Rostam aanza kutikiswa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 11 August 2009

Printer-friendly version
Akutana na kigingi Igunga
Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz

ZAMA za mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kushinda kinyang'anyiro cha ubunge bila kupingwa ndani ya chama chake, sasa zimefikia tamati, imefahamika.

Anayejitosa kumaliza himaya ya Rostam ni Deusdedit Mtambalike, mkuu wa wilaya wa zamani na mwanasiasa mwenye msimamo usioyumba.

Akizungumza na MwanaHALISI kwa njia ya simu kutoka Igunga, mwishoni mwa wiki, Mtambalike alithibitisha kujitosa katika kinyang'anyiro jimboni Igunga katika uchaguzi mkuu ujao.

Amesema, "Katika hili, hakuna mwenye uwezo wa kubadilisha msimamo wangu."

Akiongea kwa kujiamini, Mtambalike alisema, "Nagombea. Huyu bwana amezoea vya bure. Nataka hela zake zitumike vizuri," alisisitiza. Alisema tayari yupo Igunga kutekeleza kile alichokiita "Mkakati wa kuwaokoa wana-Ingunga."

Rostam aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 1994 katika uchaguzi mdogo uliotokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Charles Kabeho.

Tokea wakati huo, Rostam amekuwa akijijengea utamaduni wa kupita bila kupingwa katika uchaguzi, ndani na nje ya chama chake.

Mtambile ambaye ni hasimu mkuu wa kundi la watuhumiwa ufisadi, amekuwa akitajwa kuwa ni mwiba mkubwa kwa Rostam, kutokana na kukubalika kwake ndani ya Igunga.

Mbali ya kuwa ni mwenyeji wa huko kwa asilimia mia moja, Mtambalike ana uwezo mkubwa wa kujieleza na kujenga hoja, ikiwamo kuzungumza kwa ufasaha lugha ya Kinyamwezi ambayo ni maarufu katika eneo hilo.

Akizungumza kwa kujiamini, Mtambalike alisema, "Mwaka 2000 nilitaka kugombea, akaniomba nimuachie. Akasema hatagombea tena katika uchaguzi wa mwaka 2005. Nikamkubalia," alisema.

Alisema, "Lakini ilipofika mwaka 2005, Rostam akawachezea wananchi wa Igunga baada ya kubadilika na kuamua kuchukua fomu za kuwania nafasi hii. Safari hii, nimekuja kufuta umungu mtu wa bwana huyu."

Anasema amejipima na ameona kuwa anazo sifa zote zinazohitajika na kwamba yeye ni zaidi ya Rostam. "Unazungumzia sifa za uongozi, mimi ninazo nyingi. Mimi ni mwadilifu na mwaminifu kwa taifa langu. Hii ni sifa kubwa ya kukabidhiwa jukumu hili," anasema.

Mtambalike anasema, tofuati na miaka ya nyuma, uchaguzi wa mwaka ujao, utakuwa mgumu kwa Rostam kutokana na wana-CCM wengi kuutamani ubunge wake.

"Safari hii, mambo hayatakuwa mazuri kwa ndugu yangu. Tuko wanachama wengi wa CCM tuliojitokeza kutaka nafasi hii," alisema.

Alipoulizwa amejiaandaa vipi kukabiliana na kigogo huyo aliyekwisha jigamba kuwa miongoni mwa "wafanyabiashara wakubwa," Mtambalike alijibu haraka, "Nimejiandaa vya kutosha. Sina fedha, lakini nina watu."

Alisema, "Hapa ndiyo nyumbani kwetu. Nimezaliwa hapa. Nimekulia hapa. Karibu wapigakura wote wananifahamu, nami nawajua na kuwaheshimu. Sasa unataka nijiandae na nini zaidi ya kuwa mwadilifu," alijigamba.

Alipong'ang'anizwa kwamba Rostam anajua iwapo yeye Mtambalike atagombea ubunge katika jimbo hilo alisema, "Bila shaka anajua."

Alipoulizwa Rostam anajuaje wakati yeye hajamwambia, Mtambalike alisema, "Nakwambia anajua. Anajua kwa sababu, wapambe wake wako hapa na wananiona napita vijijini kukutana na marafiki zangu kwa ajili ya kuweka mambo sawa."

"Nakwambia anajua, lakini hana la kufanya. Hapa ninapozungumza na wewe niko Igunga, tena vijijini kabisa nakutana na marafiki zangu. Watu wake wako hapa, wananiona na wengine nimewaambia hata mimi mwenyewe, kwamba katika uchaguzi ujao, hapa hapatatosha," alisema.

Taarifa kutoka Igunga zinasema, hali ya kisiasa ya Rostam imeanza kuwa ya mashaka katika siku za hivi karibuni, hasa baada ya Kanisa Katoliki kusambaza waraka unaotoa wito kwa wananchi kujadili wale wanaotaka kuwachagua kuwa viongozi wao.

Kutajwa kwa Rostam katika mahusiano mbalimbali ya biashara na mikataba yenye utata nchini, kunaweza kuzaa maoni toauti katika mijadala juu ya wanaotakiwa kuchaguliwa kuwa viongozi.

Rostam amewahi kunukuliwa akisema hatagombea tena ubunge wa Igunga, ingawa taarifa za hivi karibu zimesema amebadili msimamo wake huo na kwamba tayari ameweka makakati wa kutetea kiti chake.

Mtu mwingine anayetajwa kugombea ubunge Igunga, ni Peter Kafumu, Kamishna wa Madini katika Wizara ya Nishati na Madini.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: