Ridhiwani Kikwete mdaiwa sugu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 01 February 2012

Printer-friendly version

WATOTO wawili wa Rais Jakaya Kikwete ni miongoni mwa wahitimu wa vyuo vikuu waliotangazwa kama wadaiwa sugu wa mkopo wa elimu ya juu uliotolewa vipindi tofauti kati ya mwaka 1994 na 2009 katika vyuo mbalimbali nchini.

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) wiki iliyopita ilitangaza majina ya wadaiwa sugu kwenye tovuti yake www.heslb.go.tz baada ya kuona wengi wa waliokopeshwa hawajarejesha hata shilingi.

Kulingana na taarifa yake, Bodi imeagiza wadaiwa hao wanaokadiriwa kufikia 80,000 wajisalimishe ndani ya siku 21, si hivyo watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwamo kuwazuia kusafiri nje ya nchi.

Watoto wa Rais Kikwete ambao majina yao yamekutwa katika tovuti ya bodi hiyo ni Ridhiwan J. Kikwete aliyehitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Salama Kikwete aliyehitimu katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHACS).

Inasemekana Salama ni mke wa Ridhiwan.

Mbali na hao, orodha ya wadaiwa sugu inaonesha wamo watoto wengine wa wanasiasa mbalimbali, wanasiasa wenyewe pamoja na watoto wa viongozi waandamizi serikalini wakiwemo waliokwishastaafu kazi katika utumishi wa umma.

Wengine wanaosakwa na bodi hiyo ambao majina yao yamehusishwa na majina ya wanasiasa au watumishi maarufu wa umma, ni Alfred J. Nchimbi anayedhaniwa kuwa kaka wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Emmanuel Nchimbi na Anna Rajab Kiravu anayehusishwa na Rajab Kiravu, aliyestaafu kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC).

Wadaiwa wengine wa mikopo ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ni Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Christina Lissu na Afisa Mwandamizi Idara ya Sera na Utafiti wa Chama hicho, Mwikwabe Mwita.

Katika orodha hiyo pia yamo majina ya Raphael Augustine Mrema anayehusishwa na Augustine Mrema ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) na Charles J. Warioba anayehusishwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba.

Pia wameonekana Baraka Hamis Msumi anayedhaniwa ni mtoto wa aliyekuwa Jaji Kiongozi, Hamis Msumi ambaye ameshastaafu, na Judith D. Mwakyusa ambaye anadhaniwa kutoka familia ya Profesa David Mwakyusa aliyekuwa Waziri wa Afya kipindi kilichopita na mbunge wa Rungwe Magharibi.

Kampuni nne za udalali, Msolopa Investment Co. Ltd, Nakara Auction Mart na Sikonge International Co. Ltd ya Dar es Salaam na nyingine ya Dodoma Universal Trading Co. Ltd ya mkoani Dodoma zimepewa jukumu la kuwasaka wadaiwa hao.

Wengi wa wahitimu wanaodaiwa na bodi hiyo walisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

Kwa mujibu wa taarifa, wadaiwa hao wanatakiwa kuwasilisha bodi maelezo yao kuhusu mahali waliposoma, mwaka wa masomo, namba za simu na mahali wanakopatikana kwa sasa.

Baada ya muda waliopewa kumalizika, wadaiwa watalazimika kuongezewa riba ya asilimia 5 kila mwaka, gharama za kuwatafuta, majina yao yatatumwa kwenye taasisi za fedha ili kuwazuia wasipate mkopo wa aina yoyote.

Wadaiwa hao pia watazuiwa kupata ufadhili wa masomo ya juu ndani na nje ya nchi na taarifa zao zitawasilishwa Idara ya Uhamiaji na balozi zote ili wasiruhusiwe kusafiri nchi yoyote nje.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: