Rostam ‘ajichimbia’ Ulaya


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
ROSTAM Aziz

ROSTAM Aziz, aliyejiuzulu uongozi wa siasa, ametajwa kuwa nchini Uswisi kwa kinachodaiwa kuwa “safari ya mapumziko,” MwanaHALISI limeelezwa.

Kada huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliondoka nchini siku moja baada ya kutangaza kujiuzulu ubunge na ujumbe wa halmashauri kuu ya chama chake.

Aliondokea uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam tarehe 14 Julai 2011 saa 10.40 alasiri.

Rostam alikwenda kwa ndege Na. EK 513 ya shirika la ndege la Emirates la Nchi za Falme za Kiarabu na alikuwa aunganishe safari kutoka uwanja wa ndege wa Abu Dhabi.

Taarifa za kuaminika zimeeleza kuwa kabla ya kuondoka nchini, Rostam aliandika barua kwa Spika wa Bunge la Jamhuri akimweleza juu ya hatua yake ya kujiuzulu ubunge.

Barua ya Rostam kwa Spika Anne Makinda, yenye Kumb. Na. Ig/42/2011 inaonyesha kuwa iliandikwa tarehe 15 Julai 2011, siku moja baada ya yeye kuondoka nchini.

Haikufahamika kwa nini hakupeleka barua hiyo kabla ya kuondoka nchini. Wala haijafahamika iwapo baada ya kujiuzulu hatashitakiwa kwa tuhuma za ufisadi ambazo zimekuwa zikimkabili.

Ujumbe mwingine muhimu katika barua hiyo ni kwamba anamweleza spika kuwa tayari amemjulisha rais na mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete, juu ya uamuzi wake wa kujiuzulu.

Haijafahamika pia ni kitu gani zaidi ya kujiuzulu alichoweka katika barua hiyo.

Hadi gazeti hili linakwenda mtamboni, Rais Kikwete alikuwa hajasema lolote juu ya kujiuzulu kwa kiongozi aliyefahamika kuwa mmoja wa maswahiba wake.

Kiongozi mmoja wa ngazi ya juu ndani ya CCM anasema, “Uamuzi wa Rostam kuachia nafasi zake zote za uongozi umelenga kupeleka ujumbe maalum kwa Kikwete, kwamba hakufurahishwa na hatua yake ya kumtumia Nape Nnauye kumshambulia yeye na wenzake.”

Rostam, aliyekuwa mbunge wa Igunga, mkoani Tabora kwa vipindi vitatu, alitangaza kujiuzulu Jumatano, 13 Julai 2011, katika mkutano wa ndani wa wanachama na viongozi wa CCM mjini Igunga.

MwanaHALISI limethibitishiwa na mmoja wa watu wa karibu na Rostam, kwamba siku moja kabla ya kiongozi huyo kuamua kuachia ngazi, alikuwa na mazungumzo marefu na viongozi na marafiki wake.

Miongoni mwa waliokutana naye siku hiyo ni pamoja na mmoja wa viongozi wa Umoja wa Vijana (UV-CCM), Hussein Bashe na mbunge wa Bumbuli, January Makamba.

Haikuweza kufahamika mara moja iwapo mazungumzo yalilenga kumshauri Rostam kubadili uamuzi wake.

Mazungumzo yalifanyika nyumbani kwa Rostam, jijini Dar es Salaam. Yalianza majira ya saa tatu usiku na kumalizika usiku wa manane.

Mara baada ya mkutano huo kumalizika, Makamba aliondoka kwenda mjini Dodoma, huku Bashe na Rostam wakienda Igunga ambako alitangazia kuachia ngazi.

Mtoa taarifa kwa gazeti hili amesema, “Siwezi kukueleza kwa undani kilichomo katika barua ya Rostam, lakini nakuambia yule bwana ameeleza sababu nyingine nyingi ambazo hakuzieleza katika mkutano wake wa Igunga.

Kumekuwa na taarifa za hapa na pale kutoka kwa marafiki wa Rostam zinazodai kuwa amekuwa akishambuliwa na Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye “kwa baraka za Kikwete.”

Mtoa taarifa anasema wamekuwa wakiambiwa na Rostam kuwa kila akikutana na Kikwete anaambiwa “hakuna mkakati wa kuwafukuza; hayo ni mambo ya Nape;” lakini akiondoka, anamsikia Nape akisema, “Ninafanya kazi niliyopewa na mwenyekiti (Rais Kikwete).”

Gazeti hili limepata nakala ya mazungumzo kati ya Nape na mhariri mmoja wa gazeti la Kiswahili, katika hoteli ya Movenpick jijini Dar es Salaam ambako Nape anakaririwa akisema, “Nimepewa kazi hii na Kikwete….”

Kwa mujibu wa barua yake kwa Spika Makinda, Rostam anasema amejiuzulu wadhifa wake wa ubunge “kwa sababu binafsi.”

Anasema, “Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, mimi nikiwa mgombea wa ubunge, nilitangazwa na Tume ya Uchaguzi, kuwa mbunge wa jimbo la Igunga. Kuanzia kipindi hicho hadi Julai 2011, nimekuwa nikilitumikia Bunge kama mbunge halali kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwa sababu binafsi, nimeamua kujiuzulu nafasi yangu ya ubunge. Nimefanya uamuzi huu kwa kuzingatia ibara ya 71 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Akiandika kwa njia ya kumpa taarifa bosi wake huyo wa zamani, Rostam anamweleza spika, “Kwa kuzingatia masharti hayo ya katiba, tarehe 12 Julai 2011, nimemuandikia barua mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kumjulisha rasmi uamuzi wangu huo.”

Anasema, “Ni matarajio yangu uongozi wa Chama Cha Mapinduzi kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama pamoja na masharti ya katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 71 watakujulisha rasmi uamuzi wangu wa kujiuzulu ubunge.”

Wakati mwanasiasa huyo akimuarifu Makinda kuwa amejiuzulu kwa sababu binafsi, Rostam aliwaambia wafuasi wake na baadhi ya viongozi wa chama chake mjini Igunga, kwamba kujiuzulu kwake kunatokana na kuchoshwa na alichoita “siasa uchwara” za CCM.

Wanaofuatilia msukosuko ndani ya CCM wanasema Rostam alikuwa akilenga Katibu Mwenezi Nape na naibu katibu mkuu wa CCM Bara, John Chiligati.

Viongozi hao wamekuwa wakishinikiza viongozi watatu – Rostam, Edward Lowassa na Andrew Chenge – ambao CCM inawatuhumu kwa ufisadi, kujiondoa wenyewe katika chama.

Wakati hayo yakiibuka, MwanaHALISI limeelezwa na mtoa taarifa wake kwamba kilichomsukuma Rais Kikwete kuibua ajenda ya “kujivua gamba” ni kusambaa kwa taarifa kuwa Lowassa na kundi lake walipanga “mkakati wa kumng’oa katika uongozi wa chama.”

Taarifa zinasema Kikwete alikabidhiwa ripoti inayoeleza “Mpango wa Lowassa na kundi lake” kumwengua Kikwete kwenye uchaguzi mkuu ndani ya chama utakaofanyika mwakani.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, ripoti aliyopelekewa Kikwete ililenga kumpa ujasiri wa kumweka mbali na “wabaya wake.”

MwanaHALISI lilipomuuliza Lowassa siku moja baada ya Rostam kujiuzulu kuhusu ukweli wa madai hayo, haraka alijibu, “Tutapangaje njama za kumuondoa mtu ambaye tumeshiriki kumuweka? Tufanye hivyo ili iweje?” Hata hivyo, Lowassa alikiri kupata taarifa hizo akisema ameelezwa na “msiri” wake. Amekataa kumtaja.

Wakati Kikwete anakabiliwa na mgawanyiko ndani ya chama chake, taarifa zinasema hata Afrika Kusini alikofanya ziara ya siku mbili hadi jana, kuna mgawanyiko pia katika chama cha African National Congress (ANC) cha Jacob Zuma.

Taarifa ya ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini inasema kuna tishio la kupasuka kwa chama hicho tawala; mazingira ambayo yanafanana na yale ya Tanzania.

Taarifa ya Ubalozi iliyopatikana jijini Dar es Salaam linasema kuna misuguano ndani ya chama tawala baina ya washirika wake Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (COSATU) na chama cha Kikomunisti (SACP).

Hivi sasa Afrika Kusini, kuna maandamano na migomo ya kupinga huduma duni za jamii; na kuna taarifa juu ya njama za kumuondoa Rais Zuma kutoka nafasi yake ya urais wa ANC.

Rais Kikwete atakuwa amejadili masuala haya, pamoja na mengine, yanayoweza kuingiza mitafaruku hata katika uhusiano kati ya nchi hizi mbili.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: