Rostam aiweka serikali mfukoni


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version
Mwakilishi wa Dowans, Rostam Aziz

ANAYEJIITA mmiliki wa makampuni ya Dowans ametua nchini kibabe kwa shabaha ya kutisha serikali, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema, iwapo atashindwa kupandikiza woga, basi atatafuta “urafiki” na kuomba mitambo ya Dowans ianze upya kutoa umeme “kwa gharama zozote zile.”

Hii ni mara ya kwanza tangu nchi hii ipate uhuru, kwa anayeitwa “mwekezaji” kutaka kutunishia serikali misuli kwa manufaa binafsi na yanayolenga kuidhalilisha.

Brigedia Mohammed Yahya Al Adawi, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita kuwa yeye ndiye mwenye hisa kubwa katika makampuni ya Dowans Holdings S.A na Dowans Tanzania Ltd.

Ofisa wa ngazi ya juu serikalini ameliambia MwanaHALISI kuwa Al Adawi ameingia nchini kwa dhamira mbili kuu: Kwanza, kuhakikisha majenereta ya Dowans yanawashwa na kununuliwa na serikali.

Pili, kuhakikisha kuwa kampuni ya Dowans iliyorithi mkataba wa kampuni feki ya Richmond Development Company LLC, na baadaye kuunganishwa na Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO), inafunga mkataba wa kuiuzia umeme serikali.

Ubabe wa “mjasiriamali” wa kiarabu ulianza alipotua nchini kwa kuamuru waandishi wa habari wasijaribu kumpiga picha. Alidai kuwa hana utamaduni wa kuonekana kwenye vyombo vya habari, ingawa amejigamba ni “mfanyabiashara mkubwa duniani.”

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari vilivyoteuliwa rasmi (MwanaHALISI likiachwa), Al Adawi alisema, "Nimekuja kuondoa mashaka yaliyopo hivi sasa kuhusu umiliki wa Dowans na kuangalia kama nitaweza kushirikiana na serikali kuondoa tatizo la umeme nchini."

Hata hivyo, waziri mmoja mwandamizi ndani ya serikali aliyeongea kwa sharti la kutotajwa jina gazetini amesema, “Huyu bwana anaonekana amekuja nchini kutisha serikali. Ndiyo maana anasema lazima serikali inunue mitambo yake au ifunge mkataba.”

Akiongea kwa sauti inayoonyesha jazba, waziri huyo aliliambia gazeti hili, “Eti anadai hukumu ya mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara (ICC), haiwezi kupingwa. Huu ni uwongo mtupu. Nakuambia hakuna mwenye ubavu wa kumtisha rais wala raia wa nchi hii kwa kutaka kufanikisha mradi binafsi.”

Kujitumbukiza kwa Al Adawi kwenye sakata la Dowans katika “dakika hizi za lala salama,” kumekuja mwezi mmoja tangu gazeti hili kuripoti kwa ufasaha kuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rostam Aziz, ndiye alishitaki serikali na ndiye anaidai Sh. 94 bilioni katika kesi ya Dowans.

Rostam anatajwa na ICC kupewa nguvu ya kisheria (Power of Attorney) ya kuajiri na kufukuza; kushitaki, kudai fedha za kampuni, kufunga na kufungua akaunti za benki za kampuni hiyo na kununua au kuuza hisa pale atakapoona inafaa.

Taarifa zinasema hata kuja kwa Al Adawi nchini kumetokana na wito wa Rostam ambaye wachambuzi wa mambo wanasema, tayari maji “yalizidi unga.” Mbunge mmoja wa Bunge la Muungano alimnukuu Rostam Aziz, wiki mbili zilizopita akisema, “Hapa lazima nimlete mmiliki wa Dowans. Vinginevyo, huko ninakopita, watu watanipiga mawe.”

Al Adawi amekuja nchini wakati kuna taarifa kuwa kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika hivi karibuni, chini ya Rais Kikwete, kiliamua serikali, ama inunue mitambo mipya au ipate ya kukodisha.

Taarifa za ndani ya baraza la mawaziri zinasema mitambo mipya ya kuzalisha umeme ambayo ilikadiriwa kugharimu dola 200 milioni, wakati mitambo ya kukodi – yenye uwezo huohuo wa kuzalisha megawati 240, na ambayo iliwasilishwa na waziri William Ngeleja, inagharimu dola 500 milioni.

Mtoa taarifa amesema wajumbe wa kikao walitofautiana kuhusu kukodisha mitambo ambako kulikuwa ghali kuliko kununua mipya, lakini rais aliagiza “waangalie utaratibu unaofaa.”

Tangu kamati ya kudumu ya bunge ya Nishati na Madini ishikwe na Januari Makamba, kumekuwa na juhudi za kutimiza matakwa ya wanaotaka ama kukodisha au kununua mitambo chakavu ya Dowans.

Taarifa zilizopatikana juzi Jumatatu usiku zilisema wakati Makamba alitaka hoja ya kuanza kutumia mitambo ya Dowans wiki ijayo, baadhi ya wajumbe wa kamati yake wamesema hilo haliwezekani kwa vile wanafungwa na azimio la bunge. Wametaka suala hilo lirejeshwe bungeni ili kupata idhini.

Naye Al Adawi ameanza kujikanyaga. Aliwaambia waandishi wa habari kuwa Dowans ilipata mkataba huo baada ya TANESCO kuridhia. Lakini taarifa zinaonyesha kuwa Dowans ilipokuwa inafunga mkataba na Richmond, TANESCO hawakuwa wanafahamu lolote kuhusu suala hilo.

Mkataba kati ya TANESCO na Richmond ulihamishwa kwa Dowans, 14 Oktoba 2006, bila ya kushirikisha shirika hilo. Kifungu 15.12 cha mkataba uliosainiwa kati ya TANESCO na Richmond, 23 Juni 2006, kinakataza wabia hao wawili kuhamisha jukumu lolote linalohusu mkataba huo pasipo makubaliano, tena kwa maandishi kati ya pande hizo mbili.

Taarifa zinaonyesha 4 Desemba 2006, aliyekuwa waziri wa nishati na Madini, Nazir Karamagi alieleza TANESCO kuwa alipokea “barua ya Richmond ya kutaka kuhamisha mkataba wake; tarehe ambayo TANESCO itaridhia mapendekezo hayo iwe ndiyo tarehe rasmi ya kuhamishia mafao na majukumu yote kwa Dowans Holdings, S.A.”

Katika maelezo yake, Al Adawi anasema kampuni yake ilikuja kuondoa tatizo la uhaba wa umeme, lakini papohapo anakiri kuwa wakati mitambo ya Dowans inaletwa nchini, tatizo la uhaba wa umeme lilikwishamalizika.

MwanaHALISI lilipowasiliana na spika wa zamani wa Bunge la Muungano, Samwel Sitta, ambaye yuko nchini India kikazi, kuhusiana na kauli ya Al Adawi ya kujiita mwekezaji, kwanza alicheka. Kisha akasema, “Kama huyu anajiita mwekezaji, basi Tanzania haihitaji mwekezaji wa aina hii.”

Sitta ambaye ni waziri wa Afrika Mashariki aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kwa miaka kumi mfululizo alisema, “Kwanza hiki kiburi alichoonyesha na ubabe, kinatosha kumfukuzisha nchini. Hawezi kujiita mwekezaji, wakati yeye amekuja nchini kulangua umeme kwa kukodisha mitambo yake na kisha anaondoka. Je, huu nao ni uwekezaji?” alihoji.

Sitta alisema kwa njia ya simu, “Tanzania inahitaji wawekezaji katika miradi mikubwa ya kilimo, ufugaji na uvuvi, badala ya ubabaishaji kama huu.”

Akiongea kwa kujiamini Sitta alisema, “Huyu bwana mmemuuliza ameleta mtaji kiasi gani? Huyu si ameleta majenereta ya kukodisha na kuondoka tu?” ameuliza.

Kilichoshangaza wengi ni majigambo ya Al Adawi kuwa ni mfanyabiashara wa kimataifa mwenye wafanyakazi 25,000 duniani lakini anaogopa kupigwa picha.

Mmoja wa waandishi waliokatazwa kupiga picha aliliambia gazeti hili kuwa picha hizo zingesaidia Rais Kikwete kumfahamu bosi wa Rostam Aziz, ambaye kwa pamoja, wameshitaki TANESCO na wanadai Sh. 94 bilioni (au Sh. 2,350 kwa kila Mtanzania hivi sasa na bila kujali umri wake).

Rais Kikwete alisema tarehe 5 mwezi huu kuwa hajui wamiliki wa Dowans wakati mwenye madaraka ya kuwakilisha kampuni hiyo ni rafiki yake, mbunge wa Igunga, mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama chake.

Akihutubia katika maadhimisho ya miaka 34 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kikwete alisema, “simfahamu mmiliki wa Dowans, simjui na wala sijawahi kukutana naye” na kwamba hana hisa katika kampuni hiyo.

Wakati Al Adawi anajigamba kuwa na uzoefu katika bishara ya kuzalisha umeme, majaji wa ICC walieleza kuwa Dowans, hadi wanaanza kuzalisha umeme jijini Dar es Salaam, hawakuwa na biashara yoyote duniani.

Mbunge mmoja kutoka Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini amelieleza gazeti hili, “Bwana huyu alikuja hapa kuwekeza katika mradi wa mkonga wa mawasiliano. Alifanya lini upembuzi yakinifu kuhusu mahitaji ya umeme na faida atakayoipata?”

Al Adawi alipoulizwa ilikuwaje mfanyakazi wa Caspian Henry Surtees, akasafiri hadi Marekani kuonana na utawala wa kampuni ya Richmond, aligeuka mbogo na kusema hakuja nchini kuzungumzia mambo ya Caspian.

Alipoelezwa kuwa pamoja na hayo aliyekwenda Marekani kuwaona Richmond ni mtumishi wa Caspian, Al Adawi alisema kuwa alikuwa amemruhusu Rostam Aziz kufanya kazi zake akiwa amempa mamlaka ya kisheria na kwamba alitaka awe na mamlaka ya kutosha kuiwakilisha kampuni yake.

Al Adawi alisema alitumia dola milioni 109 (zaidi ya Sh. 109 bilioni  wakati huo) kununua mitambo ya Dowans. Alisema gharama nyingine zote za kuanzisha mradi huo zilitoka kwenye kundi la makampuni yake.

Nyaraka za benki zinaonyesha Aprili 30 na 9 Novemba 2007, miezi michache baada ya kuhamisha mkataba kutoka Richmond, Dowans Tanzania Limited ilikopa dola 70 milioni (karibu Sh. 98.6 bilioni) katika benki mbili tofauti za Barclays na Stanbic  kwa kuifanya mitambo yake ya Ubungo kuwa dhamana.

Hadi tunakwenda mitamboni juzi Jumatatu, maofisa wa benki waligoma kuzungumzia uhai wa deni hilo. Katika mazingira haya, serikali ikinunua mitambo ya Dowans, na kama deni halijalipwa, basi mitambo inaweza kukamatwa na benki.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: