Richmond yaibabua serikali


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version
Mhe. Edward Lowassa, mtuhumiwa kashfa ya Richmond

RIPOTI ya serikali kuhusu Richmond ni "chafu" na huenda isiwasilishwe mbele ya bunge zima, imefahamika.

Taarifa zinasema ripoti ya serikali haikidhi matarajio ya wabunge; imeonyesha udhaifu wa serikali na kwamba kuiwasilisha kwa mjadala itakuwa ni kuaibisha zaidi serikali.

Lakini taarifa za baadaye zilisema juzi kuwa kama itawasilishwa, basi itakuwa mwishoni mwa mkutano wa sasa wa bunge na ikiwa “imefanyiwa marekebisho makubwa.”

“Taarifa hii ni chafu. Inaonyesha kutetea watuhumiwa wote wa ufisadi katika Richmond. Kupokea ripoti hii na kuijadili kutaaibisha bunge na serikali,” ameeleza mmoja wa wajumbe wa kamati ya uongozi.

Wiki iliyopita, serikali iliwasilisha rasmi ripoti yake ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya Richmond katika Kamati ya Nishati na Madini.

Baada ya kikao cha Kamati, mwenyekiti wake William Shelukindo aliwaambia waandishi wa habari, “Tumepokea taarifa ya serikali. Tunaipitia. Kama kutakuwa na chochote cha kusema, tutasemea bungeni.”

Hata hivyo, taarifa ambazo MwanaHALISI limezipata wakati tukienda mitamboni zimedai kwamba, Kamati ya Uongozi ya Bunge imeagiza serikali kuifanyia marekebisho ripoti hiyo.

Maazimio ya bunge yanatokana na uchunguzi wa kamati yake teule juu ya mkataba kati ya serikali na kampuni ya uzalishaji umeme wa dharura ya Richmond Development Corporation LLC ya Marekani.

Kamati ya Bunge ya Richmond, iliongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, na matokeo ya uchunguzi wake ndiyo yalisababisha kujiuzulu kwa mawaziri watatu wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete akiwamo aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa.

Wengine ni Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha. Wawili hawa walikuwa mawaziri wa Nishati na Madini kwa nyakati tofauti.

Lowassa, Karamagi na Msabaha, walituhumiwa kutoa upendeleo kwa Richmond ambayo haikuwa na sifa, uwezo wala hadhi ya kupata mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura.

Kampuni ya Richmond ilishindwa kuagiza mitambo ya umeme na hatimaye kugawa mkataba wake kwa kampuni ya Dowans.

MwanaHALISI limeambiwa na vyanzo vyake vya kuaminika kwamba, pamoja na mambo mengine, taarifa ya serikali “imewasafisha” watuhumiwa wa Richmond.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, ripoti ya serikali bado haikutaja hata ofisa mmoja wa serikali kama ametenda kosa katika kuipa zabuni Richmond.

Kitendo cha kuandaa ripoti ya serikali ambayo haikumbana ofisa yeyote wa ngazi ya juu kuhusika na uzembe wa kutoa zabuni kwa kampuni ya kitapeli, kimeudhi wabunge na baadhi ya viongozi serikalini.

“Sasa tumefika mbali. Ripoti inatetea hata waliohusika moja kwa moja na utapeli huu? Inatetea mafisadi? Hii haikubaliki,” amesema mmoja wa wabunge aliyekuwa katika Kamati ya Mwakyembe.

Kuna taarifa kwamba Waziri Mkuu Mizengo Pinda “ameagizwa” kutopeleka ripoti hiyo bungeni kwa hofu kwamba itaiumbua serikali.

Ingawa mtoa taarifa hakueleza Pinda ameagizwa na nani, taarifa zinasema ilikuwa baada ya mashauriano na rais.

Sehemu ya taarifa ya serikali imesomeka, hata hivyo, kuwa serikali inaridhika na hatua ambazo tayari imechukua katika suala la Richmond.

Sakata la Richmond ndilo kiini cha minyukano ya muda mrefu bungeni na hata kusabisha Kamati Kuu ya CCM kuunda kamati ya kuchunguza kiini cha migogoro kati ya bunge na serikali.

Kamati hiyo ilikuwa chini ya rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi. Wajumbe wengine wa kamati ni Abdulrahman Kinana na Pius Msekwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: