Richmond: Yaliofanyika hayatoshi


Chacha Kisiri's picture

Na Chacha Kisiri - Imechapwa 29 July 2008

Printer-friendly version
Richmond

KATIKA siku chache zilizopita, serikali ilitamka kwamba imevunja mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura kati yake na kampuni ya Dowans Holdings S.A iliyorithi mkataba huo kutoka kwa Richmond Development Company (LLC).

Kwa mujibu wa tangazo la serikali lililotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme la Taifa (TANESCO), Dk. Idrissa Rashid, mkataba huo unatarajiwa kuvunjwa rasmi Septemba mwaka huu.

Miaka miwili imepita tangu serikali ilipoikabidhi Richmond kazi hiyo, huku ikijua kuwa kampuni hiyo haina sifa wala uwezo wa kuzalisha umeme.

Katika nusu ya kipindi hicho, mkataba huo ulihamishwa kutoka kwa Richmond kwenda kwa Dowans.

Kwa viwango vyovyote vile, hiki ni kipindi kirefu mno. Watanzania hawana sababu ya kubweteka kutokana na kauli hii ya serikali. Hapa serikali inataka kuwapofusha Watanzania wasahau ukiukwaji wa taratibu uliofanywa wakati wa kuingiza mkataba huo.

Kutokana na uchunguzi uliofanywa na kamati teule ya Bunge, wananchi tulipata fursa ya kujua mengi kuhusu kampuni hiyo; kwamba ilishinda bila kuwa na uwezo, yaani ilipendelewa na wakubwa. Haikuwa na uwezo wa kifundi na wa kifedha.

Ni kampuni ambayo haikuwa imesajiliwa kihalali, Marekani na hapa Tanzania. Kwa kauli ya Dk. Harrison Mwakyembe, aliyeongoza kamati ya Bunge, kampuni isiyo na uwezo hata wa kuweka balbu, ndiyo ilikabidhiwa jukumu zito kama hilo wakati taifa likuwa katika hatari ya kuingia gizani.

Ni wazi hapa kulikuwa na nia mbaya nyuma ya mradi huu, kwani watawala walitanguliza shida zao badala ya shida za wananchi. Hatuwezi kulisahau hili, na hatuna sababu ya kubweteka sasa eti kwa kuwa serikali imetoa tamko la kuvunja mkataba huo.

Katika kipindi hicho cha miaka miwili, mabilioni ya pesa za wananchi (zaidi ya bilioni 110) zimechukuliwa na kampuni hii feki. Hapa ndipo umakini wa serikali unapotiliwa shaka kubwa.

Ni lazima pesa hizi zirudi kwenye hazina ya taifa, kama serikali inataka tuone imefanya la maana. Mahitaji ya taifa ni makubwa mno katika afya, elimu, miundombinu na kadhalika.

Pesa hizo ziingizwe katika hazina ya taifa zisaidie kutoa huduma za msingi tunazohitaji. Hatuwezi kuziacha zimilikiwe na matapeli, tena kwa idhini ya serikali.

Zaidi ya hayo, serikali inapaswa kuchukua hatua kali zaidi kwa kuwawajibisha wahusika, akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushindwa kutumia elimu na mamlaka yake kuzuia wizi huu kabla mkataba haujakubaliwa na kusainiwa.

Kama Mwanasheria Mkuu angekuwa makini, labda angeweza kusitisha uhuni huu na kuokoa raslimali za taifa. Hata hivyo, inawezekana naye aliingizwa katika kundi lile lile la wanasiasa waliokuwa nyuma ya mradi huo.

Vinginevyo, Watanzania wana haki ya kusema kuwa mwanasheria mkuu naye hana sifa za kuwa katika wadhifa alionao. Si hilo tu, bali wana haki ya kuona kuwa hata rais aliyemteua si kiongozi makini; vinginevyo angekuwa amemwajibisha baada ya uchunguzi uliofanywa na kamati ya Bunge.

Kwa hiyo, ingawa uamuzi wa serikali kuvunja mkataba unaweza kuwa sehemu ya utekelezaji wa maoni ya Bunge, serikali bado haijaonyesha umakini katika kulishughulikia suala hili.

Kama ingekuwa inaona uchungu kama tunaouona sisi, ingepigania pesa hizo kurejeshwa na pia ingewafukuza kazi wahusika, hasa Mwanasheria Mkuu wa serikali na kuteua mwingine.

Mwanasheria Mkuu alishindwa kubaini ubabaishaji, hivyo alishindwa kuishauri serikali kuachana na mkataba huo.

Kushindwa kwa ofisi yake kugundua tofauti za kisheria kati ya Richmond Development Company LLC, RDEVCO na RDC, majina ambayo wamiliki wa Richmond Development Company (LLC) walikuwa wanayatumia kwa kubadili badili kwa makusudi, ni uzembe usiosameheka.

Lazima awajibike. Kama angewajibishwa, hilo lingekuwa funzo kuu kwa wengine, na lingeleta imani ya Watanzania kwa serikali.

Kwa kadiri mambo yalivyo leo, serikali ilishirikiana na kampuni feki kuwanyonya wananchi, ndiyo maana inashindwa kuchukua hatua muhimu, inabaki kutoa matamko ya kisiasa.

Yupo pia Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuchunguza na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU). Kama ofisi yake ingetimiza wajibu wake, haya yote yasingetokea.

Licha ya kushindwa kuyagundua mapema, ofisi yake pia ilishiriki kuisafisha Richmond na washirika wake, pale wananchi walipoanza kuhoji mkataba huu kupitia bungeni.

Kama TAKUKURU ingefanya uchunguzi makini na kutoa taarifa ya kweli, inawezekana mkataba huu ungevunjwa kabla ya mwaka mmoja, na kusingekuwa na haja ya kuunda kamati ya Bunge.

Kwa hiyo, madhara makubwa kiuchumi yaliyosababishwa na mkataba huu, ni aibu kubwa kitaifa na kimataifa ambayo serikali yetu imepata, yamechangiwa na watendaji wazembe na wababaishaji wakiwamo hao wa TAKUKURU.

Hata hivyo, inaonekana serikali haina nia ya kukomesha wizi huu, maana katika siku chache zilizopita tumeshuhusia ikishiriki kwa njia za hila - na kupitia Chama Cha Mapinduzi - kuwasafisha baadhi ya viongozi walioshiriki moja kwa moja katika mchakato wa mkataba huu wa aibu.

Tungetarajia serikali itusaidie kuwabana zaidi mawaziri waliojiuzulu kwa tuhumu na kuhusishwa na Richmond, ili watueleze mengine wanayojua kuhusu kampuni hizi, na wataje washirika wao au waliowatuma na kuwaagiza waipe Richmond mradi huo.

Lakini serikali imejua kwamba ikiwabana sana viongozi hawa, wakianza kutaja na kutajana, yataibuka makubwa ambayo yatawagusa hata wakubwa wengine tusiowadhania - wakubwa wale wale ambao kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe walilindwa ili kulinda heshima ya serikali.

Ingawa hoja ya Dk. Mwakyembe imeibua maswali mengine, kwamba kama waziri mkuu alihusishwa na akalazimisha kuachia madaraka, hao waliobaki juu ya waziri mkuu ni kina nani? Ni makamu wa rais au rais mwenyewe?

Kama kwa kumfukuza waziri mkuu serikali haijapata msukosuko wa kutosha, ni nani huyo ambaye kama angetajwa serikali ingedhalilika zaidi?

Hali hii ndiyo inatufanya tuone kuwa nyuma ya Richmond wako wakubwa zaidi, na hawa ndio waliwapa jeuri mwanasheria mkuu na mkurugenzi wa TAKUKURU.

Kwa hiyo, uzembe wa ofisi hizi za umma, unaendekezwa na serikali kwa kuwa serikali yenyewe ndiyo imehusika katika uchafu huu. Hata hivyo, hilo halitawazuia wananchi kudai hatua makini zichukuliwe dhidi ya waliohusika, napesa zetu zirejeshwe.

Na si hayo ya Richmond tu, bali yapo pia ya makampuni mengine kama vile IPTL, AGGREKO, SONGAS, ALSTOM, na KIWIRA ambayo yanaendelea kuikamua TANESCO mapato yake na kusababisha gharama kubwa za umeme.

Kwa mfano, inasemekana SONGAS inalipwa Sh. milioni 244 wakati Richmond/Dowans inalipwa Sh. milioni 152 - kwa siku moja!

Watanzania wanachotaka ni kwamba mikataba yote ya wizi ivunjwe. Tusidanganywe tu kwa mkataba mmoja wa Richmond.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: