Rites yatengewa Sh. 31 bilioni


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 27 July 2011

Printer-friendly version
Treni ya Shirika la Reli Tanzania (TRC)

SERIKALI italipa wawekezaji wa Rites ya India mabilioni ya shilingi kwa kuvunja mkataba waliosaini Oktoba 2007 ambao uliingiza wageni hao kuendesha lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC), MwanaHALISI imegundua.

Mafao hayo yanafikia jumla ya dola 21,159,848.28 za Marekani ambazo ni sawa na Sh. 31,739,772,000 (Sh. 32 bilioni) kwa mbadilisho wa Sh. 1,500 za Tanzania kwa kila dola moja.

Mnamo mwaka 2007, serikali ya Tanzania iliingia mkataba wa miaka mitano na Rites – Rail India Technical & Economical Service – wa kuendesha lililokuwa TRC ambalo sasa linaitwa kampuni ya reli Tanzania (TRL). Rites imeuziwa hisa 51 wakati serikali imebakiwa na hisa 49.

Kulingana na nyaraka zilizopatikana na gazeti hili, mafao hayo ni mbali na hasara ya zaidi ya Sh. 98 bilioni ambazo serikali italazimika kubeba kutokana na kudhoofika kwa huduma za TRL.

Hasara hiyo imepatikana kwa miaka mitatu na nusu tu kuanzia Oktoba mosi 2007 baada ya Rites kuingia mkataba wa uendeshaji wa reli hiyo.

Mafao ambayo serikali itailipa Rites yatakuwa kwa mchanganuo ufuatao:

Nyaraka zinaonyesha mchanganuo wa malipo hayo unaanzia na dola 11,092,344 ambazo ni malipo ya kukodi injini tangu kama ilivyobainishwa kwenye mkataba mdogo wa ukodishaji huo uliosainiwa 12 Septemba 2007.

Dola 1,105,652 kwa mkataba wa kukodi mabehewa ya abiria na mizigo; dola 2,617,566.28 za Marekani zilizotumika kuajiri wataalamu mbalimbali katika kuendesha kampuni hiyo kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa 30 Agosti 2007.

Kadhalika, dola 3,976,286 kwa ajili ya ukarabati wa mabehewa 10 kati ya 73 ili kuyaweka kwenye hadhi na daraja ya juu kama makubaliano yaliyofikiwa 06 Machi 2008 huku pia dola 2,368,000 zikiwa ni malipo kwa ajili ya kukatisha mkataba ghafla.

Nyaraka zinaonyesha kuwa serikali ya Tanzania inatakiwa kulipa fedha hizo katika kipindi kinachoanzia Disemba mwaka huu mpaka Juni 2013.

Makubaliano ya kuuziana hisa kati ya serikali na Rites - Matarajio ya Serikali ya Tanzania wakati wa ukodishaji wa TRC yalikuwa ni kuimarisha sekta ya usafirishaji kwa njia ya reli kupitia utendaji wenye tija kutoka kwenye sekta binafsi.

Serikali pia ilitarajia kuwa TRL ingewekeza kwenye miundombinu ya reli, injini za treni, mabehewa na vifaa mbalimbali vya kufanyia kazi ili kuongeza uwezo na ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji kwa njia ya reli.

Hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali, matarajio ya serikali hayakutimia na TRL iliendelea kupata hasara mwaka hadi mwaka.

Taarifa ambazo MwanaHALISI imezipata zinasema mwaka 2007 TRL ilipata hasara ya Sh. 4.87 bilioni; mwaka 2008 (hasara ilikuwa Sh. bilioni 26.914; mwaka 2009 (Sh. bilioni 56.532) na mwaka 2010, mpaka kufikia Aprili, hasara ilikuwa Sh. 10.07 bilioni.

Mpango wa biashara wa Rites na TRL uliowasilishwa kwenye zabuni ya ukodishwaji ulikuwa ukieleza kuwa ifikapo mwaka 2014, watakuwa wamesafirisha mizigo tani 3.29 milioni kwa mwaka.

Katika mpango huo ambao haukufanikiwa, taarifa zinasema Rites/TRL ilipanga pia kuwa na treni sita za abiria kwa wiki kuanzia Dar es Salaam kwenda Kigoma na Mwanza.

Hata hivyo, usafirishaji wa mizigo uliendelea kushuka kutoka tani milioni 0.57 zilizosafirishwa mwaka 2007 hadi kufikia tani milioni 0.256 zilizosafirishwa mwaka 2010.

Treni za abiria kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kigoma na Mwanza zilipungua kutoka nne kwa wiki hadi kufikia moja kwa wiki kwenda Kigoma pekee mwaka jana.

Hali hii imesababishwa na kusitishwa kwa injini 25 na mabehewa 23 ya abiria yaliyokodishwa kutoka Rites, uchakavu wa injini na mabehewa vilivyorithiwa kutoka TRC, mafuriko ya Kilosa mpaka Gulwe, uchakavu wa miundombinu na migogoro ya wafanyakazi ya mara kwa mara.

Kadhalika, taarifa hizo zinasema kwamba kwa ujumla njia ya reli iliyopo sasa kwa kiasi kikubwa inajengwa na reli zenye uzito mdogo unaoanzia ratili 45 kwa yadi hadi ratili 60 kwa yadi.

“...na ni asilimia 17 tu ya mtandao wa reli ndiyo yenye reli za uzito wa ratili 80 kwa yadi. Reli hizi ndogo ni za zamani zenye umri unaozidi miaka 100,” inasema taarifa hiyo.

Vilevile madaraja mengi yana uwezo mdogo wa kubeba mzigo, na ni asilimia 18 tu ndiyo yenye uwezo wa kubeba “axle load” ya tani 25.

Hali ya miundombinu ya njia ya reli ni mbaya kiasi kwamba katika maeneo mengi mwendo kasi wa treni umepunguzwa kutoka kilometa 56 kwa saa mpaka kilometa 30 kwa saa ili kuepuka ajali zinazoweza kusababishwa na ubovu wa njia ya reli.

Katika mkataba wa ukodishaji, TRL ilitakiwa, ndani ya miaka mitano ya kwanza, kufanya matengenezo ya njia ya reli kwa kufuata Muongozo wa Uhandisi wa TRC wa mwaka 1962 – TRC Civil Engineering Manual 1962 ambao pamoja na mambo mengine unaelekeza matumizi ya wafanyakazi wanaoishi kwenye magenge kwa ajili ya kufanya matengenezo ya njia ya reli.

Bila kuzingatia masharti haya ya mkataba, TRL iliwaondoa wafanyakazi wa magengeni kwenye maeneo mengi ya njia ya reli na kuyaacha magenge yakiwa wazi.

Kutokuwa na wafanyakazi kwenye magenge kulisababisha njia kuachwa bila matengenezo kwa muda mrefu na hivyo kuwa katika hali mbaya ya ubora.

Hali hii imesababisha pia majengo ya magenge kubomolewa na mabati, milango na madirisha kuibwa. Sehemu kubwa ya njia ya reli imeachwa bila kushindiliwa kwa kokoto, kufyekwa miti na majani, kusafisha mitaro ya maji ya mvua, nk.

Mkataba wa ukodishaji uliitaka TRL pia katika miaka mitano ya kwanza, ilikuwa ni kuimarisha njia ya reli kwa kutandika reli mpya yenye uzito wa “80lb/yd” kwa umbali wa kilometa 328.

Hata hivyo, mpaka sasa ilichomudu kufanya TRL ni kutandika reli mpya kwa umbali wa kilometa 42 tu kwa kutumia reli na mataruma yaliyonunuliwa na kampuni hodhi ya huduma za reli nchini (RAHCO) kutokana na mkopo wa Benki ya Dunia.

TRL ilipoanza kazi mwaka 2007 ilikabidhiwa injini 79, mabehewa ya mizigo 1,357 na mabehewa ya abiria 97 vilivyokuwa vikitumiwa na TRC.

Katika muda wa miaka mitatu ya biashara, TRL ilitumia fedha kidogo katika kukarabati na kufanya matengenezo ya injini pamoja na mabehewa, badala yake TRL iliamua kukodisha injini za treni 25 na mabehewa 23 ya abiria kutoka India.

Kutokana na kukosa matengenezo, kati ya injini 79 zilizokabidhiwa kwa TRL, 01 Oktoba 2007 ni injini 39 tu zinazofanya kazi kwa sasa na zipo chini ya kiwango cha ubora.

MwanaHALISI limeambiwa kwamba kati ya mabehewa 1,357 ya mizigo, ni mabehewa 638 tu ndiyo yanafanya kazi na kati ya mabehewa 97 ya abiria, 45 tu ndiyo yanafanya kazi na yapo chini ya kiwango cha ubora.

“Injini 40 za treni, mabehewa 719 ya mizigo na mabehewa 52 ya abiria vilivyobaki havifanyi kazi kutokana na kutokuwepo vipuri vya kuyatengenezea,” inasema taarifa hiyo.

Kutokana na hali hiyo, haraka Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu alimwandikia barua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda tarehe 27 Aprili, mwaka huu, akiomba fedha kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kufufua reli hiyo katika mpango wa maendeleo wa mwaka 2011-2015.

Katika barua hiyo Kumb. Na. CA 98/386/01/ ya 27 Aprili 2011, ambayo MwanaHALISI imeona nakala yake, pamoja na mambo mengine, Waziri Nundu anaomba kupatiwa “bajeti ya kutosha” ili kutimiza malengo na kuwaondolea adha wananchi wanaotumia usafiri huo.

Nundu ameomba TRL pekee itengewe Sh. 95.4 bilioni, kati ya fedha hizo, Sh. 63.7 zitumike kulipia madeni mbalimbali yakiwemo ya Rites, IFC, RVR, wafanyabiashara wa nchini na mtaji wa kufanyia kazi.

TRL ilikuwa ipate fedha hizo mwaka wa fedha 2010/2011.

“Kutokana na udogo wa ceiling, naomba ofisi yako iingilie kati suala hili kwa kutafuta njia ya kutenga fedha kwa ajili ya sekta ya reli ambayo miradi yake mingi haikuwepo kwenye bajeti zilizopita kutokana na TRL kuwa chini ya menejimenti ya Rites,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Reli ya Kati ina urefu wa jumla ya kilomita 2,707 ikiunganisha mikoa 14 kati ya 24. Mtandao huu wa reli unaanzia Dar es Salaam kupitia Tabora mpaka Mwanza na Kigoma.

Reli hii inaunganishwa na reli ya Tanga-Arusha kwa reli ya Ruvu – Mruwazi. Aidha, mtandao una matawi matatu ambayo ni Kaliua-Mpanda, Manyoni-Singida na Kilosa-Kidatu.

Mtandao huu ulikuwa unamilikiwa na Serikali kuanzia mwaka 1977 kupitia iliyokuwa TRC baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.

0
No votes yet