Ridhiwani ametumwa kuvuruga CCM?


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 16 March 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Ridhiwani Kikwete

MKUTANO wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UV-CCM) mkoa wa Pwani umefanyika mjini Bagamoyo na kuibuka na matamko mazito yanayozua maswali mengi kuliko majibu.

Kwa kauli moja, Baraza la Vijana limeazimia sekretariati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iwajibike kwa kushindwa kumshauri mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete namna nzuri ya kuendesha chama.

Kwamba mawaziri wakuu wastaafu wafunge midomo yao vinginevyo watalazimishwa kufanya hivyo na chama kinachowatunza kwa fedha nyingi!

Kwamba gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndullu awajibike kwa kueleza na kufafanua hali ya uchumi badala ya kumwachia Rais Kikwete kujieleza mbele ya umma.

Akisoma tamko la Baraza la Vijana, Makamu Mwenyekiti wa UV-CCM, mkoani Pwani, Abdalah Ulega aliwashambulia baadhi ya viongozi wastaafu kwa kusema, “Kama wanataka urais wasubiri muda wachukue fomu na kuwashawishi wajumbe wawachague.

“Lakini kwa kumtukana mwenyekiti hawatapata kamwe kwa kuwa yeye ndiye anayejua ni nani muadilifu, hivyo wasiharibu nchi kwa maslahi yao. Wao wameshiba na sasa wamevimbiwa watuache na sisi tule kama wao.”

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano wa Baraza la Vijana, ni Dk. Shukuru Kawambwa waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi na mjumbe wa Baraza Kuu la UV-CCM taifa, baadhi ya wabunge wa CCM na Ridhiwani Kikwete.

Kwa tuliobahatika kunyatia habari kutoka kikao cha Bagamoyo, tunalazimika kusema kuwa wapo watu waliopandikizwa kuvuruga chama baada ya kufanikiwa kufanya kazi hiyo katika dola.

Maneno aliyoyasema ni ushahidi tosha, kwamba Ulega ametumika kuivuruga UV-CCM, serikali na chama chenyewe.

Katika hali ya kawaida, huwezi kutegemea makamu mwenyekiti wa UV-CCM, tena katika mkoa akisimama hadharani kuwatuhumu na kuwakemea viongozi wastaafu kana kwamba walichokifanya ni uhaini.

Kwanza inashangaza kuona, njia aliyoitumia Ulega na wenzake ni njia ile ile ambao wazee wale waliitumia ya kutoa maoni yao kwa kudhani chama chao kitawasikiliza ili kuchukua hatua muafaka ya kunusuru hali ya mabo inayokwenda mrama kila kukicha.

Jambo jingine linalotisha katika hotuba ya Ulega ni pale wanapodai kuwa wastaafu wanaotoa maoni yao kuhusu kasoro za chama chao, wanafanya hivyo kwa sababu ya agenda ya urais wa mwaka 2015. Na kwamba kama hiyo ndiyo agenda yao, “wamechelewa” maana ni rais Kikwete tu anayejua rais wa mwaka 2015.

Haya ni maneno mazito lakini pia ya ajabu kwa sababu urais wa taifa hili si uchifu wala urithi wa shamba la bibi. Urais ni taasisi na ni rukra kuizungumzia kwa yeyote hata kama watakuwapo wasiopenda hilo kufanyika.

Hata kama Kikwete mwenyewe aliwahi kusema urais ni suala la familia na kwamba urasi wake hauna ubia na mtu yeyote, hilo ni suala lisilokubalika kuwa rais wa 2015 anayemjua ni Kikwete peke yake. Je, Ridhiwani na Ulega wamepata wapi jeuri ya kutamka maneno haya?

Lakini kuna hili pia. Kumbe suala zima na minyukano inayoendelea ndani ya chama inahusu kula kwa zamu. Sasa ni zamu ya mkoa wa Pwani na kipekee mji wa Bagamoyo! Mwingine akilipuka akasema ni zamu ya kabila fulani, dini fulani, kundi fulani, atakuwa amekosea?

Mkorogano huu ndani ya chama unazidi kukua na kuchukua sura mpya kila uchao. Kwa kuwa CCM ni taasisi, mikorogano ni jambo linalotazamiwa. Lakini hata hivyo, iko mikorogano mingine ni vigumu kuielewa hasa pale inapochukua sura ya familia kuvuruga taasisi.

Huko nyuma tumekuwa tunasikia watu mbalimbali wakiteta na wengine kupika majungu, juu ya tabia ya familia ya Rais Jakaya kuingilia masuala ya dola. Manung’uniko yalichukua sura mpya baada rais mwenyewe kuamua kumpatia kijana wake Ridhiwani Kikwete jukumu la kutembeza fomu ya udhamini wakati anagombea urais ndani ya chama chake.

Baadaye alipoulizwa ni kwa nini alifanya hivyo. Akasema, akasema kugombea ni suala la familia. Ikafuata ajabu pale mke wa rais Mama Salma Kikwete alipoanza kutumia raslimali za serikali kuzunguka nchi nzima kunadi mgombea urais ambaye ni mme wake. Kelele zilipopigwa, inadaiwa uchakachuaji wa risiti ulifanyika ili kuficha ukweli.

Hata hivyo, tayari chama kilikuwa kimepata sura mbaya mbele ya wapiga kura. Haikuishia hapo, mtoto mwingine wa Rais, aitwaye Miraji Kikwete ilidaiwa kukabidhiwa ofisi ya fedha na mikakati iliyokodishwa maalum katika mtaa wa Undali.

Kwa kuwa hii ilikuwa ni kinyume na taratibu za chama chetu, wenye hekima wakapisha ili familia iendeshe kampeni. Matokeo ya hatua hizi wote tunajua kwamba kinachodaiwa kuwa ni kushindwa kwa chama, kunaweza kuwa ni kushindwa kwa familia kuendesha kampeni.

Kwa jinsi sasa mambo yanavyokwenda, familia ya rais ikiongozwa na Ridhiwani inataka kuwaangushia watu wengine zigo hili wengine.

Siyo siri kuwa tangu Kikwete aingie madarakani, chama hiki kimeingia katika enzi mpya. Vitendo vya kibaguzi vilivyoasisiwa na kundi la wanamtandao, uliomwingiza yeye na maswahiba zake madarakani, sasa vimemgeuka na kuanza kumtafuna mwenyewe.

Hata kizunguzungu kinachomzonga sasa hadi kushindwa kuchukua hatua madhubuti katika kurejesha nidhamu katika chama na serikali, kinatokana kwa sehemu kubwa na serikali yake kugeuka kuwa ya washikaji.

Bahati njema wengi wanafahamu kinachotendeka nyuma ya kauli hizi. Kwamba ni vita ya urais wa mwaka 2015. Sasa mbona wameanza mapema kiasi hiki? Katika hali hii, chama kitaweza kupona kweli?

Je, kundi hilo linaloanza kuwatuhumu wastaafu kuwa wamekula na kushiba na hata kuvimbiwa, wanaweza kweli kujilinganisha na wao katika hili la kula na kuvimbiwa?

Tulio karibu na watu hawa tunajua kuwa baadhi yao tayari wamekula la kuvimbiwa kupita kiasi na wanachotafuta sasa labda ni kutaka hisani kwa wanayemuona ataendelea kuwakumbatia.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: