Rosemary Kirigini: Nimekulia katika siasa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 17 June 2008

Printer-friendly version
Ana kwa Ana
Rosemary Kasimbi Kirigini

HANA majivuno. Anajiheshimu na anaheshimu wengine pia. Ni Rosemary Kasimbi Kirigini (34). Mbunge wa Bunge la Muungano kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Viti Maalum, mkoa wa Mara.

Hii ni mara yake ya kwanza kuingia bungeni, lakini ana ufahamu mkubwa ukilinganisha na baadhi ya wabunge, hasa wale wa rika lake.

Kwa wanaomfahamu wanasema, mafanikio yake yametokana na "kujiamini na kusimamia kile anachokiamini."

Hata hivyo, katika mahojiano yake na MwanaHALISI, majuzi, mjini Dodoma, Kirigini anasema mafanikio yake yametokana na kulelewa vizuri kisiasa na wazazi wake, hasa baba yake mzazi, Herman Kirigini.

"Huyu ndiye mwalimu wangu. Ndiye aliyeniingiza katika siasa. Siku zote huwa najifunza kwake na kupata ushauri wa mambo mbalimbali ya kisiasa. Hata baadhi ya kazi zangu za kibunge, huwa zinafanywa na yeye," anasema kwa taratibu.

Herman Kirigini ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe nchini. Amepata kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika serikali za awamu ya kwanza, pili na ya tatu.

Aliwahi kuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo katika serikali ya Mwalimu Julius Nyerere. Kati ya mwaka 1980 na 1985 alikuwa mbunge wa Musoma Vijijini.

Mwaka 1995 na 1998 alikuwa mkuu wa wilaya ya Kiteto mkoani Manyara. Kwa mujibu wa Rosemary, baba yake alistaafu utumishi wa umma mwaka 1998, na kwamba sasa anaishi kwa pensheni kutoka kwa watoto wake akiwamo yeye Rosemary.

Akiwa miongoni mwa wanawake wawili waliofanikiwa kuingia bungeni, kutoka katika kundi wagombea wengi waliopambanana katika mkoa wake kuwania nafasi hiyo, Kirigini anasema amejiandaa kikamilifu kuwatumikia wananchi wake.

Mbunge mwenzake wa viti maalum, katika mkoa wa Mara, ni Gaudencia Kabaka, ambaye ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Lakini siri ya nguvu yake ni nini? Anasema, "Ni kwa sababu nimeungwa mkono na wanawake wenzangu ndani ya chama changu. Mimi ni mbunge kupitia UWT (Umoja wa Wanawake wa CCM); nisingeshinda kama wenzangu wasingenikubali."

Lakini ameingiaje katika siasa? Anajibu, "Siasa imo ndani ya damu yangu. Baba yangu ni mwanasiasa, tena si mwanasiasa uchwara. Ni mwanasiasa makini na wa kupigiwa mfano.

"Mimi pia nimekuwa mwanasiasa tangu nikiwa mdogo. Nimelelewa na nimekulia ndani ya chama hiki. Nakifahamu," anasema.

Kutokana na hali hiyo, Kirigini anasema kila anayeifahamu familia yake hashangazwi na yeye kutumbikia katika siasa, maana humo ndimo alimolelewa na kukulia.

Rosemary anasema uchaguzi ulipokaribia, baadhi ya watu wanaomheshimu baba yake, walikwenda na kumuomba yeye kujitosa katika kinyang'anyiro cha ubunge katika mkoa wa Mara kupitia "sanduku la viti maalum."

Anasema ushawishi huo wa wananchi ndio uliomsukuma kujitosa katika kinyang'anyiro hicho; awali jambo hilo anasema, aliliona kuwa ni kubwa sana kwake.

"Lakini baada ya kutafakari kwa muda mrefu na kwa kina, hatimaye nilikubaliana na wazo hilo. Nikajitosa katika kinyang'anyiro na Mungu akanisaidia kupenya," anasema.

Rosemary Kirigini, alizaliwa mwaka 1974 huko Kilosa, mkoani Morogoro. Alipata elimu yake ya msingi Oyster Bay mkoani Dar es Salaam, kutoka mwaka 1981 hadi 1987.

Mwaka 1988 na 1991, Kirigini alikuwa katika shule ya Sekondari Kisutu. Alijiunga na Shule ya Sekondari Msalato, mkoani Dodoma mwaka 1993 kwa masomo ya Kidato cha Tano na Sita.

Baada ya kutoka Msalato, Kirigini alijiunga na Chuo cha Kilimo na Mifugo, Tengeru, Arusha. Alimaliza masomo yake mwaka 1998.

Anasema baada ya kumaliza masomo yake Tengeru, aliajiriwa katika kiwanda cha madawa cha Shelly's kilichoko Dar es Salaam kama Meneja Masoko. Alifanya kazi hiyo kutoka mwaka 1999 hadi mwaka 2005 alipojitumbukiza katika siasa.

Alipoulizwa kwa nini aliamua kugombea ubunge Mara, badala ya Dar es Salaam ambako ndiko alikokulia na kusomea, Kirigini alisema, "Mara ndiko nyumbani. Lakini pia, baba yangu alikuwa mbunge wa Musoma Vijijini. Niliamua kugombea huko ili kusaidiana na wazazi wangu katika kusukuma mbele maendeleo."

Anajisikiaje kuwa miongoni mwa wabunge vijana ndani ya Bunge? "Najisikia vizuri sana. Unafahamu, ukifanya kazi na wazee kama Malecela (John Samwel Malecela-Mtera CCM) na wengine wenye uzoefu wa shughuli za Bunge, na kisha wewe ukawa msikivu, hakika, unavuna mengi."

Anasema, "Ukichukua ushauri wao na kuufanyia kazi vizuri, unaweza kukupeleka mbele kisiasa na hata kimaisha. Nami hivyo ndivyo ninavyoitumia nafasi hiyo."

Kirigini anasema, awali aliona kazi ya ubunge kuwa ni kitu kigumu sana, lakini sasa hofu hiyo imeanza kuondoka, ijapokuwa anakiri kuwa kazi ya ubunge ni ngumu.

Anasema hii ni kwa sababu, kazi ya ubunge ni kazi ya utumishi; na kila mbunge anahitajika kutumia muda wake wote kutumikia wananchi.

Anasema akiwa mbunge kupitia kundi la wanawake, moja ya kazi zake kubwa alizonazo ni kuunganisha makundi ya wanawake.

Katika hilo, Kirigini anasema "naweza kusimama hadharani na kuonyesha kazi niliyoifanya." Anasema katika kipindi cha miaka miwili na nusu ya ubunge wake amejitahidi kuunganisha makundi ya wanawake na kumaliza tatizo la ukeketaji katika wilaya ya Tarime.

"Tumefanya kazi ya kuelimisha wananchi ili kuachana na mila hizi ambazo zinachangia kuwapo kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi," anasema.

Hata hivyo, anasema kuna tatizo kubwa linaloukabili mkoa wake katika kukabiliana na maambukizi ya ukwimwi nalo alisema linatokana na kuwapo kwa mfumo dume katika maeneo mengi ya nchi.

"Pamoja na kwamba wanawake ndio tunaowaelimisha juu ya hatari ya kuambukizwa, lakini mara zote uamuzi wa mwisho unakuwa wa wanaume hasa katika suala la kujamiiana salama," anafafanua.

Anasema kazi ya kuunganisha wanawake ameifanya pia katika chama chake kwa lengo la kuimarisha umoja wao.

Pamoja na udogo wake, Kirigini ndiye aliyekabidhiwa na chama chake jukumu la kuwa mlezi wa wilaya ya Tarime, ambayo ina majimbo mawili ya uchaguzi: Tarime na Rorya.

Katika kutimiza jukumu lake hilo, Kirigini anasema ameandaa mkakati kabambe wa kuhakikisha jimbo la Tarime linaloshikiliwa na upinzani linarudi mikononi mwa CCM.

Mbunge wa Tarime ni Chacha Zakayo Wangwe (Chadema), ambaye katika uchaguzi uliopita alimbwaga mshindani wake wa siku nyigi, Kisyeri Chambiri.

Hata hivyo, amekana kwamba yeye mwenyewe ndiye mwenye dhamira ya kugombea katika jimbo hilo. "Tumejiandaa kikamilifu kuhakikisha jimbo la Tarime linarudi mikononi mwa CCM," anasema.

Anasema, "lakini mimi si miongoni mwa wagombea. Sigombei, bali nataka kushiriki kukisaidia chama changu kupata mgombea mwenye sifa na atakayetuletea ushindi. Akipatikana nitamnadi kwa nguvu zangu zote."

Alipoulizwa kama chama chake kina ubavu wa kulikomboa jimbo hilo, Kirigini alisema, "Ndiyo. Mwaka 2010 Tarime na mkoa mzima wa Mara, tunataka kusiwe na mbunge wa upinzani. Hilo ndilo lengo la chama chetu."

Anasema katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, chama chake kinafanya kazi ya kumaliza makundi yaliyoota mizizi katika jimbo hilo, na ambayo yalisababishwa na ushindani wakati wa chaguzi za ndani ya chama chao.

Lakini pia wanafanya kazi ya kuhakikisha matatizo ya wachimba madini, katika machimbo ya Nyamongo, yanamalizwa.

"Tuna mkakati mkubwa. Tunaangalia kila tatizo na kulitafutia ufumbuzi. Kazi kubwa tunayoifanya ni kuweka mahusiano mema kati ya chama na wananchi," anasema na kuongeza, "bila shaka tutashinda."

0
No votes yet