Ridhiwani ‘awapa’ ulaji marafiki


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version
Ridhiwani Kikwete

MARAFIKI sita wa Ridhiwani Kikwete, yule mtoto wa rais, wameteuliwa kuwa wakuu wa wilaya (ma-DC), MwanaHALISI limeambiwa.

Wanaotajwa kuwa marafiki wa Ridhiwani na wameteuliwa kuwa ma-DC ni pamoja na Ulega Abdallah aliyepelekwa Kilwa, mkoani Lindi; na Paul Mzindakaya aliyepelekwa wilaya mpya ya Busega, Mwanza.

Wengine ni Mrisho Gambo (Korogwe), Elibariki Kingu (Kisarawe), Anthony Mtaka (Mvomero) na Hassan Masala (Kilombero).

Wachambuzi wa mambo ya siasa wanasema uteuzi huo unaweza kuwa sehemu ya mpango maalumu wa CCM kuandaa safu yake katika mbio za uchaguzi kuelekea 2015.

Mtoa taarifa ambaye ameomba jina lake lisitajwe gazetini, alisema juzi Jumatatu, “Hapo kuna mtu mmoja tu aliyeachwa katika kundi hilo; ni Anthony Peter Mavunde.

“Huyu hawamwelewi. Mara yuko kwa Ridhiwani, mara kambi ya Benno Malisa; na unajua Benno na Ridhiwani bado hawaelewani vizuri,” alisema mtoa habari.

Malisa ni kaimu mwenyekiti wa UV-CCM; Ulega mwenyekiti wa umoja huo mkoa wa Pwani; Mzindakaya mwenyekiti Rukwa; Masala mwenyekiti Lindi, na Gambo, Kingu na Mtaka ni wajumbe wa Baraza Kuu la UV-CCM.

Ulega ndiye kiongozi wa UV-CCM aliyepata kutoa tamko la mkoa kwamba “…rais ajaye wa Tanzania, hatatoka Kaskazini.”

Wachambuzi wanaona kuteuliwa kwake kuna maana kwamba uongozi wa juu wa chama na serikali, unaunga mkono tamko hilo.

Kwa upande wa Mzindakaya, ambaye ni mtoto wa kada maarufu wa CCM na mbunge wa zamani wa Kwela, Chrisant Mzindakaya, uteuzi wake unachukuliwa kuwa ni kuendeleza urafiki.

Hata hivyo, kuna malalamiko kuhusu wabunge viti maalum kupewa u-DC “…wakati kuna watu waliosotea chama kwa muda mrefu na ambao wameachwa,” zimeeleza taarifa.

Wakuu wa wilaya ambao ni wabunge wa viti maalum ni Lucy Mayenga (Uyui), Subira Mgalu (Muheza), Martha Umbulla (Kongwa), Rosemary Kirigini (Meatu) na Agnes Hokororo (Ruangwa).

Mayenga kwao ni Shinyanga, Mgalu anatoka Pwani, Umbulla (Manyara), Kirigini (Mara) na Hokororo (Mtwara).

Taarifa zinasema kuna orodha ndefu ya vijana ambao walitarajia kuwa ma-DC lakini hawakuteuliwa.

Miongoni mwao ni Marwa Mathayo (Mara), Jonas Nkya (Morogoro), Fadhili Ngajiro (Iringa) na Robert Kamoga (Tabora) ambao wametajwa kutoiva na Ridhiwani.

Wamo pia mwenyekiti wa sasa wa UV-CCM taifa, Benno Malisa, mkuu wa Wilaya ya Chemba (Dodoma) Francis Isaac; Said Sambara na Hussein Bashe aliyewahi kutuhumiwa kutokuwa raia. Hata hao wanadaiwa kutoiva na Ridhiwani.

Mwingine aliyetajwa ni Katibu Mkuu UV-CCM, Martine Shigella ambaye mbele ya hadhara hutamba kwamba “…ndani ya UV-CCM hakuna matatizo.”

Hata hivyo, Malisa anayekwepa kuzungumzia wimbi hilo, anasema anayepaswa hasa kufanya hivyo ni Shigella ambaye anawabeza wote waliohama CCM kuwa wamejivua gamba.

Lakini, Ngajiro anaonya mara moja, “…kuhama kwa Millya (James ole) kusibezwe. Unajua anapoondoka mtu kama yule anahama na watu, sasa lazima watu wakae chini kufikiria namna ya kujenga chama. Kuondoka kwake ni pigo.”

Mwenyekiti mwingine wa mkoa aliyezungumza na gazeti hili anasema, “Ridhiwani ni tatizo kaka. Kuna kukandamizana na Ridhiwani  ndiye anayesababisha yote haya.”

“Ninyi wenyewe mmeandika kwamba Millya alilalamikia ikulu kutotoa karipio la kauli ya vijana wa mkoa wa Pwani.

“Hilo jambo lilimpa jibu Millya kwamba ikulu inahusika kwa namna moja au nyingine. Katika kikao cha Baraza la Vijana Pwani inadaiwa Ridhiwani alikuwamo.

Taarifa ambazo gazeti hili limeambiwa ni kuwa Ridhiwani “hajaacha kuwa na makundi” hasa kwa mtu anayetofautiana naye kimawazo kuendeleza chama hicho kikongwe.

“Vijana wanaona wananyimwa fursa ambayo sasa wanaisaka kupitia upinzani,” anasema mwenyekiti huyo na kuongeza, “Yaani ukikosana na Ridhiwani utatuhumiwa kuwa ni fisadi.”

Naye Ridhiwani alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo, simu yake iliita bila kupokelewa. Alipopelekewa ujumbe mfupi (sms), alijibu haraka akisema, “Waulize hao wenyeviti kaka.”

Ridhiwani alikuwa ameulizwa, “Kuna tuhuma kwamba umekorofishana na wenyeviti wa UV-CCM wa mikoa ipatayo 10…tunataka utoe kauli yako.”

Sasa hata wimbi la wanachama, hususan vijana kuihama CCM kwenda upinzani, kunadaiwa kusababishwa na kile kinachoitwa “kuvunjika kwa matumaini kwa vijana wengi.”

Mmoja wa viongozi ambaye alihama mapema na kuhama kwake kumetikisa chama, ni aliyekuwa Mwenyekiti wa UV-CCM mkoa wa Arusha, James ole Millya aliyejiunga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hivi karibuni.

Mtoa habari wa gazeti hili anasema kuwa hata kitendo cha kuenguliwa kuwania ubunge wa Afrika Mashariki mwaka huu, kwa hoja kuwa amepewa karipio na chama, kimetafsiriwa kuwa ni uonevu.

“Kama onyo, mbona kuna mgombea alikuwa na onyo kama la Millya na akapitishwa. Iweje kwa Millya? Wamasai wanaona kuwa hawana fursa ndani ya CCM,” alisisitiza.

“Ndiyo maana wanahama. Wanakwenda CHADEMA. Chama chenye kutoa fursa, chenye matumaini kwa vijana. Ushahidi uko wazi,” amesema.

Millya alisema hivi karibuni kwamba CCM imefilisika kimawazo na haitoi matumaini kwa Watanzania kwa kuwa imekosa demokrasia na kupuuza maoni na mawazo ya wadau wengine.

Alidai ya kuwa Ridhiwani hakuanza sasa kuhusika “kufinyanga mawazo ya vijana,” wengine akiwamo Hamad Yussuf Masauni ambaye alijiuzulu kwa sababu za umri wake kupita.

Kuondoka kwa Millya kunaelezwa kuwa ni mwendelezo baada ya kuondoka kwa aliyekuwa mwenyekiti wa umoja huo, Hamad Yussuf Masauni, mbunge wa Kikwajuni, Zanzibar.

Masauni alipoulizwa kuhusu hali katika umoja wa vijana alisema, “Hizi ni changamoto tu. Kama kuna chama ambacho hakina changamoto hilo ni tatizo. Ukiniuliza mimi kuhusu CCM naona ni chama bora kwa msingi wake, historia, sera na ilani.”

Inadaiwa kuwa mgogoro kati ya Ridhiwani na makada wenzake ulianza mara baada ya baraza kuu la vijana kumteua Bashe, anayeelezwa kuwa mfuasi wa karibu wa Mbunge wa Monduli Edward Lowassa, kuwa mwenyekiti wa kamati ya kutafuta mpasuko ndani ya umoja huo.

Aidha, hatua ya Shigella kuridhia baadhi ya vijana kutoa kauli, tena nje ya vikao, kuituhumu serikali ya baba yake na CCM, inatajwa kuwa ni kiini kingine cha mivutano kati ya Ridhwani na kigogo huyo.

“Shigella na Benno hawataki kumtumikia Ridhiwani, badala yake kukitumikia chama. Kuona hivyo, Ridhiwani na kundi lake wakaamua kutafuta njia ya mkato kuvunja uongozi wa sasa wa UV-CCM,” ameeleza mtoa taarifa.

Pia alisema wanachama wengi watajiweka kando kwa sababu ya mfumo mbovu wa uendeshaji wa chama hicho ikidaiwa kuwa “kama huna fedha, huna nafasi ya kushiriki uchaguzi wala huwezi kushinda…mfumo huu hauvutii vijana; CHADEMA inawavutia, wanakwenda huko.”

Amesema kwamba CCM haina budi kubadilika kwa sasa. Badala ya kujadili watu ijikite kwenye kujadili na kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya watu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: