawasiliano ya kina baina ya TANESCO na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kampuni ya reli nchini (TRL).

Taarifa za kuwapo mradi huu zimekuja wiki moja baada ya serikali kufunga mkataba wa kununua jenereta za kuzalisha umeme zenye kutumia mafuta, huku ikishindwa kuendesha mitambo ya umeme ya IPTL iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam.

Kila upande katika mkataba una wajibu wa kufanya mawasiliano hayo kwa ajili ya kufanikisha kupatikana kwa idhini ya kutumia miundombinu ya mashirika hayo mawili ya umma, kulingana na majadiliano yanavyoonesha.

Taarifa zaidi kuhusu majadiliano ya TANESCO na Karpowership Limited zinasema bei halisi ya mradi huo haijaamuliwa kwa kuwa mvutano uliopo katika utaratibu wa malipo ulikuwa haujasawazishwa.

Awali, TANESCO ilikuwa tayari kutoa garantii ya mkopo wa dola 57,290 (kiasi cha Sh. 70 milioni) kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya kuendeshea jenereta hizo za kwenye meli.

Msimamo wa Karpowership Limited ni kupata dola 75,000 (kiasi cha Sh. 90 milioni) kwa ajili ya kukidhi gharama za mafuta na uendeshaji mitambo yake.

Baadaye, pande hizo zilifikia pendekezo kwamba malipo yafanywe kwa kuzingatia kiwango cha kilowati moja senti 26.16 ya dola kwa kufuatia bei ya ununuzi wa mafuta ya dola 690 kwa tani moja.

TANESCO ilitaka kutumia bei hiyo lakini kwa kuzingatia asilimia 75 ya umeme utakaozalishwa Dar es Salaam kwa kutumia jenereta lenye uwezo wa kutoa megawati 100.

Karpowership ilisema itatangulia kuleta jenereta ya megawati 100. Vielelezo vinaonyesha mradi huo utagharamiwa kwa utaratibu wa malipo ya asilimia 75 ya gharama za utunzaji mitambo iwapo Karpowership watalipwa malipo ya awali ya dola 30,000 (kiasi cha Sh. 45 milioni) na kupata garantii ya kukopa dola 75,000 (kiasi cha Sh. 90 milioni).

Iwapo Karpowership watakubaliwa kubadilisha mtambo ndani ya mwaka mmoja, basi malipo yawe asilimia 75; bila TANESCO kuwapa dhamana ya kukopa benki.

TANESCO kwa upande mwingine imetaka ilipe asilimia 75 ya gharama za umeme utakaokuwa unazalishwa kutoka mwanzo wa mkataba hadi Desemba mwaka huu.

Gharama zitabaki hivyo pamoja na Karpowership kuongeza mtambo wa megawati 60 unaopangwa kuwekwa jijini Tanga.

Tatizo linalojitokeza ni kwamba serikali imejiingiza katika mradi ambao utaigharimu fedha nyingi kwa vile tayari ina mzigo wa kugharamia mitambo ya mafuta mazito (IDO) ya IPTL inayonyonya kiasi cha Sh. 40 bilioni kila mwezi.

Mradi huo unaenda sambamba na mradi mwingine wa uzalishaji umeme kwa kutumia mafuta mazito uliosainiwa kati ya serikali na kampuni ya Aggreko. Huu utatekelezwa jijini Mwanza.

Miradi hiyo ni miongoni mwa miradi iliyotajwa na serikali bungeni katika kutafuta ufumbuzi wa haraka wa tatizo kubwa la uhaba wa umeme nchini lililosababishwa na mambo kadhaa ikiwemo upungufu wa maji katika mabwawa ya TANESCO ya Mtera, Kihansi na Pangani.

Katika hatua nyingine, nyaraka zinaonyesha kuwa Karpowership itagharamia ufungaji wa njia kubwa inayosafirisha kilovoti 132 za umeme kutoka kituo cha TANESCO Ilala mpaka bandarini Dar es Salaam.

Noni ambaye aliyewahi kuwa mkurugenzi wa Bodi ya Benki Kuu kabla ya kuteuliwa kuongoza Benki ya Raslimali, anatajwa kumiliki au kuwa na hisa katika kampuni mbalimbali nchini.

Kampuni hizo ni pamoja na HotSpot, Planetel, PEM Ltd na Six Telecom (Tanzania) yenye ubia na kampuni za kimataifa zinazotekeleza mradi wa kuzalisha megawati 100 za umeme kutokana na upepo mkoani Singida.

Mradi wa umeme wa upepo unatekelezwa na kampuni ya Wind East Africa Ltd (WIND EA), chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia iliyotoa mkopo kwao.

Hata hivyo, historia ya utendaji wa shaka kuhusu Noni inadaiwa kuwastua wakuu wa Benki ya Dunia walipokuta jina lake limo miongoni mwa wamiliki hisa katika mradi wa kuzalisha umeme wa upepo – WIND EA ambao walikuwa wakijadili jinsi ya kuupa fedha.

Nyaraka zinaonyesha kuwa washirika wa WIND EA walilazimika kukubali kufanya marekebisho ya mgawanyo wa hisa ili kuiridhisha benki ya dunia na mmoja wa washirika hao aliahidi kusalimisha taarifa zote zinazohusu mamlaka ya Noni katika kampuni.

Kampuni nyingine yenye hisa katika WIND EA inatajwa kuwa ni Kentec ya Denmark yenye hisa asilimia 10.

Kulingana na makubaliano ya maandalizi ya kubuni mradi huo yaliyofikiwa Agosti 2009, Six Telecoms watahodhi asilimia 45 ya hisa, Kentec asilimia 5 na Aldwych International ya Uingereza hisa 50 katika WIND EA.

Washirika wa Noni katika umiliki wa Six Telecom wanatajwa kuwa ni pamoja na Rashid Shamte. Nyaraka zinaonyesha kuwa Noni anamiliki pia mashamba yaliyoko Kabuku, Korogwe na Handeni, mkoani Tanga kupitia PEM Ltd.

Kampuni ya Aldwych inafungamana na matajiri wenye biashara Afrika Kusini, Uholanzi na Mauritius.

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)